Ifahamu mikakati ya Makonda kuibadili Arusha

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema kufungwa Kamera na Polisi kuwa na taswira ya kitalii ni miongoni mwa mambo yatakayofanyika kulifanya Jiji la Arusha kuwa bora kwa utalii.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema katika kutekeleza maelekezo ya kuhamasisha utalii mkoani Arusha, mji huo unatarajiwa kufungwa kamera na kuwa na Polisi watakaokuwa wanatembea kwa baiskeli kuhakikisha usalama.
Makonda ametoa kauli hiyo jijini Arusha leo, Aprili 12, 2024 alipozungumza katika kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine.
Amesema askari hao watakuwa wa kitalii na kwamba watakuwa na taswira ya kitalii, kiasi cha watakaotembelea mji huo kutamani kupiga nao picha.
“Mji wetu ni wa kitalii, tumeshakaa vikao vingi, tumekubaliana Jiji la Arusha litafungwa kamera na kuhakikisha taa zinawaka na kuwa na Polisi wa kitalii watakaokuwa wanaendesha baiskeli kuhakikisha ulinzi umeimarika, ifike hatua watu wakija Arusha wasikie raha kupiga picha na polisi,” amesema.
Pamoja na hilo, katika kufanikisha maelekezo hayo kuhusu sekta ya utalii, Makonda amesema makubaliano yamefanyika kuondoa mabango yote yanayochafua taswira ya jiji hilo.
“Tumekubaliana kuondoa mabango yote yanayochafua sura ya Jiji la Arusha na kuhakikisha tunakuwa na mwonekano mzuri, ili watalii watakapokuja wasituone kama watu wasioweza kujipanga wakati nasi tunatembelea miji yao tunaona namna ilivyo,” amesema.
Alitumia jukwaa hilo kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan afanikishe upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 20 za barabara katikati ya Jiji hilo, aliyoeleza kuwa ni mbovu.
“Kwenye kikao walikuwa wananiambia huyo si mama yako, nenda na nikipita wanatabasamu wanasema yule si mama yake aende, kwa hiyo hapa Mheshimiwa Rais napimwa kama wewe ni mama yangu au la,” amesema Makonda na kuongeza;
“Hawakuwa wanasema kamwambie Rais, kila aliyekuwa ananiambia mwana-Arusha alikuwa ananiambia kamwambie mama yako kuhusu barabara,” amesema.
Pamoja na hayo, mkuu huyo wa mkoa amemtaka kila mkuu wa wilaya ndani ya mkoa huo ahakikishe anasimamia vyema eneo lake, ili kutatua kero za wananchi.
“Hii ni sura ya chuma, sina huruma na mtu na nimechelewa, tunataka wananchi wa Arusha wenye kero na changamoto zao zitatuliwe kwa sababu mambo mengine sio ya fedha ni utawala tu, amesema.
Ametoa onyo kwa wale aliodai wanatuma watu kwa kuwalipa fedha, ili wamtukane Rais Samia, akisema leo iwe mwisho, katika hilo ameeleza baadhi ya watu hao ni mawaziri.