Idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi yaongezeka

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda.

Muktasari:

 Idadi ya hatimiliki za pamoja kati ya wanandoa zimeongezeka na kufika asilimia 10 ya hati zinazotolewa

Dodoma. Idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi imeongezeka kutoka asilimia 25 hadi 41 kupitia Mradi wa Kuboresha Usalama wa Miliki za Ardhi (LTIP).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 22, 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda alipojibu swali la mbunge wa viti maalumu, Rose Tweve.

Tweve amehoji Serikali imefikia wapi katika kuweka utaratibu rahisi wa urasimishaji na umilikishaji ardhi hususani kwa wanawake.

Katika kujibu hilo, Pinda amesema Serikali inatekeleza mradi huo kwa mkopo wa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB) unaofanyika katika mamlaka za upangaji 58 nchini.

Amesema haki za wanawake zimezingatiwa ipasavyo katika utoaji wa elimu na uhamasishaji wa umiliki wa ardhi na umiliki wa pamoja baina ya mume na mke.

“Kupitia utaratibu huo, vikosi kazi vimeundwa kwa ajili ya kushughulikia uhamasishaji na utoaji elimu kwa makundi maalumu ya wanawake, wazee na wenye ulemavu katika suala la urasimishaji makazi na umiliki wa pamoja wa ardhi,” amesema Pinda.

Amesema elimu inatolewa kupitia vyama vya hiari vya kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, CSO na NGO.

Pinda amesema mikutano ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa mradi zimefanyika katika ngazi za mitaa, kata na wilaya.

“Wananchi 3,249 wamehudhuria mikutano hiyo wakiwamo wanaume 1,518 na wanawake 1,731. Mradi pia umewezesha kuongezeka idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kutoka asilimia 25 hadi asilimia 41,” amesema Pinda.

Amesema idadi ya hatimiliki za pamoja kati ya wanandoa zimeongezeka na kufika asilimia 10 ya hati zinazotolewa.