Baadhi ya maeneo ya Dar, Z’bar kukosa umeme

Muktasari:
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na kitengo cha mawasiliano cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imesema sababu ya baadhi ya maeneo kukosa umeme inatokana na matengenezo ya mashine tatu za kituo cha Ubungo II
Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linawataarifu wateja wake wa Dar es Salaam na Zanzibar kuwa kutakuwa na upungufu wa upatikanaji wa umeme kwa baadhi ya nyakati na maeneo.
Upungufu huo utatokana na kufanya maboresho makubwa yanayohusisha matengenezo ya mashine tatu za kituo cha Ubungo II, uwekaji wa transfoma kubwa la MVA 300 kwenye kituo cha kupoza umeme cha Ubungo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Februari 16,2019 na kitengo cha mawasiliano cha Tanesco imeeleza maboresho hayo yanafanyika ili kukiongezea uwezo kituo cha Ubungo II na kwenda sambamba na ukuaji wa mahitaji ya jiji la Dar es Salaam kutakuwa na mapungufu ya upatikanaji wa huduma ya umeme kwa maeneo tajwa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Kampuni ya Songas itafanya matengenezo kinga katika mashine zake ambapo yatakamilika Juni, 2019.
Ilieleza mashine hizo za Ubungo II na Songas zimeungwa katika mfumo wa usambazaji umeme wa msongo wa kilovolti 132 wa Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar na hivyo kusababisha mapungufu katika maeneo tajwa.
“Wataalamu wetu kwa kushirikiana na Mkandarasi Kampuni ya SIEMENS kutoka nchini Sweden wanaendelea na matengenezo ya mashine na ubadilishaji wa vipuri ili kuongeza ufanisi zaidi katika uendeshaji wa mitambo hii na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar,” ilieleza taarifa hiyo
“Huduma ya umeme haitakosekana kwa kipindi chote cha matengenezo ila kwa baadhi tu ya siku na nyakati,”.