Prime
Kunani ongezeko la mauaji ndani ya familia

Muktasari:
- Ndani ya siku 45 za kwanza 2025 matukio tisa yameripotiwa na Mwananchi, wadau wataja tatizo la afya ya akili kama moja ya sababu.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wapendanao (Valentine’s) leo Februari 14, 2025 inaonekana dhahiri kukosekana upendo kunaifanya taasisi ya familia kutikitikisa kutokana na matukio ya mauaji yanayoindama
Katika miaka ya karibuni imebainika kuwepo ongezeko la mauaji yanayofanyika ndani ya familia, huku wivu wa mapenzi, tatizo la afya ya akili na ukosefu wa upendo vikitajwa kuchangia hali hiyo, wahusika wakiwa wanafamilia wenyewe.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi kupitia taarifa zilizochapishwa gazetini na kwenye majukwaa yake ya kidijitali katika kipindi cha siku 45 tangu kuanza mwaka 2025, umebaini matukio 10 ya mauaji yameripotiwa, yakiwemo yanayohusisha wenza na watu wa familia moja.
Wadau waliozungumza na Mwananchi wametaja sababu mbalimbali zinazochangia matukio ya mauaji hayo na kupendekeza suluhisho lake.
Mkurugenzi wa programu katika asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Morice Lekule amesema kiini cha tatizo hilo ni watu kukosa upendo.
“Siku hizi watu wamegeuza upendo kuwa utumwa, furaha yako inategemea mtu mwingine, unataka yeye akupende, ikitokea mambo yamekwenda tofauti unakuwa tayari kumuua na wengine wanajiua, hili ni tatizo.
“Tukiacha kutegemea kupata furaha na amani kutoka kwa watu wengine, haya mambo ya mauaji yatapungua. Anza kujipenda mwenyewe, ukijipenda hata huwezi kufikiria kumdhuru mwingine wala kujidhuru kwa sababu utafahamu athari zake,” amesema Februari 13, 2025 alipozungumza na Mwananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka amesema kinachosababisha mauaji kuendelea kutikisa kwenye taasisi ya familia ni matokeo ya watu kukosa hofu ya Mungu.
“Mtu mwenye hofu ya Mungu hawezi kufanya vitu ambavyo vitamuumiza mwenzake, sasa hivi watu si waaminifu, usaliti umechukua nafasi kubwa kwenye uhusiano na watu hawaishi kwenye uhalisia. Sasa kama haya yanatokea kwenye uhusiano, lolote la hatari linaweza kutokea.
“Hatari hiyo inatokea pale kunapokosekana hofu ya Mungu, endapo utafikiri kuhusu ukuu wa Mungu na mambo anayokataza basi utaachana na mawazo ya kumdhuru au kumuua aliyekusaliti au kukutenda visivyo, badala yake utaomba hekima,” amesema.
Rustika Tembele, anayejihusisha na utoaji elimu kuhusu changamoto ya afya ya akili amesema mauaji hayo yanachangiwa na tatizo hilo, ambalo wengi hawafahamu kuwa wanalo.
“Tatizo la afya ya akili ni kubwa lakini hatujachukua hatua madhubuti kukabiliana nalo, watu hawajui hali zao na hata wale wanaojua wanashindwa kuzungumza kwa sababu ya kuhofia unyanyapaa. Matokeo ya hili ni watu kukosa sehemu ya kupumulia changamoto wanazokabiliana nazo, hivyo kuishia kufanya mambo yasiyofaa.
“Mtu anarundika mambo kichwani, hana wa kuzungumza naye. Inapofika siku yamelipuka ndipo inamsukuma kufanya chochote bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza. Tusipojipanga vyema kama taifa matukio ya aina hii yataendelea kutusumbua,” anasema.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Amani Saadat, ambaye pia anajishughulisha na masuala hayo. Anasema ipo haja ua kufanyika uwekezaji kuhakikisha elimu ya afya ya akili inawafikia Watanzania wote.
“Ifike mahali suala hili tulichukulie kwa uzito, elimu kuhusu afya ya akili iwe kitu cha lazima kwa kila Mtanzania, ili mtu ajue hali yake na kama ana changamoto apate msaada, asionekane wa ajabu kwenye jamii,” amesema.
Watafiti katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) wamethibitisha kuwepo uhusiano wa kisayansi wa matatizo ya afya ya akili na vitendo vya ukatili.
Mfululizo wa tafiti zilizofanywa na idara ya magonjwa ya akili umethibitisha hilo, huku kukiwa na wasiwasi kuwa hatua zisipochukuliwa hali itakuwa mbaya zaidi kutokana na kuwepo watu wengi wenye matatizo ya afya ya akili bila wao wenyewe kujitambua.
Hadi sasa inaonekana ni asilimia 20 pekee ya wenye matatizo ya afya ya akili, ndio hutafuta matibabu, huku asilimia 80 iliyobaki wakiwa hawajitambui na hata wanaojitambua wanatafuta tiba mbadala, ikiwemo dawa za kienyeji na maombi kwenye nyumba za ibada.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Ester Mzilangwe amesema ukatili unaosababishwa na tatizo la afya ya akili unazidi kuongezeka kutokana na watu wengi wenye matatizo hayo kutoelewa hali zao.
Amebainisha kuwa wengi wanaofanya vitendo vya ukatili kwa ama kuwashambulia, kuwadhuru wengine au hata kujidhuru wenyewe, ni matokeo ya kukosa utatuzi au ufumbuzi wa changamato zinazowakabili.
Nini kinaendelea kwenye ubongo wa mtu anayefikia kuua?
Dk Ester amesema wapo ambao tayari wana ugonjwa wa akili unaomsukuma kujihami dhidi ya mtu mwingine anapohisi anataka kufanyiwa kitu kibaya na hilo hutokea mara chache.
Amesema hali hiyo hutokana na kutokuwepo mawasiliano yanayotengenezwa kupitia mazungumzo na makubaliano ya wenza wenyewe kwa kila mmoja kumwelewa mwenzake.
“Kwenye uhusiano kitu kikubwa ni mawasiliano, lakini unakuta wengine hawana namna nzuri ya kuweka mawazo yao yaeleweke kwa wenza wao na hana uwezo wa kukabiliana na hasira, hapa ndipo kila mmoja atashika njia yake na kufanya kila anachoona ni sawa kwake.
“Kisaikolojia hakuna anayeibuka ghafla siku moja na kufanya tukio kubwa la ukatili. Tabia inaanza kidogo kidogo, ukifuatilia yalipotokea matukio ya ukatili kwa wenza utagundua haikuanzia siku hiyo, yanaanza taratibu na hatua zisipochukuliwa itaonekana kawaida na anayefanya hivyo ataongeza kile anachofanya,” amesema.
Matukio Januari, Februari
Januari 11, 2025 katika Kitongoji cha Maweni A wilayani Babati, Shaban Rajabu alimuua kwa kumchinja na kumkatakata mkewe, Zulfa Rajabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi mwili wa Zulfa ulikutwa na majeraha, ikielezwa wawili hao walikuwa na ugomvi.
Siku hiyohiyo iliripotiwa kuwa mkazi wa Kijiji cha Namsinde, Kata ya Mkulwe mkoani Songwe, Junge Jilatu alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwaua watoto wake wawili.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augustino Senga alisema mwanamke huyo aliwakaba watoto hao wakiwa wamelala na kuwakata kwa kitu chenye ncha kali shingoni, kisha mmoja wa watoto hao alimtupa kwenye mtaro wa maji kandoni mwa barabara.
Januari 13, 2025 mwanamke mmoja alituhumiwa kumnyonga mtoto wake wa siku 21 kisha kuutekeleza mwili wake pembezoni mwa Mto Ngarenairobi wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, chanzo kikidaiwa ni ugumu wa maisha baada ya kutekelezwa na mwanaume aliyempa ujauzito.
Januari 27, 2025, Mashaka Sichone, mkazi wa Wilaya ya Kalambo aliuawa kwa kukatwa kichwa akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina na kumuua baba yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija alisema watuhumiwa wa tukio hilo la mauaji ni ndugu wa Sichone, waliokuwa wakimtuhumu kumuua baba yao mzazi kwa kutumia ushirikina.
Januari 27, 2025 Eliherema Mollel (32) alijinyonga kwa kile kinachodaiwa kuachwa na mpenzi wake ambaye ni mwanafunzi wa chuo. Mwili wake ulikutwa ukining’inia katika nyumba aliyokuwa akiishi akiwa ameacha ujumbe ulioleza ameamua kujiua, mpenzi wake asilaumiwe kwa chochote.
Februari 4, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema mwanafunzi wa kidato cha tano Benadeta Silvester (21), alifariki dunia baada ya kukabwa koo na mpenzi wake Adamu Kailanga (30) kisha naye kujinyonga ikidaiwa ni kutokana na wivu wa mapenzi.
Februari 9, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu alisema Maimuna Suleiman Said (38) Mkazi wa Chukwani, Zanzibar alijeruhiwa kwa kukatwakatwa kwa kisu mwilini na Khadija Ali Shaaban (34), ambaye ni mke mwenza sababu ikitajwa wivu wa mapenzi.
Februari 10, 2025 Abdallah Mohamed alimuua mzazi mwenzake Naomi Mwakajengele, mwalimu wa Shule ya Msingi Mataya, iliyo Kata ya Kiromo wilayani Bagamoyo.
Polisi ilisema uchunguzi wa awali ulibaini alichomwa na kitu chenye ncha ubavuni na kwenye chemba ya moyo.