Kesi ya 'Dk Manguruwe’ Shahidi aeleza alivyotapeliwa milioni 1.5 kilimo cha soya
Mkurugenzi wa Vanilla International Ltd, Simon Mkondya, maarufu Dk Manguruwe akiwa chini ya ulinzi
Muktasari:
- Mkondya na Rweyemamu wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu, kutakatisha fedha, matukio wanayodaiwa kuyatenda kati ya Januari Mosi 2020 na Desemba Mosi, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Shahidi wa 20 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Vanilla International Ltd, Simon Mkondya, maarufu Dk Manguruwe, ameieleza Mahakama jinsi alivyotapeliwa Sh1.5 milioni kupitia kilimo cha soya.
Shahidi huyo, David Mabwira, alidai alipoteza fedha hizo baada ya kuwekeza katika zao la soya lakini hakuwahi kuonyeshwa shamba wala kuvuna. Alisema alikutana na mshtakiwa kupitia tangazo la redio ya dini, kisha alielekezwa kulipa Sh1.5 milioni kupitia akaunti ya benki ya CRDB na kuingizwa kwenye mfumo wa wawekezaji wa kampuni hiyo.
Mabwira alidai aliambiwa mavuno yangekuwa miezi sita baadaye na angepata faida ya Sh4 milioni kwa ekari moja mkoani Njombe. Hata hivyo, hakuwahi kupelekwa shambani.
Alisema aligundua watu wengine walikuwa wakilalamika ofisini, hivyo walienda Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam, kutoa taarifa. Alimtambua Mkondya kwa mara ya kwanza wakati wa hatua ya utambuzi polisi.
Mahakama imepokea risiti ya malipo kama kielelezo. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ya wakili wa Serikali Theresia Mtao.
Washtakiwa, Mkondya na Rweyemamu John, wanakabiliwa na mashtaka 126, yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha (yanayomkabili Mkondya peke yake).
Inadaiwa kati ya Januari 2020 na Desemba 2023 waliendesha upatu kwa kuwaahidi watu faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizowekeza, wakikusanya fedha kutoka kwa watu zaidi ya 117.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja tisa vilivyopo Idunda, Njombe, akijua vilitokana na makosa ya awali.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 4, 2026, na Mkondya amerudishwa rumande huku John akiendelea kuwa nje kwa dhamana. Hadi sasa, mashahidi 20 kati ya 177 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi.