KONA YA WASTAAFU: Kuna maisha mengine baada ya kustaafu

Muktasari:
- Ili kuepusha Kona ya Wastaafu kuaminisha watu kwamba maisha ya ustaafu ni ya tabu, ni kuwapa moyo wastaafu watarajiwa.
Ili kuepusha Kona ya Wastaafu kuaminisha watu kwamba maisha ya ustaafu ni ya tabu, ni kuwapa moyo wastaafu watarajiwa.
Mzee wetu mstaafu anahisi itakuwa jambo jema kuelezea chembechembe za furaha zinazoibuka mara chache kwenye maisha ya ustaafu na kuwapa faraja.
Anaamini hili litasaidia pia kuwatoa hofu wastaafu na watumbuliwa watarajiwa na kuwapa matumaini kuwa ustaafu sio mwisho wa maisha.
Kuna fursa nyingi baada ya mtu kustaafu, kwa maana hiyo hakuna haja ya mtu kujipunguza umri ili aendelee kubaki kwenye ajira na katika kufanya hivyo, anaziba nafasi ya mjukuu wake aliyemaliza chuo lakini ana miaka mitano anamaliza soli za viatu barabarani akitafuta ajira ambayo imekaliwa na babu yake!
Huyu ni yule babu ambaye ana miaka zaidi ya tisa sasa kwenye ajira ya umri wa kustaafu.
Kwa mujibu wa sheria kustaafu ni miaka 60, lakini kwake kila mwaka unarudi nyuma!
Mwaka jana 2020 alikuwa na miaka 59 iliyompasa mwaka huu kustaafu kwa mujibu wa sheria za kazi, mwaka huu faili lake na nyaraka zake nyingine zote za kiofisi ghafla zinasoma kuwa ana miaka 51 na anatakiwa kustaafu miaka minne ijayo kwa hiari!
Ndiyo, unaingia ofisini unamkuta mtu mzima ambaye sura yake inaonyesha dhahiri kuwa anapaswa kuwa Jumba la Makumbusho anadonoa kompyuta, kwa maana halisi ya kudonoa, wakati barabarani huko kuna wajukuu zetu ambao wana vyeti vyote kuhusu matumizi ya kompyuta na vidole vyao vya mikono ni kama kifaa cha ziada cha kompyuta kutokana na kasi na ujuzi wa kuitumia, wanatafuta ajira!
Tuendelee. Mzee wetu mstaafu anakiri katika miaka yake 40 ya ajira iliyotukuka hakupata kupanda cheo ambacho kingeweza kumfanya aandike barua nyumbani.
Hajapata kujua sababu ya hili, maana kazi alikuwa anaifanya inavyotakiwa tena kwa kujiongeza.
Akipewa kazi moja ya kufanya na mkuu wake wa kazi, akawa akijiongeza na kufanya kumi na moja kwa kile alichodani kuwa ni kuwafurahisha wakuu wake wa kazi, lakini bado vyeo akaishia kuvisikia redioni tu hadi anastaafu!
Huwa anaishia kuhisi mambo mawili ambayo yangeweza kuwa ndio yalisababisha hili. Mdomo wake ambao aliupa uhuru wa kutetea kile alichoamini na kukisimamia hata kama sio walichoamini viongozi wake.
Na hili lilitokea kwa mengi. Au pengine ilikuwa ni kwa sababu tu, ulimi wake haukuwa na urefu na upana wa kutosha kulamba viatu vya watu waliokuwa na kauli ya mwisho linapokuja suala la yeye kupanda cheo!
Inawezekana pia ni kwa sababu mstaafu wetu hakupata kumiliki vyeti vya elimu vya uhakika vyenye hadhi ya kutundikwa ukutani ili kuwapiga mkwara wageni wake kuhusu elimu aliyonayo! Ni bahati mbaya tu, mzee wetu alianza ajira nyakati zile ambazo vyeti vya kumaliza kidato cha nne viliishapoteza hadhi ya kutundikwa ukutani tena! Mzee wetu mstaafu anasema aliishia kutundika ukutani kacheti kake alikopata baada ya kuhudhuria semina ya miezi sita kuhusu huduma kwa wateja ambayo kwa kuipandisha chati tunaiita ‘Customer Care.’
Kacheti kake hakakudumu kuwaringishia watu ukutani kutokana na timu ya wastaafu tayari wana vyeti viwili vitatu hata kama sio vyenye hadhi ya kutundikwa ukutani, wala hawakujisumbua hata kumuuliza tu baba yao. Alikuta tu cheti chake cha ‘Customer Care’ kimeondolewa ukutani na kuwekwa ghalani!
Sawa, mzee wetu mstaafu hakupata cheo chote cha kueleweka katika miaka yake 40 ya ajira ya kutukuka. Shuhudia sasa maajabu ya Mungu yanayomfanya sasa apate hata ushujaa wa kuweza kusema “Ustaafu sio mwisho wa maisha” na hakuna haja ya mstaafu kusogeza mbele umri wake wa kustaafu kwa sababu kuna maisha baada ya ustaafu!
Mzee wetu mstaafu anasema hata hakumbuki sasa ni vyeo vingapi ameishapewa na jamii aliyomo na vinamfuata hapa hapa nyumbani akiwa anafaidi ustaaafu wake, bila kuomba kazi wala kuwa hata na haja ya kutundika kacheti kake ka ‘Msomi wa Costumer Care’ ukutani. Uzoefu, umri na sura yake tu iliyokakamaa kwa uzee ni ‘vyeti’ tosha vya kupewa cheo na jamii aliyomo!
Mzee wetu hata hakumbuki kama ni mjumbe au mwenyekiti wa kamati ipi na ipi ya mtaa anaopumzisha mbavu zake. Kutoka mwenyekiti au mjumbe wa kamati ya mtaa ya maji, ulinzi au usafi hadi ya nidhamu na usuluhishi ya wana mtaa.
chesimpilipili@gmail.com
0754 340606 / 0784 340606