DED Igunga asota mahabusu watano wakiachiwa kwa dhamana
Muktasari:
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kigoma imewaachia huru kwa masharti ya dhamana washtakiwa wa tano kati ya 11 waliokuwa wanashtakiwa kwa makosa 11 huku, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga, Athumani Msabila na wenzake watano wakiendelea kusota mahabusu.
Kigoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kigoma imewaachia huru kwa masharti ya dhamana washtakiwa wa tano kati ya 11 waliokuwa wameshtakiwa kwa makosa 11 likiwemo la utakatishaji fedha wa Sh463.5 milioni, huku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga, Athumani Msabila na wenzake watano wakiendelea kusota mahabusu.
Katika kesi namba 3 ya mwaka 2023 iliyofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 7, 2023 na washtakiwa kusomewa mashtaka 11 yakiwemo ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kugushi nyaraka, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh463.5 ambapo hawakutakiwa kujibu chochote.
Akisoma uamuzi huo leo Jumatatu Novemba 20, 2023; Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Hassan Momba amesema Mahakama imejiridhisha kuwa, mashtaka walionayo hayana pingamizi kisheria kupata dhamana.
Walioachiwa huru kwa dhamana ni mshtakiwa namba saba, Joel Shirima, Jema Mbilinyi mshtakiwa namba nane, Kombe Kabichi mshtakiwa namba tisa, Frank Nguvumali mshtakiwa namba 10 wote kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Bayaga Ntamasambilo mstakiwa namba 11 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Huku, washtakiwa wengine sita akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga Athumani Msabila, Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dodoma, Frednand Filimbi, Salum Juma, Moses Zahuye ambao ni watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wakiendelea kusota mahabusu hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Desemba 4, 2023.
Hakimu Momba amesema washtakiwa hao watatakiwa kutimiza masharti waliyopewa na mahakama hiyo ikiwemo kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa mtendaji, mali isiyohamishika yenye thamani kuanzia Sh40 milioni pamoja na kufanyiwa tathmini.
“Dhamana iko wazi kwa washtakiwa watano ambao ni namba 7, 8, 9, 10, 11 cha muhimu watimize masharti yaliyowekwa na Mahakama kwani tumejiridhisha mashtaka mlionayo hayana pingamizi kisheria kupata dhamana,”amesema Hakimu Momba
Awali upande wa Mawakili wa Utetezi ukiongozwa na Wakili Sadiki Aliki, wameiomba Mahakama hiyo kuangalia upya sharti la tatu la washtakiwa kupata dhamana linalomtaka mdhamini kwenda kufanya tathmini ya mali yake isiyohamishika kwa mtathmini wa majengo.
Amesema ni wazi kuwa washtakiwa hao ni watumishi wa Serikali na wadhamini wao pia ni watumishi wa umma hivyo si rahisi wao kutoroka na kwamba ni watu wanaoaminika kwani hatua za kwenda kufanya tathmini inachukua muda mrefu na wateja wao wataendelea kukaa ndani hivyo wanaomba Mahakama iweze kuangalia upya hoja hiyo.
Wakili wa upande wa Jamuhuri, Edina Makala amesema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuwataka mawakili upande wa utetezi kufuata masharti yote kwa wateja wao ili waweze kupata dhamana.