KNCU yatakiwa kuweka mkaguzi wa awali wa mahesabu kudhibiti matumizi mabaya ya fedha

Muktasari:
- Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro Jacqueline Senzighe amesema mkaguzi huyo atapaswa kuwa miongoni mwa watumishi wa kitengo cha mahesabu katika chama hicho
Moshi. Chama Kikuu Ushirika Kilimanjaro (KNCU) kimetakiwa kuwa na mkaguzi wa awali wa mahesabu kwa ajili ya kukagua fedha zinayoingia na kutoka kabla ya mkaguzi wa ndani.
Rai hiyo imetolewa na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro Jacqueline Senzighe wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika mjini Moshi.
Amesema mkaguzi huyo atapaswa kuwa miongoni mwa watumishi wa kitengo cha mahesabu katika chama hicho.
Jacqueline amesema mkaguzi huyo atatakiwa kufuatilia kila fedha ya chama hicho, jambo litakalomrahisishia kazi, mkaguzi wa ndani wa mahesabu.
"Mkaguzi wa ndani wa awali ni muhimu sana na atasaidia kudhibiti matumizi mabaya na holela ya fedha, maana atatakiwa kupitia nyaraka zote za fedha za chama bila hata watu kujua, kabla ya fedha kuidhinishwa, hasa katika eneo la manunuzi; na apewe uhuru wa kufanya kazi kwa kuwa hii itaepusha kasoro,"amesema.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Lyamungo Amcos, Gabriel Ullomi amesema katika kutekeleza shughuli zake mkaguzi wa ndani wa awali atasaidia kudhibiti na kuepusha matumizi mabaya ya fedha za ushirika.
"Kuwepo kwa mkaguzi wa awali wa ndani ni jambo jema kwa kuwa atakuwa kioo cha chama na kupunguza matumizi ya fedha yasiyo sahihi, ni vyema kumpa mgonjwa tiba ya mapema kuliko kungojea aingie ICU,” amesema Ullomi.
Katika mkutano huo maalumu, wajumbe wameidhinisha maboresho ya masharti ya ushirika huo.
Kaimu Meneja Mkuu wa KNCU Godfery Massawe amesema maboresho mengine yaliyoidhinishwa ni pamoja na bodi kusimamia na kuhakikisha hesabu za chama zinafungwa ndani ya miezi mitatu tangu kuisha kwa mwaka wa fedha na ikishindwa kufanya hivyo, bodi iliyoko madarakani itaondolewa au itavunjwa na mrajis wa vyama vya ushirika.
Pia, mkutano huo umeridhia chama kupeleka maombi kwa mrajis wa vyama vya ushirika kuomba kuungana na cha kingine cha ushirika ili kuanzisha mradi wa pamoja na ushirika huo.