‘Tutoe taarifa za vitendo vya ukatili’

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,Mwanaidi Ali Khamis,akizungumza na Kamati za MTAKUWWA II za wilayani Arumeru,vikundi vya malezi na wadau wengine wa masuala ya watoto
Muktasari:
- Ni wajibu wa kila mmoja kuanzia ngazi za familia kuchukua hatua na kutoa taarifa za matukio ya kikatili dhidi ya wanawake na watoto
Arusha. Ili kutokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, jamii imetakiwa kutoa taarifa za matukio hayo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 16,2025 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza wilayani Arumeru katika ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa programu za malezi mbadala pamoja na programu ya uwezeshaji wa uchumi inayotekelezwa na Shirika la SOS SOS Children's Villages Tanzania.
Akizungumza na kamati za Mpango Kazi wa Pili wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto(MTAKUWWA II 2024/25 hadi 2028/29 ) za wilayani humo pamoja na vikundi vya malezi, amesema ni muhimu kamati hizo kushirikiana kwa ukaribu na jamii.
Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuanzia ngazi za familia kuchukua hatua na kutoa taarifa za matukio ya kikatili dhidi ya wanawake na watoto ili hatua zichukuliwe na kukomesha vitendo hivyo.
“Pale panapotokea changamoto mtu amefanyiwa ukatili tushirikiane pamoja na mwathirika wa tukio kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa.
“Tunajua kuna undugu na jamaa miongoni mwa matukio hayo ila tukiendelea kuwaficha kwa sababu huyu ni mdogo wangu, ukatili hautaisha kwenye jamii, tuwe wawazi kwa vyombo vya ulinzi na usalama na wadau wengine ili tusiendeleze vitendo hivi,” amesema.
Naibu waziri huyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha vikundi 3,963 vya malezi chanya kwa lengo la kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii.
Mkurugenzi wa Shirika la SOS nchini, Asha Ali amewaomba viongozi wa dini katika madhehebu mbalimbali kuendelea kusisitiza jamii hasa wanaume juu ya malezi na matunzo katika familia.
“Malezi na matunzo kwa familia ni muhimu, viongozi wa dini tunaomba mkumbushe jamii hasa wanaume juu ya malezi kani tunaona familia zinapovunjika watoto wa mitaani na waishio katika mazingira magumu wanaongezeka, hii sio sawa.
“Tunayoyaona kwenye jamii kwa sasa ikiwamo kutokuwepo kwa maadili kwa baadhi ya vijana kunatokana na malezi mabovu, sasa tujitahidi kushirikiana kujenga jamii yenye malezi na maadili mema na sisi kama shirika tutaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanalelewa na kupata matunzo na haki za msingi,” amesema.
Mwenyekiti wa wazee wa mila wa Kabila la Wameru Elias Nanyaro, amesema kutokana na elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii wameshirikiana na wadau wengine kupunguza vitendo hivyo kwa wanawake na watoto.
“Tumekuja kugundua watoto wanakutana na changamoto sana, kwa sababu wananyanyasika katika jamii, wengine wanaozesha watoto katika umri mdogo na jamii inaona ni kitu cha kawaida, tulikubaliana kila ukoo kuhakikisha hakuna anayeruhusu vitendo hivyo kwenye jamii zao na tumeona mabadiliko makubwa,” amesema.