Afrika yakutana kujadili huduma za afya kwa wote

Muktasari:

Mkutano wa afya wa kimataifa, ‘Africa Health Agenda 2019’ umewakusanya pamoja watunga sera, watafiti na wadau mbalimbali wa masuala ya afya kujadili namna bara la Afrika linaweza kuongeza kasi hasa katika upatikanaji wa huduma za afya, ubora, vikwazo vya kiuchumi na uwajibikaji.


Kigali, Rwanda. Zaidi ya wadau wa afya 1,500 barani Afrika, wamekusanyika kujadili  uboreshaji huduma za afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi, Universal Health Coverage (UHC).

Mkutano huo wa kimataifa uliozikutanisha nchi zote barani Afrika 'Africa Health 2019' unaanza rasmi leo Jumanne Machi 5, 2019 huku ajenda kuu ikizungumzia uboreshaji huduma za afya kwa wote, ikiwa ni utekelezaji wa lengo namba tatu la mpango wa maendeleo endelevu.

Ajenda hiyo itakayojadiliwa kwa siku tatu, imekuja wakati Tanzania ikiwa katika mchakato wa kupeleka muswada wa huduma za afya kwa wote bungeni ifikapo Aprili, 2019 ili kutungiwa sheria.

Mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Utafiti na Tiba na Afya barani Afrika ‘Amref’, umewakusanya pamoja mawaziri wa afya na manaibu kote barani Afrika katika kujadili mustakabali wa lengo hilo na masuala mengine kuhusu afya yanayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.

Majadiliano hayo yanafanyika wakati ambapo kasi ya kimataifa ya kampeni ya afya kwa wote ikiwa juu.

Wakati huohuo, mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) utakaozungumzia ajenda hiyo unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, majadiliano ya kikanda yanayofanyika katika mkutano huu yatakuwa na fursa ya kuunda majadiliano ya kimataifa.

Bima ya afya ni mpango ulioandaliwa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kidunia ya afya katika nchi 17 wanachama wa UN kwenye kupokea Mpango wa Maendeleo Endelevu ulioanzishwa mwaka 2015.

Mkutano huo ni wa pili kufanyika ambapo awali ulifanyika mwaka 2017, nchini Kenya.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri kwenye mkutano huu