Ufaransa yatoa Sh96 bilioni kujenga mradi wa umeme Kakono

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini, Celine Robert, wakisaini mkataba wa Euro milioni 34.86 (Sh96.47 bilioni) kwa ajili ya mradi wa kufua umeme wa nguvu za maji wa Kakono, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Muktasari:

 Ujenzi wa mradi mpya wa umeme wa Kakono mkoani Kagera ni mwendelezo wa Serikali kuwa na vyanzo vipya vya kuzalisha nishati hiyo ili kuondokana na mgawo

Dodoma. Megawati 87.8 za umeme zinatarajiwa kuongezwa katika gridi ya Taifa baada ya Serikali kutia saini mkataba wa msaada wa Sh96.47 bilioni (Euro milioni 34.86) kwa ajili ya mradi wa kufua umeme wa nguvu ya maji wa Kakono, mkoani Kagera.

Utiaji saini umefanyika leo Jumanne, Aprili 9, 2024 kati ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ikiwa ni jitihada zinazofanyika za kuongeza vyanzo vipya vya uzalishaji wa nishati hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba amesema mradi huo unatarajiwa kuongeza idadi hiyo ya megawati utakapokamilika.

“Mtambo unaotarajiwa kujengwa wa kufua umeme wa Kakono upo Mto Kagera, takribani kilomita 90 Magharibi mwa Manispaa ya Bukoba, ambayo ni kona ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania,” amesema Dk Mwamba.

Amesema lengo la mradi ni kuongeza uzalishaji wa umeme nafuu wa nguvu za maji ili kukabiliana na upungufu katika gridi ya Taifa maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Dk Mwamba amesema ujenzi wa mtambo huo utakuwa mbadala wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ambayo hutumika kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kwenye gridi ya Taifa ili kupunguza mgawo. 

“Utekelezaji wa mradi huu unaendelea na utakamilika mwaka 2026 na kukabidhiwa kwa Serikali Desemba 2028,” amesema.

Amesema mradi unafadhiliwa na wafadhili watatu, Shirika la Maendeleo la Ufaransa lililotoa Sh304.37 bilioni (Euro milioni 110), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Sh413.95 bilioni (Dola za Marekani milioni 161.47), na Umoja wa Ulaya Sh96.47 bilioni (Euro milioni 34.86).

“Leo tumesaini mkataba wa mwisho wenye msaada kutoka Umoja wa Ulaya, utakaosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa,” amesema Dk Mwamba.

Amesema mradi huo mbali na kutoa huduma ya umeme kwa watumiaji, pia utatoa ajira.

“Inatarajiwa ajira 1,000 za muda zitapatikana wakati wa utekelezaji wa mradi na ajira 100 za kudumu wakati wa uendeshaji wa mradi. Ajira hizi zitachochea ukuaji wa uchumi wa watu wanaozunguka mradi na kuboresha maisha yao,” amesema Dk Mwamba.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini, Celine Robert, amesema mradi huo unaenda sambamba na malengo ya kimataifa kuhusu tabianchi na utasaidia Tanzania kupunguza kiwango cha kaboni katika sekta ya nishati.

‘‘Mradi huu unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya eneo hili linalokua kwa kasi, ambalo liko katikati mwa eneo la Maziwa Makuu, kukuza uchumi wa viwanda na kuchochea ukuaji si tu Tanzania bali hata katika nchi jirani,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amesema Wizara kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) watahakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema mradi utarahisisha upatikaji wa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Kagera na mingine ya jirani, utaongeza ajira, utapunguza gharama za umeme na kuongeza mapato ya Tanesco.

Wakati wa utuaji saini mkataba mradi wa umeme wa Malagarasi wa megawati 49.5 uliopo mkoani Kigoma, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema mradi huo ni jitihada za Serikali za kuongeza vyanzo vipya kukabiliana na upungufu wa umeme.

Hivi karibuni mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 umeanza kazi na kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba 9.

Dk Biteko alisema wizara haitabweteka na kuanza kazi kwa JNHPP, bali kasi ya utekelezaji wa miradi mingine mipya inaendelea ikiwemo miradi ya Rumakali wa megawati 222, Ruhudji megawati 358, na ya jotoardhi ya Ngozi na   Kiejo-Mbaka.

Mwingine ni mradi wa umeme jua wa Kishapu wa meghawati 150.

 “Lazima, tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka, mahitaji yameongezeka lakini vyanzo ni vilevile kwa miaka mingi, mfano Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1980, Kidatu mwaka 1975, Kihansi mwaka 2000, Pangani 1995, Hale 1968, Nyumba ya Mungu 1964 na mwaka 2019 baada ya gesi kuanza uzalishaji umeme mahitaji yalikuwa pungufu kuliko uzalishaji, lakini sasa ni makubwa kuliko vyanzo,” amesema.