Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyeua mtalaka mwenzake akwaa kisiki kortini

Muktasari:

  • Septemba 28, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Songea ilimhukumu Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha 08/691 KJ Chandarua mkoani Ruvuma, Sajenti Batsin Sanga, kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwaua kwa risasi mtalaka wake na mwanajeshi mwenzake.

Tanga. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa aliyokata askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi cha 08/691 KJ Chandarua mkoani Ruvuma, Sajenti Batsin Sanga, aliyekuwa akipinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuwaua kwa risasi mtalaka wake na mwanajeshi mwenzake.

Tukio hilo lilitokea Desemba 27, 2018 katika lango kuu la kambi hiyo, askari huyo mwenye namba za kijeshi MT81337, akiwa na bunduki aina ya SMG, aliwashambulia kwa risasi Veronica Kayombo na Sajenti Juma Uwesu, waliofariki papo hapo.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 14, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Othman Makungu na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Jaji Mwarija amesema baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, wamejiridhisha kuwa kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka kupitia mashahidi wa jamhuri pamoja na maelezo ya onyo ya mrufani ambayo alikiri kumuua mtalaka wake pamoja na mwanajeshi mwenzake.


Kesi ya msingi ilivyokuwa

Katika kesi ya msingi, Sajenti Batsin alipandishwa kizimbani kwa makosa mawili ya mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, ambapo katika kosa la kwanza alimuua Veronica (mtalaka wake) na kosa la pili siku hiyohiyo alimuua Sajenti Juma.

Awali, kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Yose Mlyambina, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 15 huku mrufani huyo akiwa shahidi pekee wa upande wa utetezi.

Siku ya tukio hilo, Veronica aliyekuwa amepewa amri na Mahakama iliyomruhusu kumchukua mtoto huyo na kukaa naye kipindi cha likizo kwani alikuwa akitunzwa na baba yake (mrufani), ambapo alienda mahakamani na kuchukua amri hiyo ili aipeleke kwa mrufani.

Baada ya kuipata, alienda kazini kwa mrufani akiwa na rafiki yake, Jamila Saidi (shahidi wa kwanza) na katika lango la kambi ya kijeshi, alikabidhi kwa MT.65751 Sajenti Daniel Mcharo (shahidi wa sita) ambaye aliipeleka kwa mkuu wa makarani kwa taratibu za kiofisi.

Shahidi wa 14, MT.118022 Henry Msagala alieleza kuwa alimpa mrufani bunduki aina ya SMG yenye namba NM 184641 (kielelezo cha tatu) na risasi 30.

Shahidi huyo alitoa kitabu cha silaha chenye maingizo kati ya Januari 11, 2018 hadi Mei 19, 2019 ili kuthibitisha kuwa kielelezo hicho cha tatu kilitolewa kwa mrufani.

Shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo, bunduki hiyo ilirudishwa na Mohamed Idd (shahidi wa 11) ikiwa na risasi 20 huku risasi 10 zikiwa zimetumika ambapo maganda yake yalikabidhiwa Aprili 15, 2019 kwa Sajenti Elia aliyeipeleka Kitengo cha Uchunguzi Dar es Salaam.

Watu waliokuwa eneo la tukio ambao ni shahidi wa kwanza, sita, nane, 11 na shahidi wa 13 walidai kuwa risasi zilizozababisha vifo vya marehemu zilifanywa na mrufani.

Shahidi wa kwanza, alieleza akiwa amekaa kwenye benchi na Veronica (marehemu), mrufani alitokea akiwa ameshika bunduki na kumuuliza amefuata nini, akamjibu wamehudumiwa.

Ghafla mshitakiwa alichukua bunduki hiyo na kumfyatulia risasi Veronica, kisha akaanza kumbikimbiza askari mwenzake aliyekuwepo eneo hilo na kumfyatulia risasi pia ambapo naye alifariki dunia.

Jamila alidai alifanikiwa kutoroka kwa kukimbia na alipokuwa anakimbia alisikia milio mingine ya risasi.

Ushahidi huo wa shahidi wa kwanza uliungwa mkono na shahidi wa sita, nane na shahidi wa 11 ambapo shahidi wa sita alidai Desemba 27, 2018, alimsindikiza mrufani mahakamani kusikiliza rufaa kati yake na Veronica (marehemu).

Shahidi wa 13 alieleza kuwa alitambua mgogoro baina ya mrufani na Veronica kuhusu malezi ya mtoto wao na kuwa siku ya tukio, yeye ndiye alimuamuru askari mwingine kumsindikiza mrufani mahakamani kwani sheria za kijeshi zinamtaka askari anayekwenda mahakamani kusindikizwa ili mrejesho utolewe pia.

Alieleza kuwa mahakama ilitoa amri ya kumtaka mrufani kumpeleka mtoto huyo kwa Veronica (marehemu) wakati wa likizo ya shule na amri hiyo itekelezwe kwa msaada wa ofisi yake.

Shahidi huyo aliiambia Mahakama kwamba siku ya tukio alisikia milio ya risasi lango kuu na alipotaka kutoka nje ya ofisi yake alishauriwa asifanye hivyo na ghafla akasikia milio ya risasi kwenye ofisi yake ambapo alimshuhudia mrufani akifyatua risasi mlangoni.

Alieleza kuwa baada ya askari wengine kufanikiwa kumdhibiti mrufani, alimweleza kuwa ana bahati sana.

Baada ya kukamatwa, maelezo ya onyo ya mrufani yalirekodiwa na shahidi wa 15 ambapo kwa mujibu wa ushahidi wake, mrufani huyo alikiri kutenda kosa hilo, maelezo ambayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo cha tisa bila pingamizi lolote.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa maelezo ya ziada ya mrufani huyo yalirekodiwa Desemba 28, 2018 na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Felista Ngwelo (shahidi wa saba) ambapo pia alikiri kutenda makosa hayo.


Utetezi

Katika utetezi wake, mrufani alithibitisha siku ya tukio alikuwa zamu na alipewa bunduki (kielelezo cha tatu) na baada ya kuchukua bunduki na kutembea takriban hatua 6 au 8 kutoka kwenye chumba cha kuhifadhia nguo, alisikia milio ya risasi.

Alieleza kuwa alipojaribu kuangalia alimuona shahidi wa 13 ambaye alimuamuru arudishe bunduki na baada ya kufanya hivyo askari wengine walimpeleka hadi lango kuu ambapo aliona maiti mbili.

Alidai kuwa baadaye alifungiwa na siku iliyofuata, alifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka huku akipinga shahidi wa upande wa mashtaka akidai kuwa bunduki iliyotumika katika tukio hilo si ile aliyokabidhiwa na PW14 na kukana kuandika maelezo ya kosa.

Baada ya kuzingatia upande wa mashtaka na ushahidi wa upande wa utetezi, Mahakama Kuu ilijiridhisha kuwa, makosa yote mawili yamethibitishwa dhidi ya mrufani,ambapo Jaji aliegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza, 14 na maelezo yake ya onyo.


Rufaa

Kutokana na kutoridhishwa na hukumu hiyo, mrufani huyo aliwasilisha hati ya rufaa iliyokuwa na sababu saba ikifuatiwa na hati ya nyongeza yenye sababu 14 ambapo baadaye wakili wake aliwasilisha hati ya pili ya nyongeza ya rufaa yenye sababu tatu.

Miongoni mwa sababu hizo ni kuhukumiwa kwake kulitokana na ushahidi usiotosha, unaopingana na usioaminika, kutiwa kwake hatiani kulitokana na ushahidi wa vielelezo ambavyo mlolongo wa uhifadhi wake haukuanzishwa na maelezo ya onyo yalikubaliwa bila utaratibu na Mahakama haikuzingatia utetezi wake.

Nyingine ni tatu, kwamba, taarifa zilizoonywa na zisizo za kisheria zilikubaliwa bila utaratibu, nne, kwamba, hukumu yake ilitokana na ushahidi wa shahidi ambaye hakuwa mtaalamu mwenye sifa na tano, kwamba, Mahakama Kuu haikuzingatia utetezi wake.

Sababu nyingine ni Mahakama ilikosea kisheria na kuwaruhusu wazee wa baraza kuvuka kuwahoji mashahidi badala ya kuuliza maswali yanayostahili, Mahakama ilikosea kumtia hatiani kwenye kesi ambayo haikuthibitishwa bila shaka yoyote.

Katika rufaa hiyo, mrufani huyo aliwakilishwa na mawili wawili huku upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) naye akiwakilishwa na mawakili wawili waandamizi wa serikali.

Baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa hiyo majaji hao wamesema baada ya kuchunguza rekodi hawakubaliani kuwa wazee wa baraza waliwahoji mashahidi kwani hakuna swali lolote la mzee wa baraza katika kurasa zilizorejelewa na wakili wa mrufani.

Jaji Mwarija amesema kinyume chake, maswali hayo yalilenga kupata ufafanuzi wa vipengele mbalimbali vya ushahidi wa mashahidi.

Kuhusu kesi hiyo kutothibitishwa,Jaji Mwarija amesema baada ya kugundua kwamba, mrufani alikuwa amekiri kutenda kosa hilo kupitia vielelezo vya nne na tisa na kuwa suala linaloangaliwa ni kuhusu bunduki ambayo ilitumika katika kutenda kosa ikiwa ni ile ambayo ilitolewa kwa mrufani katika siku husika au lah.

Jaji Mwarija akipitia sehemu ya maelezo ya onyo ya mrufani huyo ambaye alikiri baada ya kumuona mtalaka wake hasira zilimjia na alipomuuliza amefuata nini akamjibu hawezi kuongea naye anaongea na mkuu wake wa kambi,alijikuta akikoni silaha na kumpiga risasi mbili.

Aliendelea kukiri kwamba: “Baada ya hapo kwa kuwa mkuu wa kambi alikuwa ofisini kwake, niliondoka kumfuata nikiwa na silaha yangu kabla ya kufika ofisini nilikutana na Sajenti Juma Mkele nakumbuka nilimpiga risasi moja mgongoni wakati alikuwa ameanguka chini.”

Jaji Mwarija amesema ni kanuni kwamba, ungamo linalofanywa kwa hiari na mtuhumiwa ni ushahidi bora katika kesi ya jinai na kuwa ukiri huo wa kumfunga mshtakiwa, lazima uthibitishwe bila shaka yoyote na upande wa mashtaka kuwa umefanywa kwa uhuru na kwa hiari.

“Kukiri kwa mrufani kama inavyoungwa mkono na ushahidi wa shahidi wa 14 na 11,unatosha kuthibitisha pasipo shaka yoyote kwamba, ni bunduki ambayo ilitolewa kwa mrufani ambayo ilitumika katika kutenda kosa hilo. Ushahidi ulithibitisha pia kwamba, kosa hilo lilitendwa na mrufani.

“Kwa hiyo, tunaona kwamba hukumu ya mrufani juu ya makosa hayo mawili, ilikuwa na msingi. Kwa hiyo, tunaona kwamba, rufaa hiyo haina mashiko,” alieleza.

Jaji Mwarija amesema kabla ya kuhitimisha wanatoa maoni juu ya hukumu ya awali ambapo alikuhukiwa kwa makosa yote mawili na kuwa haikuwa sahihi, adhabu ya kunyongwa hadi kufa inapaswa kutolewa mara moja.

“Katika kesi za Agnes Doris Liundi dhidi ya Jamhuri, ambapo mrufani alitiwa hatiani kwa makosa matatu ya mauaji, Mahakama pamoja na mambo mengine ilisema: “Hukumu ya kifo ilipaswa kupitishwa kwa shtaka moja tu, hukumu kwa makosa mengine mawili kuruhusiwa kubaki kwenye rekodi.”

“Kwa msingi wa msimamo uliotajwa hapo juu, tunabadilisha sentensi na kutamka kwamba, hukumu iliyotolewa kwa mrufani kwa kosa la mauaji liwe kwenye hesabu moja pekee. Hatia kwenye hesabu ya pili inapaswa kubaki kwenye rekodi pekee,” amehitimisha.