‘Tozo Daraja la Kigamboni zilizingatia maoni’

Muktasari:
Mhandisi Karrim Mattaka wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) amesema kuwa wao hawana mamlaka ya kupunguza au kuongeza ushuru wa kupita katika daraja hilo na kwamba mwenye mamlaka hiyo ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Wamiliki wa daladala zinazotumia Daraja la Nyerere Kigamboni jijini Dar es Salaam wanaodai tozo ni kubwa katika daraja hilo wameshauriwa kupeleka malalamiko yao Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili zipitiwe upya.
Mhandisi Karrim Mattaka wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) amesema kuwa wao hawana mamlaka ya kupunguza au kuongeza ushuru wa kupita katika daraja hilo na kwamba mwenye mamlaka hiyo ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Alipoulizwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho alisema uamuzi wa tozo kwa watumiaji wa daraja hilo ulifanywa kwa kuzingatia maoni na ushauri kutoka kada mbalimbali na kuwa endapo kutakuwa na haja ya kurejea upya tozo hizo watazihusisha kada hizo.
Viwango vya tozo vinaonyesha wenye baiskeli wanalipa Sh300, pikipiki Sh600, baiskeli za miguu mitatu (guta, mikokoteni, bajaji) Sh1,500, magari madogo Sh1,500, pick-up Sh2,000, mabasi madogo Sh3,000 na mabasi makubwa Sh7,000.
Pia, matrekta hutozwa Sh7,000, matrekta yenye tela Sh10,000, magari ya uzito kati ya tani mbili na saba Sh7,000, tani saba hadi 15 Sh10,000, tani 15 hadi 20 Sh15,000, tani 20 hadi 30 Sh20,000, na magari yenye uzito kuzidi hapo Sh30,000. Gharama hizo hulipwa kila chombo cha usafiri kinapopita.
Amin Mohamed anayeendesha moja ya mabasi sita yanayotoa huduma kupitia daraja hilo alisema: “Yaani kwa sisi wa daladala tunaweza kupita hapa zaidi ya mara 15 na kila tunapopita tunapaswa kulipia Sh7,000.”
Daraja hilo lililopo Kigamboni linalotajwa kuwa kubwa na la kihistoria kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, lilizinduliwa Aprili 19 na Rais John Magufuli katika sherehe zilizohudhuriwa na mamia ya wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali , akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.