Gari la mbunge lataifishwa, wahamiaji haramu watupwa jela

Gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T888 BTY likiwa eneo la maegesho Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Muktasari:

  • Mahakama pia imeamuru kutaifishwa lori lililokamatwa likisafirisha wahamiaji haramu

Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Moshi, zimeamuru kutaifishwa magari mawili yaliyokamatwa yakiwasafirisha wahamiaji haramu 12 raia wa Ethiopia, likiwamo linalodaiwa kumilikiwa na mbunge.

Mbali na kutaifishwa kwa magari hayo kuwa mali ya Serikali ya Tanzania, mahakama zimewahukumu wahamiaji hao kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Magari yaliyotaifishwa kwa amri ya mahakama hizo iliyotolewa leo Julai 2, 2024, ni Toyota Land Cruiser namba T888 BTY ambalo jina la mmiliki linalosomeka kwenye nyaraka za umiliki, linafanana na la mbunge mmoja nchini Tanzania.

Gari lingine lililotaifishwa ni lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KCV 571Y za nchi jirani ya Kenya ambalo lilikamatwa katika mji wa Tarakea wilayani Rombo, Juni 19, 2024 likiwa na wahamiaji haramu watano.

Hukumu dhidi ya wahamiaji hao zimetolewa na mahakimu wawili tofauti, moja ikitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Moshi, Rehema Olambo dhidi ya raia saba wa Ethiopia waliokamatwa Juni 4, 2024. Walikamatwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 namba T888 BYT katika eneo la Njiapanda wilayani Moshi. Dereva aliyekuwa akiliendesha gari hilo alitoroka na hadi leo hajakamatwa.

Hukumu ya pili imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Herieth Mhenga dhidi ya Waethiopia watano waliokutwa wamejificha chini ya uvungu wa lori kutoka Kenya.


Kesi zilivyokuwa kortini

Katika kesi dhidi ya washtakiwa saba waliokamatwa wakiwa kwenye Toyota Land Cruiser linalodaiwa ni mali ya mbunge anayetokana na CCM, Wakili wa Serikali, Agatha Pima akishirikiana na Wakili Henry Daud waliwasomea maelezo ya awali.

Hatua hiyo ilitokana na washtakiwa kukiri makosa walipofikishwa kortini kwa mara ya kwanza Juni 14, 2024. Kesi iliahirishwa hadi Julai 2, 2024 ili upande wa mashtaka uwasomee maelezo hayo.

Lori likiwa limeegeshwa kwenye kambi ya Polisi Moshi.

Washtakiwa hao, Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso, baada ya kusomewa maelezo  waliyakubali ndipo wakatiwa hatiani na mahakama chini ya Hakimu Olambo.

Baada ya kuwatia hatiani amewahukumu kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja. Wameshindwa kulipa faini hiyo.

Baada ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali, Agatha Pima kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), ameiomba mahakama itoe amri ya kutaifishwa kwa gari lililotumika kuwasafirisha, ombi ambalo mahakama ililikubali na kutoa amri hiyo.

Katika kesi ya pili iliyowahusu Admasu Bakala (18), Dagife Dasta (18), Abayna Safa (19), Emanuel Tegese (18) na Mesgana Trfo (18) ambaye ni mwanafunzi, upande wa mashtaka uliwasomea maelezo ya awali ambayo waliyakubali kuwa ni sahihi.

Walidaiwa Juni 19, 2024 eneo la Tarakea wilayani Rombo, washtakiwa waliingia nchini kinyume cha sheria kwa kutumia lori.

Katika kosa la pili, ilidaiwa siku hiyo katika eneo hilohilo, walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Herieth Mhenga aliwatia hatiani kwa kosa la kukutwa wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini Tanzania.

Mahakama iliwahukumu washtakiwa kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja, walishindwa kulipa faini na kupelekwa gerezani.

Baada ya kuhukumiwa adhabu hiyo, mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo waliiomba mahakama itaifishe lori la kubeba gesi kutoka Kenya lililotumika kuwasafirisha wakijificha uvunguni, ombi ambalo liliridhiwa na mahakama.


Sheria ya Uhamiaji inavyosema

Kulingana na kifungu cha 46(1) cha Sheria ya Uhamiaji sura ya 54 kama ilivyorejewa mwaka 2016, kimetamka makosa mbalimbali yanayoweza kutendwa na mtu, ikiwamo kusafirisha na kuwahifadhi wahamiaji haramu.

Kifungu hicho kinatoa adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya makosa hayo kuwa ni faini isiyopungua Sh20 milioni au kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Kulingana na kifungu kidogo cha (2) ni kuwa mbali na adhabu hiyo, mahakama kwa utashi wake yenyewe au maombi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), inaweza kuamuru kutaifishwa kwa chochote kile kilichotumika.

Hii kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2)(a), inaweza kuamuru kutaifishwa kwa pesa na mali zilizopatikana kwa kuwaingiza kiharamu wahamiaji haramu na 2(b) chochote kile iwe nyumba au gari iliyofanikisha biashara hiyo haramu.