Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAG abaini kasoro lukuki sekta ya mifugo

Muktasari:

  • Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 2023/24 ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu utoaji huduma za ugani kwa rasilimali za mifugo imebainisha maeneo yenye changamoto na kushauri hatua za kuchukua.

Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kuwa na mifugo ya aina tofauti, ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha huduma za ugani zinazotolewa zinawafikia asilimia tisa tu ya wafugaji nchini.

CAG imebaini upungufu wa asilimia 67 ya maofisa ugani nchini ambao unasababisha asilimia 91 ya kaya zinazojihusisha na ufugaji kukosa huduma za ugani, kinyume na matakwa ya Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 inayosisitiza uratibu madhubuti wa huduma hizo.

Ripoti hiyo ya 2023/24 ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu utoaji huduma za ugani kwa rasilimali za mifugo iliyowasilishwa bungeni jana Jumatano, Aprili 16, 2025 imebainisha uwiano wa maofisa ugani kwa mkulima Tanzania ulikuwa 1:2,800, ikiwa ni chini ya uwiano wa 1:500 uliopendekezwa na Benki ya Dunia.

Aidha, kulikuwa na upungufu wa asilimia 38 ya maofisa mifugo katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na asilimia 42 katika sekretarieti ya mkoa.

Kwa mujibu wa ripoti hali hiyo imesababisha ufanisi mdogo katika utambulisho, usajili na ufuatiliaji wa mifugo, upo upungufu katika usajili, utambulisho, na ufuatiliaji wa mifugo, ambapo ni jambo muhimu kwa huduma bora za ugani.

Asilimia 11 tu ya mifugo milioni 45.9 iliyokadiriwa ilipachikwa lebo za kielektroniki, ambapo ng'ombe walifikia asilimia 18 ya lengo, punda (16), mbuzi (3), na kondoo asilimia 4.

Sababu za changamoto hii ni pamoja na gharama kubwa za lebo za sikio, hofu ya wakulima kuhusu kodi na upungufu wa mipango ya kina.

Miongoni mwa Halmashauri za Wilaya zilizotembelewa Tanganyika ilisajili asilimia 61, Kongwa asilimia 11, Handeni asilimia 0.3, na hakuna mifugo iliyosajiliwa katika wilaya ya Bariadi.

Ikiwa asilimia 25 tu ya Halmashauri za wilaya 184 zilifanya shughuli za usajili na utambulisho wa mifugo. Katavi ilifikia asilimia 100 ya lengo, wakati Simiyu ilisajili asilimia 0. Dodoma na Tanga walifikia asilimia 75 na 60 ya lengo.

Huku ripoti imesema mfumo wa ufuatiliaji haukuwa na ufanisi, kwani ulitegemea ukusanyaji wa data kwa njia ya mikono kwa kutumia programu ya ODK, ambayo haikuwa na uwezo wa kuchanganua data.

Kwani lebo za sikio za kieletroniki ziligoma kusawazishwa bila skana za msimbo wa bari, hivyo kufanya mfumo kutokuwa na ufanisi, matokeo yake data za mifugo 5,068,617 hazikutumika katika kupanga au kuboresha huduma za ugani.

Zaidi ya hayo, Halmashauri za Wilaya ya Kongwa na Tanganyika hazikuwa na maofisa maalumu wa usajili wa mifugo, wakati Bariadi na Handeni, zilikuwa na maofisa hazikuweza kusajili na kufuatilia mifugo 430,176 na 140,474 katika mwaka wa 2021/22–2022/23.

Kwa mujibu wa CAG Charles Kichere amesema kampeni za uhamasishaji hazikufanywa ipasavyo, na hivyo wakulima walikosa ufahamu wa umuhimu wa usajili, hali iliyosababisha kushiriki kidogo na kudhoofisha mfumo wa ufuatiliaji na huduma za ugani.

Upungufu wa rasilimali kwa huduma bora za ugani: watu, fedha, miundombinu na vifaa vya kazi.

Miongoni mwa changamoto zilizobainika kuhusu utoaji wa rasilimali za binadamu, fedha, miundombinu, na vifaa vya kazi kwa huduma za ugani ni upungufu wa asilimia 67 wa maofisa ugani wa mifugo nchini.

“Ukaguzi ulionyesha upungufu mkubwa wa maofisa ugani wa mifugo, ambapo asilimia 67 ya nafasi zinazohitajika zilikuwa hazijajazwa. Kati ya maofisa 13,279 waliokuwa wanahitajika, maofisa 4,406 pekee walikuwapo. Katika baadhi ya halmashauri za wilaya, upungufu ulifika hadi asilimia 86,” amesema CAG katika ripoti hiyo.

Hali hiyo ilisababisha ofisa mmoja wa ugani kulazimika kuhudumia hadi vijiji saba vilivyotawanyika kijiografia, jambo lililoathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora. Vilevile, kulikuwa na upungufu wa asilimia 38 ya maofisa madaktari wa mifugo katika ngazi ya Halmashauri za Serikali za Mitaa (LGA), na upungufu wa asilimia 42 katika ngazi ya mikoa.

Hali hii ilisababisha kazi za kitaalamu za mifugo kufanywa na watu wasio na sifa, na hivyo kuhatarisha afya ya mifugo.

Uwezo Hafifu wa Halmashauri

Katika halmashauri zilizokaguliwa, ni jumla ya Sh829.93 milioni tu zilizohifadhiwa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya mifugo, huku Sh277.63 milioni zikiwa hazikuhifadhiwa kama ilivyopaswa, kwani mapato ya mifugo yalielekezwa katika sekta nyingine kama afya na elimu.

Halmashauri za Sengerema, Monduli, Longido na Tanganyika hazikuhifadhi kiasi chochote kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya mifugo. Kwa, halmashauri za Kongwa na Hanang ziliweza kuhifadhi zaidi ya asilimia 15 kama ilivyopangwa, huku halmashauri nyingine zikiwa chini ya kiwango hicho.

Amesema huduma za ugani ziliwekwa kando katika mipango mikuu ya kitaifa, ambapo zilipewa chini ya asilimia sita ya uwekezaji wote katika Mpango Mkuu wa Mifugo na asilimia 2.2 pekee katika Mpango wa Mageuzi ya Sekta ya Mifugo (LSTP).

Huduma za Ugani

Kwa upande wa ufuatiliaji wa huduma za ugani ulikwamishwa na mfumo uliopo wa utoaji taarifa wa siku hadi siku (day-by-day), ambapo maofisa ugani walikuwa wakiripoti kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia halmashauri, bila kuwa na uhusiano wowote wa moja kwa moja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mfumo huu ulipunguza uwezo wa kitaalamu wa wizara kufuatilia ubora wa huduma na kuwawajibisha maofisa.

Vilevile, amesema ukosefu wa mifumo rasmi ya mawasiliano kati ya wizara na halmashauri ulisababisha matumizi hafifu ya maofisa ugani.

Ripoti zinaonesha katika maeneo mengi, maofisa ugani walitumika kwenye majukumu yasiyo ya ugani kama ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi, hali iliyowapotosha kutoka katika majukumu yao ya msingi.

Mabwawa ya kuogeshea mifugo

CAG amesema ukaguzi ulibaini kulikuwa na upungufu wa asilimia 66 wa mabwawa ya kuogeshea mifugo kote nchini. Katika maeneo yaliyotembelewa, asilimia 39 ya mabwawa yaliyopo hayakuwa yanatumika, jambo lililochangia kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na kupe. Hali hii ilisababisha visa 15,375 vya magonjwa na vifo vya mifugo 1,398.

Pia, nchi ilikuwa na uhaba wa vituo vya kutengeneza na kuhifadhi gesi ya “liquid nitrogen,” ambapo vituo viwili pekee vilikuwa vikifanya kazi Arusha na Mwanza. Hali hii iliwalazimu wafugaji kusafiri umbali mrefu kwa gharama kubwa kutafuta huduma hizo.

Ukosefu wa mafunzo

Katika ripoti hiyo, CAG Kichere amesema maofisa ugani walikosa mafunzo ya kutosha ili kuendana na mbinu za kisasa katika sekta ya mifugo. Katika Wilaya ya Kilosa, mafunzo yalipangwa kufanyika mara moja tu katika kipindi cha miaka mitano (2019/20–2023/24), lakini hata hilo halikufanyika.

Vilevile, Wilaya ya Handeni ilipanga kufanya mafunzo 20 lakini ilitekeleza tisa tu asilimia 45. Wilaya za Kongwa na Tanganyika hazikupanga kabisa mafunzo yoyote, jambo lililowaacha maofisa bila fursa ya kuongeza ujuzi. Kukosekana kwa mafunzo kulichangia utegemezi wa mbinu za zamani za ufugaji, na hivyo kupunguza ufanisi wa huduma za ugani kwa wafugaji.

Hawakuwa na pikipiki

Ukosefu wa vifaa vya kazi na usafiri uliathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za ugani. Takriban asilimia 66 ya maofisa ugani hawakuwa na pikipiki, hali iliyowazuia kufikia maeneo ya mbali.

Katika baadhi ya mikoa, pikipiki moja ilihudumia hadi vijiji 13. Zaidi ya hayo, maofisa wengi hawakuwa na vifaa muhimu vya kazi, hali iliyopunguza ubora wa huduma zao kwa wafugaji.