Fahamu mazoezi yanayoimarisha afya ya moyo
Muktasari:
- Kufanya mazoezi ni moja ya hatua muhimu kuelekea katika afya bora ya mwili, kwani ni moja ya nyenzo rahisi yenye kuboresha afya.
Magonjwa ya moyo au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na yanaongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani.
Hata hivyo, matatizo mengi ya moyo yanayotokana na miendendo na mtindo mibaya ya maisha yanaweza kuepukwa, endapo tutafanya mazoezi mepesi mara kwa mara.
Kufanya mazoezi ni moja ya hatua muhimu kuelekea katika afya bora ya mwili, kwani ni moja ya nyenzo rahisi yenye kuboresha afya.
Mazoezi huboresha afya ya moyo, misuli, kudhibiti uzito wa mwili, kuisaidia mishipa ya damu isiharibiwe na mafuta mabaya, kudhibiti kiwango cha sukari katika damu ambacho kinaweza kukusababishia shambulizi la moyo na kiharusi.
Ukweli ni kwamba mwili unahitaji mchanganyiko wa mazoezi ambayo yakifanyika unaweza kunufaika na faida zake.
Wanasayansi wa mazoezi ya mwili wanapendekeza mchanganyiko wa mazoezi ya aina tatu ambayo watafiti wa mazoezi na afya wamebaini kuwa na mchango mkubwa kwa afya bora ya moyo.
Moyo huweza kupata matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwamo mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo kuharibika huweza kusababisha kupata shambulizi la moyo tatizo ambalo lisipodhibitiwa huweza kujirudia au kusabaisha kifo cha ghafla.
Moyo ni ogani nyeti ya mwili ambayo huitajika kuwa na utendaji wenye ufanisi, kwani moyo unaposimama kila kitu mwilini kinakwama kwani ndiyo ogani inayosukuma damu kwenda maeneo mbalimbali mwilini.
Ni kwa vipi aina za mazoezi tunayofanya kila siku yanatunufaisha kwa upande wa afya zetu na kuweza kuishi maisha marefu?
Mazoezi mepesi ndiyo mazoezi rahisi yanayoboresha afya ya moyo kirahisi, kwani yanaimarisha mzunguko wa damu hivyo kuleta matokeo mazuri ikiwamo kushusha shinikizo na kasi ya moyo na huku pia ukileta msukumo mzuri wa damu toka katika chemba za moyo.
Ili kupata faida hizi kisayansi inashauriwa kufanya mazoezi haya angalau dakika 30-60 kwa siku kwa siku tano za wiki.
Mfano wa mazoezi haya ni pamoja na kutembea, kukimbia kidogo kidogo, kuogelea, kuruka kamba, kuendesha baiskeli na kucheza muziki wa kasi na kushiriki michezo inayoishughulisha viungo vingi vya mwili.
Aina ya pili ya mazoezi kwa ajili ya afya ya moyo ni mazoezi kinzani ambayo hujulikana kama Resistance Training au strength work ambayo yanahusisha ufanyaji zoezi magumu katika eneo fulani mwilini.
Mfano kwa mtu mwenye unene au kuwa na mrundikano mwingi wa mafuta ikiwamo kuwa na kitambi ndiyo wanahitajika kuchanganya zoezi hili na megine, ili kukata mafuta ikiwamo mafuta mabaya yaani lehemu mbaya (bad cholesterol) na kuongeza lehemu nzuri (good cholesterol).
Mazoezi haya huweza pia kuondoa au kupunguza mafuta yaliyorundika na kuongeza ukubwa misuli pamoja na kuikakamaza na kuwa imara.
Mfano wa aina hii ya mazoezi ni pamoja na kupiga “push up” mazoezi ya tumbo unyanyuaji miguu juu chini huku umelala, kubeba vitu vizito vya wastani au kutumia mashine maalum zile za vituo vya mazoezi ambazo huwa na uzito unaokuhitaji kubeba, kunyanyua au kusukuma.
Wakufunzi huweza kuwafanyisha aina ya mazoezi ambayo huwa ni magumu kiasi kwa kunyanyua vitu vizito au kufanyishwa mijongea ya kimazoezi inayoshughulisha misuli ya eneo lenye mafuta mengi.
Kanuni nzuri ya kufanya mazoezi kinzani ni kuyafanya kwa siku mbili za wiki lakini sio kufanya kwa mfululizo bali siku hizo ziachanishwe mfano ukifanya leo kesho unapumzika unafanya keshokutwa ama mtondogoo.
Aina ya tatu ya mazoezi ni yale ya kunyoosha viungo, ulainishaji na kupasha misuli na viungo vya mwili ambayo hujulikana kama stretching, flexibility and balance.
Aina hii ya mazoezi si kama yanaboresha moja kwa moja afya ya moyo bali tu huwa na faida zaidi katika mfumo wa misuli na mifupa kwa kuandaa mwili kufanya aina ya kwanza na ya pili ya mazoezi.
Mazoezi hayo yanaufanya mwili kuwa na utimamu na wepesi kimwili, kuondoa uchovu, kulainisha maungio ya mwili, kupunguza hatari ya kubanwa na misuli na majeraha wakati wa kufanya mazoezi mengine.
Mazoezi haya yafanyike kwa dakika 5-10 na yanafanyika kila siku, kabla na baada ya mazoezi mepesi na kinzani.
Mchanganyiko wa ufanyaji mazoezi haya ndiyo unaungwa mkono na madaktari wa moyo wa taasisi maarufu ya Tiba duniani ijulikanayo kama John Hopkins ya nchini Marekani.
Tafiti za kituo hiki zimeonyesha aina hii ya mazoezi na muda huo kuwa na tija katika kuboresha afya ya moyo na mwili kiujumla na hivyo kuwafanya watu wanaofanya mazoezi haya kuishi muda mrefu.