Daraja la Kigongo Busisi sasa kuitwa JPM

Muktasari:
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema daraja la Kigongo- Busisi limepewa jina la Rais John Magufuli ili aendelee kukumbukwa milele kutokana kazi kubwa aliyoifanya kwenye utawala wake.
Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema daraja la Kigongo- Busisi limepewa jina la Rais John Magufuli ili aendelee kukumbukwa milele kutokana kazi kubwa aliyoifanya kwenye utawala wake.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 18, 2020 alipotembelea na kukagua ujenzi wa daraja hilo ulioanza mwaka 2020 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2024.
Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 litakuwa na nguzo 67 na litagharimu Sh699.2 bilioni. Linajengwa na kampuni ya CCECC ya nchini China.
"Limepewa jina lake ili aendelee kukumbukwa milele," amesisitiza Majaliwa.
Amesema ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea nchini lengo ni kurahisisha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira mazuri.
Amewataka watanzania kupuuza kauli za baadhi ya watu kwamba serikali inajali zaidi vitu badala ya kuleta maendeleo ya watu.
"Tupuuze hizi taarifa hizi ni za watu wenye nia ovu, huwezi kupata maendeleo bila kuirahisishia mambo kama haya ya usafiri," amesema
Amesema mbali na kuboresha miundombinu hiyo lakini kupitia miradi hiyo inaongeza ajira kwa watanzania.