Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atengeneza filamu kutangaza utalii Mlima Kilimanjaro

Mwongozaji wa filamu, Ram Ally K akiwa pamoja na mshirika mwenzake Elizabeth Mrembo, Mtanzania mwenye asili ya Kichina wakiwa kwenye mapumziko njiani wakielekea Kibo Hut, katika safari ya kupandisha Mlima Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Mtanzania huyo amesema wamelenga kuimarisha juhudi za Tanzania za kulinda urithi wa asili na kuutangaza utalii wa nchi kwa soko la kimataifa, hususan China.

Dar es Salaam. Mwongozaji mzawa wa filamu anayefanya vizuri ndani na nje ya nchi, Ram Ally, amebuni na kutengeneza filamu mpya ya “Guardians of the Peak Season I: Kumbatia Asili, Linda Kesho” yenye mahadhi ya filamu bora ya utalii ya Tanzania.

Akishirikiana na raia wa Tanzania mwenye asili ya China, ambaye pia ni Msimamizi na Mratibu wa Mradi, Elizabeth Mrembo, filamu hiyo imebobea kutangaza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na utalii endelevu katika Mlima Kilimanjaro.

Akizungumzia filamu hiyo mwishoni mwa wiki, Ally, anayetamba na filamu ya “Nyara: The Kidnapping” inayopatikana kwenye mtandao wa filamu duniani wa Netflix, amesema wamelenga kuimarisha juhudi za Tanzania za kulinda urithi wa asili na kuutangaza utalii wa nchi kwa soko la kimataifa, hususan China.

“Uzinduzi wa filamu hii, unaendeleza jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia filamu ya The Royal Tour, katika kutangaza Tanzania kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji duniani.

“Uzinduzi wa Guardians of The Peak, hautakuwa tu onyesho la filamu, bali ni wito wa kuchukua hatua katika kulinda mazingira yetu, onyesho la uzuri wa asili wa Tanzania na uthibitisho wa nguvu ya ushirikiano katika kuhifadhi urithi wa kizazi kijacho,” amesema Ally.

Kwa mujibu wa Ally, filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Mei 2025 katika ukumbi wa Century Cinemax, Mlimani City, Dar es Salaam.

“Hii ni filamu ya kipekee inayochunguza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na utalii endelevu katika Mlima Kilimanjaro, sambamba na juhudi za Tanzania za kulinda urithi wa asili na kuutangaza utalii wa nchi kwa soko la kimataifa,” amesema Ally.

Amesema filamu hiyo imebeba mtazamo wa kipekee wa kitamaduni na kimataifa, uliosimamiwa na Elizabeth mwenye uzoefu kutoka China.

Ally amesema filamu hiyo ni mafanikio ya Mradi wa Ushirikiano wa Kimkakati kwa ajili ya Mazingira na Utalii, uliohusisha kampuni ya Ram Films, Zara Tanzania Adventures, Taasisi ya Tanzania-China Friendship Promotion Association (TCFPA) na Bodi ya Filamu Tanzania.

Amesema ushirikiano huo, umewezesha kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio, huku ukihimiza ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya filamu na taasisi za Serikali.

“Kwa kutambua umuhimu wa filamu hii, Bodi ya Filamu Tanzania imeidhinisha na kuunga mkono mradi huu kwa sababu unasaidia katika kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, hususan katika Mlima Kilimanjaro.

“Pia mradi huu unasaidia kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa, hasa katika soko la China na kuhamasisha sekta binafsi na Serikali kushiriki katika utalii endelevu,” alisema Ally.

Kwa upande wake, Elizabeth amesema mbali na kutumika kuadhimisha juhudi za uhifadhi wa mazingira, pia uzinduzi huo utawakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Serikali, wawekezaji, mashirika ya uhifadhi wa mazingira na washirika wa kimataifa.