Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Abood aivaa Zimamoto ajali ya moto Morogoro

Moto ukiteketeza mabanda ya kuuzia samani za ndani kwenye Mtaa ya Ngoto Manispaa ya Morogoro tukio lililotokea Machi 21, 2025 saa 2.30 usiku. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Mbunge wa Morogoro Mjini AbdulAziz Abood amesema hilo si tukio la kwanza kutokea jirani na ofisi za Zimamoto lakini wamekuwa wakichelewa kufika na kuna wakati wanakuja na maji kidogo.

Morogoro. Kufuatia ajali ya moto iliyoteketeza karakana na mabanda ya kuuzia samani za ndani katika Mtaa wa Ngoto mjini ya Morogoro, Mbunge wa jimbo hilo, Abdulaziz Abood amelitupia lawama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro kuwa utendaji kazi wake hauridhishi katika kukabiliana na majanga ya moto.

Abood ameyasema hayo baada ya kufika eneo la tukio na kusema hilo si tukio la kwanza kutokea jirani na Ofisi za Jeshi la Zimamoto, lakini waokoaji wamekuwa wakichelewa kufika na kuna wakati wanakuja na maji kidogo ambayo hayawezi kuzima moto.

“Bado sijafahamu changamoto hiyo inatokana na nini, kitengo chetu cha Zimamoto bado kiko chini, wamefika eneo la tukio kwa kuchelewa, wafanyabiashara hawa wamepata hasara na hata nyumba zilizopo jirani na mabanda haya zimeteketea kwa moto,” amesema Abood.

Mbunge huyo amesema kutokana na changamoto hiyo, amepanga kuwasilisha taarifa hiyo kwa viongozi wa Serikali ili kitengo hicho kifanyiwe maboresho.

“Tunachoshukuru kwenye tukio hili hakuna vifo wala madhara ya kibinadamu, zaidi ya hasara waliyoipata hawa ndugu zetu wafanyabiashara wa samani, tunaamini vyombo vinavyohusika vitaendelea kuchunguza chanzo cha moto huu,” amesema Abood.

 Ofisa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Daniel Myalla ametoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya wananchi na mbunge dhidi yao, akisema taarifa za moto huo zilichelewa kuwafikia ofisini.

“Sio kweli kwamba tumechelewa kufika eneo la tukio, na sio kweli kwamba tulikuja bila maji, isipokuwa taarifa zilikuja kwa kuchelewa na tulipofika eneo la tukio tulikuta tayari moto umeshika kasi na ulikuwa ni mkubwa,” amesema Myalla.

Ameongeza kuwa: “Tulikuja na gari lenye maji na tuliweza kuudhibiti moto lakini maji yalipoisha tulikwenda kuongeza maji na wakati huo tayari wenzetu wa Jeshi la Wananchi walifika na kuongeza nguvu.

Amesema walifanikiwa kuzima moto ambao ulikuwa unawaka kwenye vibanda 10 na nyumba moja iliyokuwa jirani na vibanda hivyo.”

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala amesema uchunguzi wa moto umeanza kufanywa na baada ya kupata taarifa ya uchunguzi huo, atatoa taarifa ya chanzo cha moto huo.

“Asubuhi hii ndio nimepokea taarifa kutoka kwa Jeshi la Zimamoto na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhusu tukio hili, nikiipitia nitatoa taarifa ya nini kimetokea na nini kinaendelea,” amesema Kilakala.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema kabla ya moto huokusababishan uharibifu huo, waliona moto ukiwaka kwenye sehemu ya nyaya za umeme, muda mfupi baadaye ukashika kwenye vibanda.

Vibanda vikivyoteketea ni vinavyotumika kuuzia samani za ndani kama vile vitanda, makabati, viti, milango, sofa na meza za chakula.