Akamatwa kwa tuhuma ya kumuua mpenzi wake wa zamani

kamanda wa polisi mkoa wa Njombe John Makuri Imori akizungumza na waandishi wa habari.
Muktasari:
- Jeshi la polisi Njombe linamshikilia mtuhumiwa wa mauaji ya mwanamke ambaye mwili wake ulikutwa msitu wa Tanwat mtoto wake akiwa pembeni.
Njombe. Jeshi la polisi mkoani Njombe linamshikilia Samwel Nduluhundu (38) mkazi wa Mtaa wa Ramadhani Halmashauri ya mji wa Njombe kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Felister Danda (24) ambaye alikutwa ameuawa na kutelekezwa katika misitu ya Tanwat huku mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili akiwa pembeni yake.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe, John Imori akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema mtuhumiwa huyo alidaiwa kutekeleza mauaji hayo kutokana wivu wa kimapenzi baina ya wawili hao.
Kamanda Imori amesema marehemu na mtuhumiwa huyo walikuwa wapenzi lakini baadae marehemu aliamua kukataa kuendelea na mahusiano hayo jambo ambalo mtuhumiwa hakukubaliana nalo.
"Mtuhumiwa hakukubaliana na maamuzi hayo ya marehemu na kumtaka amrudishie vitu ambavyo aliwahi kumnunulia lakini marehemu alikataa kurudisha akimwambia hata yeye amemtumia,”amesema.
Kamanda Imori amesema mtuhumiwa alimlaghai marehemu ampeleke kwa mganga wa kienyeji katika Wilaya ya Wanging’ombe atakayetibu tatizo lake la shingo ambalo alikuwa nalo tangu zamani.
“Alhamisi usiku mtuhumiwa alimchukuwa nyumbani kwake marehemu akiwa na mtoto wake kuelekea Wanging’ombe lakini walipofika eneo la msitu wa Tanwat ndipo inadaiwa alitekeleza mauaji hayo,”amesema.
Kamanda Imori amesema polisi walifika eneo la tukio siku ya pili na kukuta mwili wa marehemu, mtoto wake akiwa hai na helmet (kofia ngumu ya pikipiki) ambayo imechukuliwa kwa upelelezi.