Dk Nchimbi awaandaa kisaikolojia wagombea CCM

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa ziara yake Mei 29, 2024 kuanzia mkoani Singida, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amekuwa akiwataka makada wa chama hicho kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu.

Moshi. Wakati joto la chaguzi zijazo likiendelea kufukuta ndani ya vyama vya siasa nchini Tanzania, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameanza kuwaandaa kisaikolojia wanachama wake endapo watashindwa kwenye uchaguzi kutokuwa na kinyongo.

Dk Nchimbi amesema historia ya chaguzi zilizowahi kufanyika zinaonyesha katika kila nusu ya waliokuwa madarakani kwenye Serikali za mitaa, madiwani na wabunge hushindwa kutetea nafasi zao.

Hii ni katika michakato ya ndani ya vyama na wengine hushindwa kwenye masanduku ya kura dhidi ya washindani wao na wakishindwa walikubali na waendelee kuchapa kazi.

Jana Jumatano Juni 5, 2024, Dk Nchimbi akihutubia mkutano wa hadhara, Stendi Kuu ya Moshi, mkoani Kilimanjaro alisema kila uchaguzi wa miaka mitano nusu yao wanakuwa wapya, wengine wanatoka na kuingia. Anayepata anapata, anayekosa anakosa.

"Kutokuwa kiongozi hakukuondolei wajibu wa kutumikia Watanzania wetu, kuna nafasi mbalimbali na kila mwananchi kwenye eneo lake tumikia wajibu wako hapo ulipo," alisema Dk Nchimbi.

Kauli kama hiyo, aliitoa pia akiwa mkoani Arusha ambapo alisema kuwa mwanasiasa mzuri ni yule ambaye amewahi kushinda na kushindwa, akitolea mfano yeye kwenye harakati zake za kisiasa amewahi kushindwa mara nne na wala hakukata tamaa.

"Na hata niliposhindwa sikulalamika, nawaambia kama wewe ni mwanasiasa na hujawahi kushindwa basi hujakomaa, lazima ushindwe kidogo na ukishindwa kubali," alisema Dk Nchimbi aliyewahi kuwa Mbunge wa Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma.

Kuonyesha joto linafukuta, Mei 30, 2024, Dk Nchimbi katika kikao cha ndani cha viongozi mbalimbali mkoani Singida aliwaonya wale wote wanaopanga safu za wagombea au kujipitisha kuacha mchezo huo.

Amesema hatua hiyo inawanyima usingizi viongozi waliopo kwenye dhamana kutekeleza wajibu wao, kwa hiyo, "tukatae mchezo huu wa kupanga safu na wale wote wanaotaka kugombea kama fursa."

“Kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila mmoja, hatuwezi kwenda wote, tunachagua wachache kwenda kutuwakilisha, sasa wakati ukifika tuchague watu ambao watasomana mbele kwa wananchi wetu, si wale wanaotafuta fursa,” amesema.


Jicho la Mwananchi Digital

Katika maeneo mbalimbali ambapo msafara huo umepita, Mwananchi Digital limeng'amua sura tofauti za kisiasa.

Mathalani, makundi ya chaguzi zilizopita hayajamalizika. Waliokuwa wagombea katika Uchaguzi Mkuu 2020 wanaendelea kupiga jaramba.

Kuna wale walioongoza kura za maoni ama walikuwa nafasi ya pili au ya tatu lakini walikatwa, waliowahi kuwa wabunge au madiwani wa maeneo wakiwa mstari wa mbele.

Kila Dk Nchimbi alipopita walihakikisha wanamfikia, kwa kuteta naye, kupiga picha na wakati mwingine kuchagia miradi ya maendeleo ya chama hicho ndani ya eneo husika.

Pia wagombea ama watia nia nafasi za madiwani na wabunge wa viti maalumu hawakuwa mbali. Unaweza sema ni 'vikumbo' kwa kila mmoja kuhakikisha ushiriki wake unaonekana na wakati mwingine kuwafikia viongozi walioambatana na Dk Nchimbi

Mmoja wa waliowahi kuwania ubunge katoka moja ya majimbo ya mikoa ya Kaskazini amesema:

"Kaka, hii ziara hupaswi kukaa nayo mbali kama una malengo ya 2025. Lazima uwe karibu na ushiriki, hata kama wanasema kampeni bado ila kujipitisha pitisha kwa katibu mkuu muhimu, ndio siasa zenyewe hizi."

Wabunge mbalimbali waliopo hawakuwa mbali kueleza mafanikio waliyoyafanya na kujinadi kwa wananchi waendelee kuwaamini na ikiwa Dk Nchimbi atapelekewa fitina awe nazo makini.

Hata hivyo, baadhi ya wagombe wanapitia joto kali kwa washindani wao ambao wanaonyesha nia za kutaka nafasi walizopo kama vile wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wenyeviti wa halmashauri au mameya, hali inayowafanya wasiwe na utulivu.


Mchakato kupata wagombea

Hoja ya wajumbe iliibuka pia Juni 1, 2024, Babati Mjini, Mkoa wa Manyara kwenye mkutano wa hadhara ambapo Andrew Omary, mwanachama wa chama hicho aliyeshauri utaratibu wa wanachama kuwapigia kura madiwani urejeshwe na kwa ubunge unaweza kuendelea wa wajumbe.

Ambapo Dk Nchimbi alisema ameupokea ushauri wa Omary na ataufikisha kwenye vikao husika.