Kichanga chaokotwa kikiwa kimekufa jalalani ndani ya boksi Iringa

Muktasari:
- Kichanga kinachokadiriwa kuwa na siku moja kimeokotwa kikiwa tayari kimekufa ndani ya boksi lililokuwa limetupwa katika jalala la Kihesa, Manispaa ya Iringa.
Iringa. Wananchi wa Mtaa wa Kihesa, Manispaa ya Iringa wameuokota mwili wa mtoto mdogo anayekadiriwa kuwa na siku moja akiwa amefariki ndani ya boksi katika maeneo ya jalala la mtaa huo.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Augustino Kimilike amesema alipewa taarifa za kuwepo kwa mtoto huyo jalalani leo Mei 17, 2023 baada ya muokota makopo kumfuata na kumueleza juu ya tukio hilo.
“Asubuhi kabisa kuna mtu alikuja kunitaarifu na nilipoenda nimeona kweli mtoto wa kike ametupwa na ameshafariki. Tumetoa taarifa polisi na wamekuja kuchukua mwii,” amesema Kimilike.
Amesema hakuna mwanamke wanayemdhania kuwa amehusika na tukio hilo kwenye eneo lao lakini wanaendelea kufanya uchunguzi ili kujua muhusika ambaye anatakiwa kuchukuliwa hatua.
Baadhi ya wakazi wa mtaa huo walisema hilo ni tukio la nne kwa mtoto kichanga kuokotwa kikiwa tayari kimekufa.
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hii, fikiria wengine tunahangaika kupata watoto kiasi kwamba tunapewa mpaka masharti magumu na waganga na bado hatuzai lakini wapo wanawake wanajifungua na kuua watoto,” amesema Hilda Kulai, mkazi wa Kihesa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kumbaini muhusika.
Mtaalamu wa masuala ya saikolojia, John Paul amesema yapo mambo mengi yanayosababisha kuongezeka kwa ukatili ikiwamo utupaji au kutelekeza watoto ikiwamo ugumu wa maisha na kukataliwa.
“Mwanaume anampa binti mimba anakataa, akirudi nyumbani anafukuzwa anaamua kwenda kujihifadhi kwa rafiki yake huyu asipopata msaada wa kisaikolojia anaweza kusababisha madhara makubwa. Msaada wa kisaikolojia kwa jamii linatakiwa kuwa eneo muhimu zaidi,” amesema Paul.