Dk Mpango ashiriki mazishi ya hayati Chilima wa Malawi

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa  aliyekuwa Makamu wa Rais wa Malawi, hayati Saulos Klaus Chilima.

Muktasari:

  •  Taifa la Malawi leo Jumapili Juni 16, 2024 limefanya mazishi ya kitaifa ya Makamu wake wa rais, hayati Saulos Klaus Chilima aliyefariki katika ajali ya ndege pamoja na wenzake tisa Juni 10, 2024.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Malawi, hayati Saulos Klaus Chilima.

Ibada ya Mazishi hayo imefanyika leo Jumapili, Juni 16, 2024 katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi.

Akitoa salamu za rambirambi, Dk Mpango amesema Tanzania inatoa salamu za pole na kuungana na waombolezaji wote walioguswa na msiba huo katika kipindi hiki kigumu.

Dk Mpango amesema hayati Chilima alikuwa kiongozi imara, mwanamajumui wa kweli wa Afrika ambaye wakati wote alitanguliza mbele masilahi ya wananchi anaowaongoza na Afrika kwa ujumla.

Pia, amemtaja hayati Chilima kama kiongozi aliyesimamia umoja, amani,  usalama, mageuzi ya kiuchumi ya Malawi na utawala wa kidemokrasia nchini humo.

Makamu wa Rais amesema wananchi wa Malawi na ukanda wote kwa ujumla wanapaswa kumuenzi hayati Chilima kwa kuendeleza yale aliyosimamia na kuendelea kumuombea apumzike kwa amani.

Dk Mpango  ameambatana na Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamza Hassan Juma, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato pamoja na Balozi wa Tanzania, Agnes Kayola.

Hayati Chilima (51) alifariki dunia katika ajali ya ndege na wenzake tisa iliyotokea katika msitu wa Chikangwa. Ndege hiyo iliondoka Lilongwe saa 3:17 asubuhi ya Juni 10, 2024 na ilipangwa kutua Uwanja wa Ndege wa Mzuzu saa nne asubuhi, lakini haikuweza kutua kutokana na hali mbaya ya hewa na kuamriwa kurejea katika mji mkuu, ambako haikufika.