Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajasiriamali, wawekezaji wajipanga kukuza biashara Afrika

Mratibu wa Accelerate Africa Tanzania, Pendo Lema (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano wa Accelerate Africa 2024 utakaofanyika Arusha Novemba mwaka huu. Wengine kutoka kushoto ni Mratibu wa Maendeleo ya Vijana wa Accelerate Africa, Isaac Fivawo na Katibu Mtendaji Jabeen Shiraz.

Muktasari:

  •  Tanzania inakuwa mwenyeji wa mkutano wa Accelerate Africa 2024 kwa mara ya kwanza baada ya kufanyika kwa ufanisi nchini Rwanda na Afrika Kusini

Dar es Salaam. Wajasiriamali, wawekezaji na viongozi wa kibiashara zaidi ya 200 kutoka Afrika wamepanga kushirikiana kusukuma ukuaji wa biashara ndogondogo na za kati (SMEs) barani humo.

Wadau hao wa uchumi kutoka nchi 10 wanatarajiwa kushiriki mkutano wa Accelerate Africa 2024, jijini Arusha Novemba 28 na 29 mwaka huu kujadili masuala mbalimbali ya kibiashara.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya kufanyika kwa ufanisi  nchini Rwanda na Afrika Kusini. 

Akizungumza leo Jumatano Septemba 18 2024 kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Accelerate Africa Tanzania,  Pendo Lema amesema mkutano huo pia, unalenga kuonyesha mitazamo na utaalamu wa aina mbalimbali kutoka sekta za biashara, teknolojia na maendeleo.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kuwezesha Biashara NdogoNdogo na za Kati kwa Ukuaji Endelevu na Ubunifu Barani Afrika.”

"Dhamira hii inalenga nafasi ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kukuza ubunifu barani Afrika,” amesema Pendo.

Pia, amesema Accelerate Africa ni jumuiya ya washauri mabingwa wa fikira za kiuchumi barani Afrika na ni jukwaa lenye nguvu na ubunifu linalosaidia ukuaji na maendeleo ya biashara ndogondogo na za kati Afrika. 

Pendo amesema wajasiriamali watakaohudhuria mkutano huo wanatoka nchi za Botswana, Cameroon, Malawi, Ghana, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Tanzania na Zimbabwe, ambazo ni nchi wanachama zinazounda Accelerate Africa.

Akizungumzia sababu za Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo amesema, “Tanzania ilichaguliwa kuwa nchi mwenyeji kutokana na eneo lake la kimkakati katika Afrika Mashariki, uchumi wake unaokua kwa kasi na dhamira yake ya kusaidia biashara ndogo ndogo za kati na ubunifu.”

Wakati huohuo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imetangaza kushiriki katika mkutano huo unaolenga kuwezesha biashara ndogondogo na za kati na kuwa kichocheo kikubwa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi barani Afrika. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga amesema:  “Tunajivunia kushirikiana na mkutano wa Accelerate Africa Tanzania 2024, tunatambua umuhimu wa biashara ndogondogo za za kati na katika ubunifu, kutengeneza ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

“Kwa kushirikiana na waandaaji, tunalenga kuwapa wajasiriamali nyenzo, rasilimali na mitandao ambayo wanahitaji ili wafanikiwe hapa nchini na barani Afrika.”

Amesema kupitia ushiriki huo, taasisi hiyo itachochea kasi ya ukuaji wa sekta binafsi na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji ndani na nje ya Tanzania.

Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa na wazungumzaji  katika mkutano huo ni uongozi na ubunifu, kuwezesha biashara ndogondogo na za kati kwa ukuaji endelevu, ubunifu na upanuzi wa soko, upatikanaji wa fedha na uwekezaji, uwezeshaji wa wanawake na vijana pamoja na mageuzi ya kidijitali Afrika.

Zaidi ya hayo, amebainisha pia unalenga  kukuza ushirikiano na fursa za mtandao kwa biashara ndogondogo na za kati Afrika, kutoa maarifa ya upanuzi wa soko, uongozi na ubunifu.

Malengo mengine ni kuhimiza Watanzania waishio nje ya nchi kuwekeza katika biashara ndogondogo na za kati za Afrika, kukuza uchumi na kuwezesha jamii, kubadilishana fursa za biashara na mawazo ya ubunifu kwa wajasiriamali wa Afrika.