Wanasheria wawezesha wanawake kupata hati za ardhi

Wanasheria wawezesha wanawake kupata hati za ardhi

Muktasari:

  • Shirika lisilo la kiserikali la Legal Services Facility (LSF) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo imezindua mradi utakaowawezesha wananawake wanaomiliki ardhi katika wilaya ya hiyo kupata hati za umiliki wa ardhi.

Dar es Salaam. Shirika lisilo la kiserikali la Legal Services Facility (LSF) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo imezindua mradi utakaowawezesha wananawake wanaomiliki ardhi katika wilaya ya hiyo kupata hati za umiliki wa ardhi.


Mradi huu ujulikanao “Hati yangu maisha yangu” umeanzishwa ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wanawake wa hali ya chini ambao wanamiliki ardhi lakini wameshindwa kukamilisha umilikishwaji kutokana na kutoweza kumudu gharama.

Akizungumza leo Agoti 5 wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Ofisa mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema; “Tunatambua wanawake wanapitia changamoto nyingi sana zikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, kutopata fursa sawa katika masuala ya kiuchumi , kiuongozi lakini pia wamekuwa na majukumu mazito katika kulea na kuhakikisha ustawi wa familia zao.


“Hivyo tunaamini kupitia mradi huu tutawawezesha kumiliki ardhi walizonazo na kuzitumia katika kupata mitaji na kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa manufaa ya familia zao na taifa kwa ujumla.”

Amesema kupitia mradi huo watawafikia wanawake takribani 2000 kwa kuwapatia elimu na zaidi ya wanawake 300 watapata hati miliki zao kwa kuchangia asilimia 20 ya gharama zote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, Beatrice Kwai  alitoa shukrani zake za dhati kwa TAWLA ambao ni watekelezaji wa program pamoja na LSF ambao ni wafadhili wa program hiyo, kwa kuweza kutambua changamoto zinazowakabili wanawake katika jamii na kuamua kuchagua kutekeleza program hii katika Halmashauri ya Ubungo.

“Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutekeleza miradi ikiwepo kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa kudhibiti na kuzuia makazi yasiyopangwa (2012-2021) katika maeneo ya miji na mijini. Dar es Salaam ikiwa ni moja ya mikoa inayonufaika na mpango huo hususani katika Wilaya ya Ubungo,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile amesema chama hicho kitafanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo ili kufanikisha wanawake pamoja na makundi maalum  kupimiwa ardhi na kupatiwa hati miliki.

“Tutaongeza uelewa kwa wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi na jinsi ya kutumia ardhi kama vyanzo vya uchumi, kutoa elimu kwa viongozi katika ngazi za kata na mitaa, viongozi wa dini na wasaidizi wa kisheria juu ya wajibu wao,” amesema Tike.