Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya nyama ilivyoleta maumivu Pasaka

Muktasari:

  •  Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Nyama Tanzania, hadi Machi 26, 2024, bei ya wastani ya mifugo (ng’ombe na mbuzi) katika mnada wa Pugu imepanda kidogo ikilinganishwa na bei ya wiki iliyotangulia

Dar/mikoani. Bei ya nyama ya ng’ombe kwa siku mbili za sikukuu ya Pasaka katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam imeongezeka kutoka wastani wa Sh8,000 kwa kilo hadi kufikia Sh11,000 huku baadhi ya maeneo ikiuzwa hadi Sh15,000.

Kupanda kwa bei hizo kulishuhudiwa kuanzia Machi 31 hadi leo Jumatatu Aprili mosi na sababu ya kupanda zikitajwa ongezeko la bei ya ng’ombe.

Imeelezwa kuwa bei ya ng’ombe mwenye uzito wa kilo 100 imepanda kutoka Sh800,000 hadi kufikia kati ya Sh900,000 na Sh950,000.

Bei ya nyama kwa Dar es Salaam ambayo awali ilikuwa ikiuzwa kwa Sh8,000 kilo moja katika  maeneo ya Kimara Korogwe sasa inauzwa kwa Sh11,000, Tabata Sh10,000,  Chanika Sh15,000, Tegeta Sh10,500, Bunju Sh11,000,  Kinondoni Sh10,500 mpaka Sh11,000 na Buguruni ni kati ya Sh9,000 na Sh10,000.

Kwa mujibu wa takwimu za  Bodi ya Nyama Tanzania, hadi Machi 26,2024, bei ya wastani ya mifugo (ng’ombe na mbuzi ) katika mnada wa Pugu imepanda kidogo ikilinganishwa na bei ya wiki iliyotangulia.

Ongezeko hilo la bei ilichangiwa na kupungua kwa ugavi wa ng’ombe na mbuzi mnadani hapo.

Ng’ombe wa kilo 200 na kuendelea, ameuzwa kwa Sh1.8 milioni ikilinganishwa na wiki moja kabla alipouzwa Sh1.425 milioni na yule mwenye kilo100 aliuzwa kwa Sh1.275 wakati awali aliuzwa kwa Sh950,000.

Mkoani Mwanza, bei ya kiteweo hicho katika maeneo imeongezeka kwa wastani wa Sh1,000 kwa kilo moja.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini bei ya nyama ya kawaida (mchanganyiko) imeongezeka kutoka Sh7,000 hadi Sh8,000 kwa kilo.

Inaelezwa kuwa kilo moja ya maini imepanda kutoka Sh8,000 hadi Sh10,000 huku utumbo nao ukipanda kutoka Sh5,000 hadi Sh6,000.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu, Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Lucas Chassama amesema bei ya nyama huamuliwa na soko.

“Hili ni soko huria, hakuna namna ya kupanga bei, nguvu ya soko ndiyo inayoamua bei,” amesema.

Muuza nyama katika soko la Vingunguti Vincent Zacharia amesema kwa kipindi cha sikukuu nyama huwa wanauza kwa Sh 10,000 sikukuu ya Pasaka lakini wameanza kushusha sasa na sikukuu ya Eid El Fitr bei hiyo itapaa tena kutokana na mahitaji kuongezeka.

“Tumeanza kushusha kufikia Sh9, 000 lakini itapanda tena sikukuu ya Idd kutokana na mahitaji kuongezeka,” alisema.

Mfanyabiashara wa nyama katika Soko la Vingunguti, Joel Meschak ameiambia Mwananchi kuwa bei ya jumla ya kitoweo hicho ilikuwa Sh8, 500 hadi Sh10, 000 na wafanyabiashara wengine wanakwenda kuuza Sh11,000 na kuendelea.

“Sababu ya bei kupanda ni mahitaji kuongezeka, gharama za usafiri na bei ya ng’ombe. Wa kilo 100 amepanda kutoka Sh800,000 hadi kufikia Sh900,000 hadi Sh950,000,” alisema

Beatrice Joseph, mkazi wa Kimara Korogwe Dar es Salaam, alisema Pasaka walinunua nyama kwa Sh11, 000.

“Kipindi cha sikukuu wananchi tunapitia maumivu makali sana, nilichojifunza sikukuu nyingine nitafanya manunuzi kabla mapema kuepuka hizi ongezeko la gharama,”alisema.

Aisha Jumanne, mkazi wa Tabata alisema Machi 31, 2024 bei ya nyama ilikuwa Sh10,000 kutoka Sh8,000 lakini leo imeshuka hadi Sh9,000.

Mkoani Mwanza, muuzaji wa nyama eneo la Buhongwa, Alphonce Fortunatus ametaja mfungo wa Ramadhani na sikukuu ya Pasaka kuchangia ongezeko la bei ya kitoweo hicho. 

Amesema kilo moja ya maini imepanda kutoka Sh8,000 hadi Sh10,000 na utumbo ikipanda kutoka Sh5,000 hadi Sh6,000.

"Kipindi cha Sikukuu matumizi ya nyama yanaongezeka, lakini wanyama nao wanachinjwa kwa wingi, hivyo kusababisha upungufu ndiyo maana tunalazimika kuongeza bei ili tupate faida," amesema Fortunatus.

Kutokana na ongezeko hilo, mamalishe eneo la Buhongwa jijini humo, Leah Jumanne amesema amelazimika kuongeza bei ya supu kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 ikiwa na finyango nne za nyama.

"Hatuna namna kwa sababu buchani bei imeongezeka, sasa nasi tunalazimika kuongeza bei ili angalau tupate faida, japo wateja wanalalamika lakini wanakula," amesema Leah.

Ongezeko hilo limemgusa Emmanuel Sabiba ambaye ameiomba Serikali na Bodi ya Nyama Tanzania kufuatilia upandishaji holela wa kitoweo hicho ili kuleta unafuu kwa wananchi hasa waliopo kwenye mfungo wa Ramadhan.

"Kwa mfano sasa hivi ndugu zetu Waislamu wamefunga na sisi Wakristo tulikuwa kwenye mfungo lakini bei ya nyama ambayo katika jamii yetu ni kitoweo pendwa imeongezeka. Hii ni kutuumiza na kuathiri mfungo wetu," amesema.