Baba ampaka chumvi mwanaye, amshushia kipigo kisa Sh1,200

Muktasari:
- Mtoto mwenye umri wa miaka minane (jina linahifadhiwa) mkazi wa mtaa wa Mission jijini Mwanza anaugulia majeraha kwenye makalio baada ya kuchapwa kwa waya huku akiwa amepakwa chumvi kwenye kwa tuhuma za kuiba Sh1, 200.
Mwanza. Mtoto mwenye umri wa miaka minane (jina linahifadhiwa) mkazi wa mtaa wa Mission jijini Mwanza anaugulia majeraha kwenye makalio baada ya kuchapwa kwa waya huku akiwa amepakwa chumvi kwenye kwa tuhuma za kuiba Sh1, 200.
Ukatili dhidi ya mtoto huyo anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Sahara jijini Mwanza unadaiwa kutendwa na baba yake mzazi.
Mwalimu wa darasa ndiye aliyebaini majeraha ya mtoto huyo kwenye makalio yote mawili baada ya kumtilia shaka kutokana na kuchechemea kila alipotembea.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mission, Musa Fereji amesema baada ya kuhojiwa, mtoto huyo alieleza jinsi alivyopata majeraha hayo katika tukio lililotokea Februari Mosi, 2021.
“Baada ya kumpokea mtoto huyo ofisini alipoletwa na mwalimu wake, tulimhoji ndipo tukabaini kuwa majeraha hayo yalitokana na fimbo aliyochapwa na baba yake mzazi,” amesema Fereji
Akizungumza akiwa chini ya ulinzi, mama wa kambo wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Auliditensia Bwire amesema siku ya tukio, mume wake aliyemtaja kwa jina la Rahman Suleiman alimtuhumu mtoto wake kuiba Sh1, 200 ndipo alipoanza kumchapa huku akimpaka chumvi kwenye makalio.
“Mwanzoni alianza kumchapa akitumia fimbo ya mti lakini ulipokatika akaanza kumchapa kwa kutumia waya ambao naamini ndiyo umemsababishia mtoto madhara kutokana na ile chumvi aliyopakwa,” amesema Auliditensia
Baba mzazi anayetuhumiwa kutenda kosa hilo alitoroka muda mfupi kabla ya mgambo waliotumwa na uongozi wa mtaa kufika nyumbani kwake.
Mwalimu mkuu msaidizi shule ya msingi Shahara, Beata Lema amesema baada ya kumwona mtoto huyo akipata shida kunyanyua miguu wakati wa kutembea aliamua kumhoji ndipo akagundua ukatili huo na kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa.
Mhuduma wa afya ngazi ya jamii kata ya Pamba, Zabina Wandwi amewashauri wazazi na walezi kuepuka kutoa adhabu za kikatili kwa watoto kwa sababu licha ya kuwaathiri kimwili, pia huwasababishia madhara ya kisaikolojia.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro kuzungumzia tukio hilo zinaendelea.