Alichokisema Samia kuhusu ubaguzi wa kijinsia

Muktasari:

Makamu wa Rais wa nchini Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeweka mikakati na mipango madhubuti ya kuimarisha uchumi na kuondoa ubaguzi wa kijinsia katika nyanja zote muhimu.

Dar es Salaam.  Makamu wa Rais wa nchini Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeweka mikakati na mipango madhubuti ya kuimarisha uchumi na kuondoa ubaguzi wa kijinsia katika nyanja zote muhimu.

Mipango na mikakati hiyo imelenga kuondoa umaskini na kukuza uchumi kwa upana na ulinganifu ili kunufaisha jinsia zote.

Samia ameyasema hayo leo Jumatano Machi 4, 2020 wakati akifungua kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya wanawake duniani lililoandaliwa na Mtandao wa wanawake na katiba na Chama cha Waandishi wa habari wanawake (Tamwa).

Katika mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, makamu wa rais amesema halmashauri kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanawake zinatoa matokeo chanya.

Amesema kinachofanyika sasa fedha hizo zimekuwa zikitolewa kisiasa na matokeo yake zinaonekana kuwa na tija haba.

“Nazitaka halmashauri kupunguza utitiri wa vikundi kwa kuwapa fedha kidogo na badala yake watoe fedha za kutosha kwa vikundi vichache ili kupata matokeo chanya,” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa wanawake Tanzania (WFT), Profesa Ruth Meena amesema licha ya takwimu kuonyesha uchumi kukua bado mwanamke anakabiliwa na umaskini.

Amesema wanawake wanakumbwa na tatizo la umiliki wa rasilimali na ardhi huku takwimu zikionyesha ni asilimia nane tu ndiyo wanamiliki ardhi.