KONA YA MSTAAFU: Siku ya wajinga inapowafikirisha wastaafu
Inaelezwa kuwa pamoja na Umoja wa Mataifa (UN) kupenda sana kugawa siku maalumu kwa jamii kwa ajili ya kuadhimisha jambo au kitu fulani kwenye jamii hiyo, kama siku ya choo au siku ya kunawa mikono, haikugawa Aprili mosi ya kila mwaka kuwa siku ya wajinga.
Labda wajinga walianza kuwepo mwaka 1786 watu wa huko dunia ya kwanza walipoanza kufanyiana mizaha na kutaniana na kuifanya siku hiyo kuwa rasmi siku ya kufanyiana mizaha kutaniana na kuongopeana. siku ya wajinga duniani ikashika kasi.
Tuliamka tu miaka hiyo na kukuta wazazi wetu, kaka na dada zetu wakiisherehekea siku hiyo pakubwa, japokuwa siku hizi imepungua kashi kashi zake; lakini bado inasumbua sana kama mwaka ulee gazeti moja kubwa lilipoandika habari kwa maandishi makubwa ukurasa wa mbele' kuwa 'Serikali kuhamishia Mlima Kilimanjaro kuja Dar!'
Tukaamini, na ilikuwa patashika ya nguo kuchanika siku nzima ile tukiipitisha kwa kubishana kiasi cha kutiana makonzi kueleza jinsi Serikali itakavyousafirisha Mlima ule hadi Dar, enzi hizo gazeti likiwa chombo muhimu sana cha habari! Kweli tulikuwa mazumbukuku! Kesho yake gazeti lile lilipoandika kuwa ilikuwa siku wa wajinga, tukaishia kucheka na kujiona mazumbukuku kweli!
Mwanzoni mwa wiki hii ilikuwa Siku ya Wajinga. Mstaafu alikuwa hata ameisahau siku hiyo, maana hata wajukuu zake hawaijui wala kuiadhimisha kama tulivyofanya sisi enzi zile. Sasa hivi wajukuu zangu wanakumbuka zaidi Siku ya Wapendanao' na Siku ya Choo, Sio Siku ya Wajinga
Mstaafu hakuikumbuka Siku ya Wajinga lakini akajiona sasa kuna watu wanamfanya mjingakila siku na ustaafu wake baada ya miaka 40 ya kulitumikia Taifa lake kwa jasho na damu yake, lakini anapoona wenye meno ndio wanaitafuna nchi huku yeye aliyekuwa na moyo wa kuijenga nchi anaishia kuambiwa hapaswi kutafuna keki ya Taifa maana ana kisukari...
... lakini wazee wanaomzidi wanatafuna mapande ya keki ya Taifa kama hakuna kesho, na kisukari kikijaribu tu 'kujiunga' nao, fasta kinapelekwa India, Uingereza ama Ujerumani, siyo Muhimbili. Kinaambiwa kitulize boli watu wanataka kuihomola keki ya Taifa. Siyo Mstaafu. Laki mbili na nusu zake zinamtosha!
Mstaafu amefanya kazi ya kulijenga Taifa hili kwa jasho na damu yake kwa miaka 40, huku miaka yote hiyo akikatwa kwenye mshahara wake akiaminishwa kuwa ni akiba yake ya uzeeni atakayoifaidi akistaafu, miaka 40 ijayo!
Miaka 40 ilipofika akaishia kulipwa kiinua mgongo cha shilingi 31 milioni baada ya kazi ngumu ya kulijenga Taifa kwa miiaka 40. Pensheni yake ikawa Shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi. Ile 'atakayoifaidi' alivyoambia wakati akianza kazi miaka 40 iliyopita, ikachapa lapa na sikukuu zake za mjinga zikaanzia hapa!
Kibubu kilichomtunzia akiba yake uzeeni kikajiongeza, bila kutuuliza sisi wenye hela zetu na ghafla kikawa kampuni ya jenzi ikijenga majengo makubwa ya ghorofa kwenye mikoa yote nchini kikiyauza na kuyakodisha kwa bei iliyotukuka bila kutwambia chochote sisi wenye hela zetu, kuhusu walichokuwa wakipata kwenye kodi na mauzo hayo.
Kibubu kikaikopesha hata siri- kali kujenga madaraja makubwa na siri-kali ilipojitutumua kulipa mikopo hiyo, sisi wenye hela zetu hatukupata chochote na hela za malipo hayo wala hatukuambiwa zilikoishia! Tukabaki na laki moja na elfu tano zetu. Siku ya wajinga inazidi kunoga.
Mwezi Desemba mwaka jana kibubu cha akiba yetu au siri-kali kikatuongeza pensheni iwe shilingi laki mbili na elfu hamsini kutoka shilingi laki moja na elfu tano tulizokuwa tukipata kwa miaka 21 huku majengo yakikodishwa na kupigwa bei, lakini wenye hela zetu hakuna tunachopata. Kibubu kinajua zaidi kutuhakiki kuliko kutulipa hela yetu waliyofanyia biashara.
Ni sikukuu za wajinga. Hakuna matibabu ya bure, hakuna benki ndogo kwa wastaafu ili waweze kukopa kununua dawa kwa ajili ya magonjwa ya kizee yanayoshika kasi zaidi ukishastaafu. Wala hakuna hela yoyote tunayopata kutokana na hela yetu iliyotumika kujenga na kuuza majengo haya, na tunahishia kulipwa na kibubu chetu shilingi milioni tano na laki tano tukishafariki...sio tukiwa hai.
Lakini kama alivyosema yule kuli kwenye sentensi ya mwisho kabisa ya kitabu chake zha Kuli...'Yana mwisho haya'... Ujinga una mwisho. Gen-O inatuhusu wastaafu.
0754 340606 / 0784 340606