Chongolo: Sijaridhika utatuzi changamoto ya maji

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo
Muktasari:
- Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo imeendelea kuwa shubiri kwa watendaji Wizara ya Maji.
Chemba. Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo imeendelea kuwa shubiri kwa watendaji wa Wizara ya Maji.
Akihutubia Mkutano wa hadhara uliofurika mamia ya wananchi, katika Kijiji cha Mrijo Chini, Chongolo alisisitiza kuwa hajaridhishwa kabisa na miradi ya maji katika wilaya nzima ya Chemba.
Chongolo alisema hajaridhishwa na usimamizi wa miradi ya maji ambayo imechangia vijiji vingi vya wilaya hiyo kukosa maji licha ya miradi kuanzishwa lakini utekelezaji wake ni hasi.
“Niwahakikishie, nimeyaona, nimeyachukua mwenyewe naenda kumwambia aliyewateua kuhusu mambo yanavyoendelea na namna ambavyo sijaridhika na utatuzi wa changamoto ya maji, nimezunguka maeneo yote sijaridhishwa kabisa,” amesema Chongolo.
“Hatuwezi kupewa dhamana tukaja kuwapiga wananchi, hatuwezi kukaa tukabembelezana kwa mambo ya msingi wakati wananchi mnataka matokeo na sisi tuliahidi kuyatatua sasa kama mtu hataki kuyafanyia kazi aende akalime kwao asikae kwenye nafasi ya kushughulikia matatizo ya wananchi.”
Aweso aliitwa Mpwapwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Dodoma Juni 15, 2023 ambapo alimtaka akatatue tatizo la maji Kijiji cha Lupeta na siku iliyofuata aliitwa tena Kijiji cha Pwaga wilayani humo.
Leo Mbunge wa Chemba Mohamed Moni amemwambia Katibu Mkuu kuwa hakuna mradi wa maji ambao umeanzishwa wilayani hapo na kukamilika zaidi ya maneno matupu.