Ahukumiwa miaka 60 jela kwa kumpa ujauzito shemeji yake

Siha. Mahakama ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro imemuhukumu Abedi Kingazi (36), mkulima mkazi wa Kijiji cha Matadi kwenda jela miaka 60 kwa makosa mawili ya kubaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa Shule ya Msingi Lemosho (17) wilayani humo ambaye ni shemeji yake.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 20 mwaka huu na Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Jasmin Abdul, baada ya kuridhika na ushahidi wa watu wanne akiwamo mwathirika mwenyewe na daktari.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, David Chishimba akisoma mashtaka mbele ya hakimu huyo amesema tukio hilo lilifanyika kwa tarehe tofauti tofauti mwaka 2022 huko Kijiji cha Matadi.

Amesema mshtakiwa alimdanganyi mwanafunzi huyo ambaye ni shemeji yake amuingilie ili apone ugonjwa uliokuwa unamsumbua wa kutokwa damu sehemu za siri na puani.

Ugonjwa huu uliomsumbua kwa muda mrefu ndipo mshitakiwa kuamua kwenda kwa waganga ili kupata tiba, na aliporudi alimwambia ili mwanafunzi huyo apone ugonjwa huo lazima amuingilie kimwili mara tatu kama mganga alivyosema ndipo apone bila kumwambia mtu.

Chishimba amesema mshtakiwa alifanikiwa kufanya unyama huo na kusababisha mwanafunzi huyo kupata ujauzito hivyo, mahakama kuamuru kwenda kutumikia kifungo cha miaka 60 jela kwa kuitumikia yote kwa pamoja

Kosa la kwanza miaka 30 ni kubaka kinyume na kifungu 130(1)(2)(e)na 131 cha sheria ya kanuni ya  adhabu sura ya 16 marejeo ya 2022, kosa la pili miaja 30 jela kumpa mwanafunzi mimba kinyume na kifungu 60 A (3)cha sheria ya elimu sura ya 353  hivyo kuitumikia yote kwa pamoja.

Mshtakiwa aliomba kupunguziwa adhAbu kuwa anafamilia inamtegemea, hata hivyo hakimu alisema ili iwefundisho kwa wengine akatumikie adhabu hiyo, kwani matukio ya ukatili yanazidi kuongezeka.