Prime
Gari la ‘mafao’ lilivyokatisha uhai wa mwalimu mstaafu, mwanawe

Muktasari:
- Alistaafu utumishi wa umma Oktoba 2024, akapata mafao yake na kuamua kwenda jijini Dar es Salaam kununua gari. Hakufika nyumbani akapoteza maisha ajalini akiwa na mwanawe wa mwisho na rafiki yake.
Arusha. Ni simanzi na majonzi kwa familia ya Apaikunda Ayo (61) ambaye ni mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Imbaseni aliyefikwa na mauti kwa ajali ya barabarani akiwa njiani kurejea nyumbanii kwake Kijiji cha Imbaseni, Arumeru akitokea Dar es Salaam alikokwenda kununua gari jipya kutokana na fedha za mafao.
Wengine waliofikwa na mauti katika ajali hiyo iliyotokea asubuhi ya Februari 1, 2025 eneo la Mdawi, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro ni Mark Exaud (22) ambaye ni mtoto wake wa mwisho aliyemsindikiza mama yake kurudi kwao.
Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Esther Luxury na gari dogo aina ya Toyota RAV4 yenye namba T592 EKU ambayo mwalimu Apaikunda aliinunua jijini Dar es Salaam na alikuwa anarejea nyumbani kwake.
Mbali na Mwalimu Apaikunda na mwanawe Exaud, pia kwenye gari hiyo alikuwamo Paul Sita (25) aliyekuwa dereva wa gari hilo dogo.
Inaelezwa Paul ni rafiki wa Exaud ambaye alimua kumsindikizi rafiki yake kumrudisha mama ambapo wote walifikwa na umauti.
Februari 1, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alizungumzia ajali hiyo akisema chanzo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kujaribu kuyapita magari mengine, bila kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na basi la abiria la kampuni ya Esther luxury.
Apaikunda amefikwa na mauti takribani miezi mitatu tangu alipostaafu ualimu katika Shule ya Msingi Imbaseni, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha. Sherehe ya kumuaga ilifanyika Desemba 6, 2024.
Leo Jumatatu Februari 3, 2025, Ruth Ayo, mdogo wa marehemu Apaikunda amesema wamepoteza watu muhimu na dada yao amefikwa na mauti akitokea Dar es Salaam alikofuata gario hilo pamoja na kuwasalimia watoto wake wawili waishio jijini humo.
“Katika ile ajali tumempoteza dada yetu na mtoto wake wa mwisho ambaye ni Mark. Dada alifuata hilo gari Dar es Salaam lakini pia alikwenda kusalimia watoto wake wawili waishio huko,” amesema.
Ameongeza: “Baada ya kumaliza aliamua kurudi Arusha, ndipo mtoto wake (Mark) akaamua kumsindikiza mama yake. Dada alikuwa na watoto wanne, amecha mume na watoto watatu,” amesema Ruth.
Mwananchi lilipomuuliza Ruth, gari hilo lilitokana na fedha alizozipata baada ya kusitaafu amesema:”Ndiyo lakini sijajua ni bei gani alinunua kwani alikuwa hajatueleza. Kiukweli alikuwa mkarimu sana, dada yangu alikuwa anajua kuishi na watu vizuri sana na alikuwa mzee katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Imbaseni.”
Ruth amesema wanatarajia maziko ya wanafamilia hao kufanyika kesho Jumanne Februari 4, 2025 katika Kijiji cha Imbaseni, wilayani Arumeru alipokuwa akiishi marehemu. Huku mwili wa Paul ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam haijafahamika utazikwa wapi.
Mkuu wa shule asimulia
Mwananchi limezungumza na Naetwe Emmanuel, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Imbaseni aliyokuwa akifundisha Apaikunda, ambaye amesema amepoteza mshauri mzuri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mwalimu huyo amesema amefanya kazi na marehemu kwa muda wa miaka miwili kabla hajastaafu Oktoba 2024 na wao kama ofisi walifanya sherehe ya kumuaga Desemba 6, 2024 na bado walikuwa wakiendelea kushirikiana naye katika masuala mbalimbali ya kijamii.
“Nimefanya naye kazi kwa miaka miwili, alikuwa akitupa ushauri katika utekelezaji wa kazi na Desemba 6, mwaka jana tumemuaga rasmi baada ya kustaafu. Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wake,” amesema.
“Mimi binafsi mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Alhamisi iliyopita Januari 30, 2025 na aliniambia alikuwa akifuatilia masuala ya mafao yake. Msiba huu tumeupokea kwa mshtuko na hata leo umeathiri utendaji kazi wetu kwani bado tulikuwa tukishirikiana naye,” amesema mwalimu Naetwe.