Kamati: Utegemezi fedha za kuhudumia kwenye VVU uondolewe

Muktasari:
- Kamati za Bunge zimeitaka Serikali kuongeza fedha za ndani kwa huduma za VVU, kupunguza utegemezi wa misaada na kuboresha utekelezaji wa bajeti na miradi muhimu ya maendeleo.
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ukimwi na Masuala ya Afya imetahadharisha Serikali kuhusu utegemezi wa fedha za nje katika kuwahudumia watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo katika bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2025/26 leo, Jumatano Aprili 9, 2025, Jackline Kainja amesema ni lazima Serikali ije na mpango wa kuongeza fedha za ndani katika eneo hilo.
Hivi karibuni, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kupunguza msaada wa kibajeti katika fedha ambazo taifa hilo kubwa limekuwa likitoa kwa nchi changa ikiwemo Tanzania.
Kainja pia amesema mpango wa kuagiza dawa za kufubaza VVU kutoka nje, unapaswa kuangaliwa upya, badala yake Serikali iwekeze katika viwanda vya ndani vizalishe dawa za kutosha.
Mbunge huyo amesema kwa hali ilivyo duniani, suala la kuendelea kuwa na utegemezi wa fedha za nje si jambo jema, hivyo Serikali inapaswa kusaidia watu wake kwa kujenga uwezo wa ndani.
Kamati hiyo pia imeeleza kuhusu ugumu wa upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Ukimwi kwa watu wanaoishi na VVU walioko magerezani, na kuiomba Serikali kulipa kipaumbele eneo hilo.
“Kamati inashauri badala ya kuendelea kuagiza nje dawa za kufubaza makali ya Ukimwi, zipatikane hapa nchini kwani kuna wakati hali inaweza kuwa mbaya,” amesema.
Pia Kamati imeshauri Serikali kuongeza nguvu katika upimaji wa maambukizi ya VVU kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii, Fatuma Tawfiq amesema Serikali inapaswa kuongeza bajeti yake katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Tawfiq ameeleza masikitiko ya Kamati hiyo kwa Serikali, hasa baada ya kushindwa kuongeza fedha hizo licha ya kupokea mapendekezo ya Kamati.
Amesema hadi sasa Serikali imeweka Sh1 bilioni katika mfuko huo badala ya Sh5.6 bilioni zilizopendekezwa.
Katika maoni ya Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, wajumbe wamelalamikia ucheleweshaji wa kukamilika kwa majengo ya nyaraka na ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo amesema majengo hayo yanapaswa kukamilika mapema ili yaanze kutoa huduma kwa kuwa ni muhimu na yanapaswa kuhudumia Watanzania.
Kwa upande wake, Kamati ya Bajeti imezungumzia upungufu wa fedha kwa kuwa bajeti inayotengwa haipelekwi kama inavyopaswa.
Akisoma maoni ya Kamati hiyo, Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe ameshauri fedha zinazotengwa katika bajeti ya Waziri Mkuu kwenye idara zake zifikishwe kama zilivyotengwa bila kupunguzwa.