Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atupwa jela maisha kwa kusafirisha dawa za kulevya

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu John Juma ‘Vunjabei’ kifungo cha maisha jela na baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 595 za bangi na kumiliki kilo 59.20 za mbegu za mmea huo.

Tabora. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Tabora, imemhukumu John Juma maarufu kwa jina la Vunjabei, kutumikia kifungo cha maisha jela kwa makosa mawili, likiwamo la kusafirisha kilo 595 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Lakini katika kosa la pili, mshitakiwa huyo Mahakama Kuu imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la pili la kumiliki mbegu za kuzalisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 59.20 kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Tabora, Dk Adam Mambi alisema kwa kuwa adhabu zote mbili zitatumikiwa kwa pamoja, mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha maisha jela.

Hukumu hiyo imetolewa Mei 5, 2026 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa katika tovuti ya mahakama leo Mei 8, 2026 ambapo Jaji ameagiza pia kuteketezwa kwa kielelezo P3 ndani ya mwezi mmoja, ambacho ni bangi pamoja na mbegu.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kosa hilo lilitendeka Septemba 17, 2021 katika kijiji cha Miyega-Mwakashindye katika wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora ambapo alikamatwa na magunia 19 yakiwa na bangi yenye uzito wa kilo 595.56.

Katika shitaka la pili, alishitakiwa kwamba siku hiyo hiyo na katika eneo hilo hilo, alipatikana na gunia moja lenye uzito wa kilo 59.20 likiwa na mbegu za bangi.

Mshitakiwa katika utetezi wake, alikanusha shitaka hilo na kusimulia kile kilichotokea siku anakamatwa ambayo ulikuwa ni usiku wa manane.

Alieleza kwamba alikuwa anakaa peke yake nyumbani kwake kwenye chumba kimoja ambapo usiku maofisa wengi wa polisi walifika nyumbani kwake wakimtuhumu aliiba pikipiki na walimkamata kwa kushindwa kuthibitisha umiliki.

Alijitetea kuwa baada ya siku tano, maofisa wa polisi walimwambia kuwa alikamatwa kwa sababu walipata bangi nyumbani kwake na kusisitiza kuwa hahusiki nayo na viongozi wa kijiji hawakuhusika wakati wa kukamatwa kwake.


Hukumu ya Jaji

Katika hukumu hiyo, Jaji Mambi alisema swali la msingi mbele ya mahakama hiyo ilikuwa ni kwamba je upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi au mashtaka yasiyo na shaka dhidi ya mtuhumiwa na kuwezesha kutiwa hatiani.

“Upande wa mashtaka ndio unabeba jukumu la msingi la kuthibitisha hilo. Hii katika sheria ina maana kwamba mzigo mkuu ni juu ya  mshitaki (mwendesha mashitaka),”alisema Jaji Mambi katika hukumu hiyo na kuongeza kusema:-

“Kwa kuwa mzigo upo kote kwa Jamhuri, mtuhumiwa hana mzigo au jukumu la uthibitisho isipokuwa katika kesi chache angekuwa na mzigo huo”

“Ni kanuni kuu ya sheria kwamba kwa upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha  hatia ya mtuhumiwa katika biashara ya kesi za dawa za kulevya, na ni lazima athibitishe kuwa dawa zilizokamatwa kweli ni bangi,”alieleza Jaji.

Jaji alirejea ushahidi wa shahidi wa kwanza, Bonavencha Masembu, alieleza namna alivyopokea magunia 19 yaliyokuwa na majani yaliyodhaniwa ni bangi na baada ya kufanya uchunguzi wa kimaabara, alithibitisha kuwa ilikuwa ni bangi.

Kwa mujibu wa Jaji, ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ambao walishuhudia kukamatwa kwake, unaonyesha kuwa mshitakiwa alikamatwa na bangi na kwamba hana mashaka upande wa mashitaka ulithibitisha juu ya suala hilo.

“Kwa kuzingatia ushahidi wa upande wa mashtaka ni wazi kuwa mshtakiwa alipatikana  na kukamatwa akiwa na dawa za kulevya,”alisema Jaji na kuongeza;-

“Katika suala hili, ninaona mshitakiwa alipatikana akiwa na dawa za kulevya na mbegu ambazo zinatengeneza kosa aliloshitakiwa nalo na alishindwa kueleza ni kwa namna gani alizipata dawa hizo za kulevya au zilifikaje mikononi mwake.

“Ushahidi wa Jamhuri unaonyesha wazi kwamba vipengele muhimu vya ushahidi juu ya kupatikana na dawa za kulevya vimetimizwa katika kesi hii.

“Ushahidi hasa wa shahidi namba 2 uliweka wazi kuwa walienda Kijiji cha Mwakashindye kufanya operesheni ya Polisi iliyofanikisha kukamatwa kwa Juma John "Vunjabei" akiwa na magunia na mifuko yenye dawa hizo.

“Ukiangalia utetezi wake, alikanusha mashtaka, alidai kwamba hakupewa hati ya upekuzi na hati ya kukamata na maofisa wa polisi walipopekua nyumba yake.

“Nimechambua kwa makini ushahidi na mlolongo wa ushahidi na matukio ya kukamatwa kwa mtuhumiwa. Uchambuzi wangu unaonyesha utetezi wake kwamba alikamatwa kwa tuhuma za wizi pikipiki ni utetezi wa kujinasua.

“Cheti cha kukamata ambacho ni kielelezo namba 4 kilichosainiwa na mtuhumiwa kilitolewa na kukubaliwa na mahakama hii na pia iliifanya mahakama hii kuamini kwamba  ushahidi wa utetezi ulikuwa hauaminiki,”alieleza Jaji Mambi.

Kutokana na uchambuzi huo, Jaji Mambi alisema mahakama imemtia hatiani kwa makosa yote mawili na kwamba kosa la kwanza atatumikia kifungo cha maisha na la pili kifungo cha miaka 30 jela na adhabu hizo mbili zitatumikiwa kwa pamoja.