Dk Mwinyi awaapisha mawaziri wake, waahidi kazi iliyotukuka
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi
Muktasari:
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amewaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri baada kufanya mabadiliko ya baraza hilo hivi karibuni.
Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amewaapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri baada kufanya mabadiliko ya baraza hilo hivi karibuni.
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Unguja leo Alhamis Machi 10, 2022 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Wakizungumza baada ya kuapishwa mawaziri hao wameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa ili kurudisha heshima kwa Rais aliyewaamini na kuwapa nafasi hizo.
Dk Saada Mkuya Saalum ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, amesema Rais Mwinyi amemuamini na kumkabidhi kazi hiyo ambayo inahitaji utekelezaji na uadilifu mkubwa.
“Nitahakikisha natekeleza wajibu wangu kwa mujibu sheria, kanuni na utaratibu uliokuwepo ili kuweza kupeleka mbele maendeleo ya Zanzibar kama wanavyotarajia wananchi,” amesema
Amesema amepewa dhamana kubwa ya fedha hivyo hatokuwa tayari kuona wizara yoyote inafanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Amesema ubadhirifu wa fedha za umma wa aina yoyote ile na ufisadi haukubaliki hasa serikali ya awamu nane hivyo atapigana kuhakikisha kila senti inatumika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi na Mandeleo ya Makazi, Nadir Abdullatif alisema ni wakati sasa kufanya kazi na kujipanga kwani wizara aliyoteuliwa ina changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi.
Ameahidi kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku ili kuona dhamira ya Rais ya kuwaletea wananchi maendeleo inafikiwa.
Hassan Khamis Hafidh ambaye ni Naibu Waziri wa Afya aliahidi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na kuhakikisha wanashirikiana pamoja katika kufanya kazi kwa pamoja katika kuwatumikia wananchi.
Naibu huyo amesema atahakikisha anasimamia majukumu na utendaji kwa watumishi wa wizara hiyo ili kuona wanafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanazipatia ufumbuzi changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo ukosefu wa dawa.
Aidha kwa upande Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi, Suleiman Masoud Makame alisema mikakati yake katika wizara hiyo ni kuitangaza dhana ya uchumi wa bluu kwani bado haijatangazwa vyema.
Hata hivyo amesema wana kazi nyingi za kufanya katika sekta hiyo hasa kwa wapandaji wa mwani, wavuvi na wale wote wanaoguswa na uchumi huo ili kuona unaleta tija kwa wananchi wa Zanzibar kimaendeleo.