Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyemuua mzazi mwenza, kumjeruhi mwanaye ahukumiwa kunyongwa

Muktasari:

  • Hukumu hiyo imetolewa Jumatano, Juni 3, 2026 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joachim Tiganga baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

Mbeya. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa Barnaba Mtewele, mkazi wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya mzazi mwenzake na ndugu wa mwanamke huyo.

Pia, Mahakama hiyo imemhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumjeruhi mtoto wake aliyemzaa na mwanamke aliyemuua.

Hukumu hiyo imetolewa Jumatano, Juni 3, 2026 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joachim Tiganga baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

Katika kesi hiyo, Barnaba alishtakiwa kwa kosa la kuwaua kwa makusudi mzazi mwenzake, Herriet Lupembe (37), aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Mbugani na mdogo wake, Ivon Tatizo aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Isenyela.

Pia, katika kesi hiyo ya jinai namba 6799/2025, Barnaba alishtakiwa kwa kosa lingine la kumjeruhi Daud Mtewele (7) ambaye ni mtoto wake aliyemzaa na marehemu Herriet, makosa ambayo yote aliyatenda Machi 31, 2023.

Katika kuthibitisha mashtaka hayo, upande wa Jamhuri ambao wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Augustino Magesa, uliwaita jumla ya mashahidi wanane na kuwasilisha vielelezo mbalimbali.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Barnaba alizaa na mwalimu Herriet Lupembe mtoto wa kiume, Daud Barnaba (7).

Katika ushahidi wake, mtoto huyo aliieleza Mahakama kuwa mara kadhaa baba yake alikuwa akija kula pamoja nao na kwamba wakati mwingine alikuwa akiingia chumbani kwa mama yake.

Alisema anachokumbuka siku ya tukio baba yake alimpiga mama yake na ndugu wa mama yake waliokuwa wakiishi pamoja kwa sululu, kisha akampiga na yeye kwa sululu hiyo hiyo.

Alisema baada ya kupigwa na sululu, alipoteza fahamu na kuvuja damu nyingi. Baada ya siku kadhaa alipata fahamu ndipo alipoeleza kuwa mhusika wa matukio yote ni baba yake mzazi.

Shahidi mwingine ni ndugu wa Herriet aliyeiambia Mahakama kuwa Daud akiwa hospitalini alimwambia kuwa baba yake ndiye aliyempiga kwa sululu mama yake, dada yake na yeye mwenyewe.

Daktari aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao, aliiambia Mahakama kuwa vifo vyao vimesababishwa na kuvuja damu nyingi.

Pia, mpelelezi wa kesi hiyo alieleza namna alivyopokea taarifa kutoka kwa balozi baada ya kumtafuta marehemu Herriet kwa simu bila mafanikio, kisha akaamua kwenda kwake ambako alikuta milango yote ikiwa imefungwa kwa ndani.

Hivyo, walilazimika kuvunja mlango na walipoingia ndani walikuta miili miwili ikiwa na majeraha huku damu ikiwa imetapakaa.

Polisi walipofika walikuta eneo la tukio kuna sululu kando ya miili hiyo miwili na mtoto Daud ambaye alikuwa amepoteza fahamu.

Kwa upande wa daktari aliyemtibu mtoto Daud, alidai kuwa Daud alijeruhiwa katika fuvu la kichwa na kuvuja damu nyingi, hali iliyosababisha kupoteza fahamu.

Upande wa utetezi ambao uliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Joyce Kasebwa, uliwaita mashahidi wanne akiwemo mshtakiwa mwenyewe ambaye alikana kuhusika na mauaji hayo na uliwasilisha kielelezo kimoja ambacho ni cheti cha ubatizo kinachoonyesha kuwa siku ya tukio mshtakiwa alisimamia ubatizo katika Kanisa la Anglikana Wilaya ya Chunya hadi usiku.

Ilielezwa kuwa ushahidi huo haukuthibitisha kama mshtakiwa alirejea nyumbani siku hiyo au la. Ushahidi wake uliungwa mkono na Katekista Mapunda na Joyce Kayombo.

Hata hivyo, Mahakama katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili, kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 11:30 jioni, ilitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa na mashahidi wake.

Jaji Tiganga alisema kuwa licha ya kuwasilisha cheti hicho, mashahidi hao hawakuweza kuieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alikwenda wapi baada ya ibada hiyo.

Hivyo, alikubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka na kumtia hatiani mshtakiwa Barnaba Daud Mtewele kwa makosa yote matatu aliyoshtakiwa nayo.

Baada ya Mahakama kumtia hatiani, Wakili wa Serikali, Magesa aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa mujibu wa sheria huku wakili wa upande wa utetezi akiomba Mahakama kuona namna ya kutoa adhabu kwa mtuhumiwa kwa sababu ilikuwa ni kosa lake la kwanza.

Akitoa adhabu hiyo, Jaji Tiganga alimhukumu mshtakiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kumuua Herriet Lupembe na Ivon Tatizo, pia kifungo cha miaka 10 kwa kumjeruhi mtoto wake Daud.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Mawakili wa Serikali Augustino Magesa na Geofrey Kibasa wamesema wameridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ili iwe fundisho kwa watu wengine.