Baba miaka 30 jela kwa kuzini mwanaye

Muktasari:
- Baba huyo alishtakiwa kwa kuzini na binti yake tarehe tofauti kati ya Januari hadi Desemba 2023 katika eneo la Kung'ombe wilayani Bunda, mkoa wa Mara, kinyume na kifungu cha 158 (1) cha Kanuni ya Adhabu.
Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Musoma, imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mkazi wa Bunda, aliyohukumiwa kwa kosa la kuzini na binti yake wa kumzaa aliyekuwa na umri wa miaka 12.
Kulingana na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kosa la kuzini na ndugu wa damu (incest by male) huangukia kifungu cha 158 cha sheria hiyo, na ni tofauti na kosa la kubaka linaloangukia kifungu 131.
Kifungu cha 158 cha Kanuni ya Adhabu, kinasema mwanaume yeyote ambaye amekatazwa kufanya ngono na mwanamke yeyote ambaye anamjua kuwa ni mjukuu wake, binti yake, dada yake au mama yake, atakuwa ametenda kosa hilo.
Baba huyo alishtakiwa kwa kufanya kitendo hicho na mtoto wake ambaye alikuwa wanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Kung’ombe, kwa nyakati tofauti kati ya Januari hadi Desemba 2023.
Mahakama katika hukumu yake iliyotolewa Aprili 10,2025 na Jaji Marlin Komba, baada ya kutupilia mbali rufaa ya baba huyo aliyoikata kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda.
Jaji Komba alisema baada ya kupitia sababu za rufaa na ushahidi uliokuwa umetolewa kwenye kesi ya msingi, Mahakama Kuu imeona upande wa mashitaka ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.
Awali Mahakama ya Wilaya ya Bunda ilimtia baba huyo hatiani katika kesi ya msingi ya jinai baada ya kujiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo.
Mahakama ilimuhukumu adhabu hiyo baada ya kuthibitishwa kuwa alijamiiana na maharimu wake kinyume na kifungu cha 158(1) cha Kanuni ya Adhabu.
Kesi ya msingi
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, baba huyo alitenda kosa hilo kwa tarehe tofauti kati ya Januari hadi Desemba 2023 katika eneo la Kung'ombe wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.
Ilielezwa katika ushahidi kwenye kesi ya msingi kama ulivyorejewa kwa muhtasari katika hukumu ya Mahakama Kuu, mtoto huyo alieleza kuwa Desemba 12,2023 jioni baba yake alimwambia wakaokote kuni.
Alieleza kuwa walipofika mahali walipopanga kukusanya kuni hizo, baba yake alimuamuru avue nguo zake na alimvua nguo na kuanza kumfanyia kitendo hicho hadi alipokutwa na mtoto wake mwingine (dada wa mwathirika wa tukio hilo).
Ilielezwa kuwa kufuatia kelele zilizopigwa katika eneo hilo watu wengi walifika wakiwemo majirani, waliompeleka mrufani Kituo cha Polisi Bunda.
Katika rufaa hiyo, baba huyo alikuwa na sababu nane ikiwemo upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha vipengele muhimu vya kosa pasipo shaka yoyote na kuwa ushahidi wa mashahidi haukuwa wa kuaminika.
Nyingine ni ushahidi uliotolewa haukutosha kuunga mkono hukumu bila shaka yoyote, upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha suala la ushahidi wa vinasaba (DNA), ushahidi mwingine wa kitaalamu unaomuhusisha na kosa hilo na mahakama kukosea kukubali baadhi ya vielelezo kinyume cha sheria.
Katika rufaa hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Beatrice Mgumba, huku mrufani akijitetea mwenyewe.
Kuhusu hoja ya kuthibitisha uhusiano kati yao, wakili huyo amesema shahidi wa nne (dada wa mwathirika) alishuhudia kitendo hicho shambani kati ya baba yake na mdogo wake.
Amesema ushahidi mwingine ni wa shahidi wa tano aliyekuwa mke wa mrufani ambaye alithibitisha huyo ni binti yao.
Akijitetea mahakamani hapo, mrufani alisema ana watoto saba na wengine watatu wa dada yake (aliyefariki) ambao anawalea ni mkulima na kwa kuwa familia yake ni kubwa aliiomba Mahakama imuachie huru.
Uamuzi Jaji
Jaji Komba amesema kwa ujumla, mrufani analalamika kwamba kosa aliloshtakiwa halikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika jambo ambalo halina shaka.
Jaji huyo amesema kwa kuwa hiyo ni Mahakama ya kwanza ya Rufaa, anauchambua ushahidi wote na sababu za rufaa na majibu ya yaliyotolewa na upande wa mjibu rufaa.
Kuhusu uhusiano, amesema shahidi wa kwanza, wa nne na wa tano, walishuhudia kwamba mrufani ni baba wa mwathirika hivyo anaona kosa lilithibitishwa kwa kiwango kinachohitajika.
“Kwa kuwa kosa lilifanyika kwenye eneo la wazi na shahidi wa nne alieleza wakati wa kesi kuwa ilikuwa mchana, ina maana alifanikiwa kuona wazi na anawafahamu wote mrufani na mwathirika hivyo aliwatambua. Naona hakukuwa na haja ya DNA kama mrufani alitambuliwa katika eneo la tukio na shahidi wa kwanza, wa tatu na nne.
Baada ya kuchambua sababu zote Jaji alitupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa sifa na kueleza kuwa shitaka dhidi ya mrufani lilithibitishwa pasipo kuacha shaka.