Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

IGP Wambura aonya wananchi kujichukulia sheria mkononi

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Camillus Wambura, akiwasili katika Shule ya Polisi Tanzania – Moshi kwa ajili ya kufunga Mafunzo ya Awali ya Askari Polisi, Mei 22, 2026.

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura amewataka Watanzania kuendelea kuviamini vyombo vya dola na kuviachia vifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria za nchi.

Moshi. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amewaonya wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi, hali ambayo amesema imekuwa ikileta taharuki na kusababisha madhara kwa jamii.

Amesema matukio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa kutoa taarifa za upotoshaji na kuleta taharuki kwa jamii jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 22, 2026 wakati wa sherehe ya kuhitimu mafunzo ya awali ya jeshi hilo, katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Napenda kutoa rai kwa wananchi wote kuepukana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa sababu yoyote ile. Matukio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa habari za upotoshaji na kuleta taharuki kwa jamii, jambo ambalo ni kinyume cha sheria pia husababisha madhara makubwa,” amesema IGP Wambura.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuviamini vyombo vya dola na kuviachia vifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria za nchi.


Aonya matumizi holela ya simu

Pamoja na mambo mengine, amewataka maofisa hao wa Jeshi la Polisi kuepuka matumizi holela ya simu wawapo kazini na kuzingatia utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

 “Ndugu maaskari wote mliopo hapa, napenda kusisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Hakikisheni mnahudumia wananchi kwa kuzingatia utu heshima na weledi kwa kutambua kuwa wananchi ndio msingi wa kazi yetu ya ulinzi na usalama,” amesema IGP Wambura.


Mitandao ya kijamii

Katika hatua nyingine, IGP Wambura amewataka askari hao kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii hususani ushabiki usio na tija.

Amesema vitendo hivyo vinaweza kusababisha hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo, Ramadhani Mungi amesema kati ya wanafunzi 5,780 waliopokewa shuleni hapo mwaka 2025 waliofaulu ni wanafunzi 5,514 katika mafunzo hayo huku 234 wakishindwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu.

Aidha, amesema wapo baadhi ya wanafunzi ambao watabaki shuleni hapo kwa muda wa wiki tatu kutokana na kutokamilisha baadhi ya mafunzo.

Amesema askari hao wamepikwa vizuri shuleni hapo na wapo tayari kuitumikia nchi yao kwa uzalendo na kwa weledi mkubwa.