Afariki dunia ndani ya basi akitoka Kilwa

Baadhi ya mashuhuda wakiwa wamelizunguka gari lililo beba mwili wa marehemu Lukia wakiwa nje ya eneo la hispitali ya sokoine.
Muktasari:
- Sintofahamu yaibuka mochwari, Kaimu Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Mkoa Sokoine atoa ufafanuzi
Lindi. Rukia Saidi, mkazi wa Kijiji cha Pande, wilayani Kilwa amefariki dunia akiwa njiani kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Mkoa Sokoine.
Tukio hilo limetokea mchana wa leo Jumanne Machi 11, 2025. Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Shedrack Lusasi amethibitisha kupokewa mwili wa Rukia.
Zakia Yusufu, mama mdogo wa marehemu akizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali hiyo ya Mkoa wa Lindi, amesema Rukia amefariki dunia akiwa kwenye gari.

Baadhi ya mashuhuda wakiwa wamelizunguka gari lililo beba mwili wa marehemu Lukia wakiwa nje ya eneo la hispitali ya sokoine.
Sintofahamu mochwari
Zakia amesema walipofika geti kuu la hospitali hiyo walielekezwa kwenda mochwari kwa kupitia geti lingine, lakini walipofika wahudumu waliwazuia kuingia ndani wakisema hawana kitanda.
"Kondakta ndiye aliyekwenda kuwaambia tumepakia abiria amefariki dunia wakatuambia tuje geti hili. Wametugomea kupokea mwili mara mbili,” amesema.
“Nikawaambia basi kama wamekataa iacheni hapa. Wakaja watu wengine wakatuambia tuingie tukawaambia basi kwa sababu mmekataa mara mbili. Kuna kina kaka wakaja wakaniambia watanisaidia kwa sababu wameshakataa mara mbili, wakaanza kunisaidia kutafuta gari," amesema Zakia.
Amesema kitendo cha kukataliwa kupokewa mwili wa mwanaye kimemuumiza kwa kuwa walikaa nje ya hospitali hiyo kwa zaidi ya saa moja.
Akizungumzia malalamiko hayo, Kaimu mganga Mfawidhi, Dk Lusasi amesema mwili hauwezi kuingizwa mochwari kabla ya madaktari kuthibitisha kifo.

Baadhi ya mashuhuda wakiwa wamelizunguka gari lililo beba mwili wa marehemu Lukia wakiwa nje ya eneo la hispitali ya sokoine.
"Mwili hauwezi kuingizwa mochwari kabla kifo hakijathibitishwa. Sijui ni nani aliyewaambia waende geti dogo. Walipofika waliambiwa warudi ili madaktari waje wathibitishe. Ndugu walipoambiwa walisema hawawezi kurudi.
“Timu ya wafanyakazi ilifika na machela ili waingize mwili ndani ndugu waliendelea kukataa wakisema ninyi mlikataa na hata walipo shauriwa wakubali waliendelea kukataa na mwili ukabaki nje,” amesema.
Dk Lusasi amesema ndugu hao walitafuta gari wakaendelea kubaki eneo hilo.
“Sisi hatukujua walikuwa na lengo gani," amesema Dk Lusasi.
Mashuhuda wasimulia
Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo akiwamo Tausi Jafari ambaye alikuwa abiria wa gari alimokuwa Rukia akitokea wilayani Kilwa amesema alifariki dunia wakiwa njiani.
"Tumefika pale geti kubwa tukaambiwa tuje huku mochwari moja kwa moja, tulipofika wakatuambia hawana kitanda na geti hatufungui, baada ya muda wakaja na kitanda wakati huo gari la abiria lilikuwa limeondoka na limeshapatikana lingine ndipo watu wakagoma wasichukue maiti," amesema.
Abdallah Mtaji, abiria mwingine wa gari hilo amesema:
"Hii ni simanzi kubwa, wengine hatujawahi kushuhudia tukio kama hili. Tulifika tukawakuta wahudumu kule geti kubwa tukawaambia kwenye gari kuna mtu amefariki wakatuambia tuje geti hili, tulipofika wakafungua geti kisha wakafunga wakaenda kujadiliana, waliporudi wakatukatalia. Baadaye walikuja na kuhitaji tuingize ndani mwili tukakataa kwa sababu tumekaa nje zaidi ya saa moja. Tukawaambia hatutaki tutasaidiana tusafirishe mwili," amesema.
Mwili huo umesafirishwa baada ya wasamaria wema wakiongozwa na madereva bodaboda kuchangisha fedha zikapatikana Sh101,100. Mwili umesafirishwa kwenda Kijiji cha Pande, wilayani Kilwa.