Chanjo ya Ukimwi kuanza na watu 56

Muktasari:
- Utafiti wake wafikia hatua ya tatu ambapo itaanza kujaribiwa kwa binadamu.
Dar es Salaam. Chanjo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) iliyokuwa inafanyiwa utafiti muda mrefu na Kampuni ya Moderna ya Marekani inatarajiwa kuanza majaribio kwa binadamu leo.
Hatua hii imekuja baada ya kampuni hiyo ambayo inatengeneza chanjo za aina mbili za Ukimwi, kufuzu hatua za awali za kimajaribio na hivyo kuanza kutumika kwa binadamu katika awamu ya tatu.
Chanjo hizo ni pamoja na mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core, ambazo zimeshachunguzwa na kufanyiwa majaribio ya awali na kuonekana salama kabla ya kujaribiwa kwa binadamu kwa mara ya kwanza.
Kampuni hiyo ilisajili watu wazima 180 nchini Marekani kwa ajili ya jaribio la kutathmini usalama na katika jaribio la nguvu ya kinga inayoitwa mRNA-1010, watajaribiwa watu 56 ambao hawana maambukizo, wenye umri kati ya miaka 18 mpaka 56.
Mordena ina matumaini ya kupata chanjo hiyo kutokana na teknolojia mpya ya mRNA iliyotumika, sawa na ile inatumika kutengeneza chanjo ya kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (Uviko-19), kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 na ikiwa jaribio litafanikiwa litasababisha kupatikana chanjo ya VVU iliyosubiriwa kwa miaka 38.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mordena, Stephane Bancel alisema Moderna inatumia teknolojia ya mRNA, ambayo husababisha mwitikio wa kinga kwa kutoa molekuli za maumbile zilizo ndani ya seli za mwanadamu, zinazoweza kuharakisha ukuaji na kuongeza utepetevu.
Kufuatia hatua hiyo, mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema kuendelea kwa hatua nyingine ya majaribio kwa chanjo hiyo ni jambo zuri kwa kuwa dunia imekaa muda mrefu bila kuwa na chanjo nyingine inayotafutwa kupambana na VVU.
Alisema hiyo ni hatua nzuri, kwani kumeshafanyika majaribio mengine, ikiwemo Tanzania ambako yameshafanyika zaidi ya mara mbili, lakini mafanikio hayakuwa makubwa.
“Kwa mfano, kampuni kama ya Moderna inataka kujaribu hiyo chanjo na wao ndio waliotengeneza mojawapo ya chanjo ya Uviko-19 kwa kutumia teknolojia ya mRNA na wanataka kutumia hiyo pia kufanikisha chanjo dhidi ya VVU, hivyo ni hatua kubwa.
“Tuna matumaini kwamba inaweza kutupatia majibu. Dunia inasubiri kwa hamu kama watapata chanjo, maana yake mzigo mzito kupambana na haya maradhi utapungua na badala yake dunia itajielekeza katika matatizo mengine ya kiafya, kiuchumi na kijamii,” alisema.
Dk Osati alisema pia kumekuwa na changamoto kwa wagonjwa wenyewe, hasa suala la kumeza dawa kila siku ambalo si jambo dogo, hivyo kama muafaka utapatikana itakuwa vema.
Meneja programu wa tiba na utunzaji watoto wenye VVU kutoka shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (Egpaf), Juma Songoro alisema kwenye magonjwa yote, chanjo ina faida zaidi kuliko matibabu.
Alisema majaribio mengi yamefanyika lakini hayakupata mafanikio, kwa kuwa yalikuwa yakitumia teknolojia ya zamani kutafuta vichochezi.
“Kuna utafiti umewahi kufanyika nchini Thailand ambao ulifanikiwa kwa asilimia 30 pekee, watu wengi walionekana kupata maambukizi, lakini ukichunguza Moderna, wao wanatumia teknolojia mpya na hiyo inaweza kuwa bora kwa maana inakuwa na risk (athari) kidogo. “Ikipatikana chanjo kuna imani maambukizi mapya yatamalizika, wenye virusi tutawadhibiti na watu wapya hawatapata ugonjwa, hii ina maana dunia itapata faida kubwa kwa kuzuia wenye maambukizi wasiambukize wengine,” alisema Songoro.
Alisema kufanikiwa kwa hatua zilizobaki za chanjo hiyo utakuwa mwarobaini kuliko hata kupata dawa.
“Chanjo itakuwa ni bora zaidi inasaidia maambukizi mapya na ndiyo changamoto tuliyonayo, ndiyo maana Ukimwi unaua na watu wengi wanakufa kutokana na magonjwa nyemelezi yanayosababishwa na VVU,” alisema Songoro.
Mkuu wa kitengo cha utafiti wa Ukimwi kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Lucas Maganga alisema tangu kuanza kwa janga la Ukimwi kuna tafiti mbalimbali zaidi ya 200 zimefanyika duniani.
Alisema chanjo zote zilikuwa na nia ya kuhakikisha mwili unatoa kinga kwa kutengenezwa visisimua mwili, kisha utoe kinga, hata hivyo chanjo ya VVU bado ilishindikana kuzuia virusi katika hatua ya mwisho ya majaribio.