Prime
Sintofahamu yagubika upanuzi wa barabara ya Kibaha–Chalinze

Muktasari:
- Ni miaka mitano sasa tangu viongozi wa Serikali watoe ahadi mbalimbali kuhusu ujenzi wa barabara ya Kibaha–Chalinze, mkoani Pwani hadi Morogoro, ahadi ambazo zimetolewa ndani na nje ya Bunge.
Dodoma. Sintofahamu imeibuka kuhusu upanuzi wa barabara kutoka Kibaha hadi Chalinze, mkoani Pwani, kisha Morogoro, inayolenga kupunguza msongamano wa magari, kutokana na mradi huo kutotekelezwa kwa muda mrefu.
Kwa zaidi ya miaka mitano sasa, utekelezaji wake umegubikwa na kauli za viongozi, jambo linalosababisha sintofahamu juu ya lini upanuzi huo utafanyika, licha ya changamoto zinazowakabili watumiaji wa ndani na nje ya nchi.
Mchakato wa maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam–Chalinze–Morogoro ulianza mwaka 2017, ambapo taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2015–2017 ilieleza kuwa mtaalamu mwelekezi alikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na hatua za kumpata mwekezaji/mbia zilikuwa zinaendelea.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Aprili 10, 2025, Katibu wa Chama cha Wasafirishaji kwa Njia ya Barabara (Tarwotu), Mussa Nsese amesema barabara hiyo kati ya Kibaha na Chalinze imekuwa kero kwa madereva.
Amesema changamoto nyingine ni upana mdogo wa barabara hiyo, ambao husababisha matatizo wakati madereva wanapotaka kuyapita magari mengine ama kukwepa maeneo yaliyoharibika.
“Haya yote yamekuwa yakisababisha foleni kubwa katika barabara hiyo, na wale wanaojaribu kuyakwepa mabonde yaliyo katika barabara hiyo wanaweza kukutana uso kwa uso na magari ya upande wa pili kwa sababu hakuna hata pa kukwepea,” amesema.
Amesema Serikali ingeongeza upana wa barabara kutoka pale ilipoishia eneo la Mbezi hadi Chalinze, kwa kuwa ndio maeneo yenye changamoto kubwa ya foleni.
Nsese ameshauri Serikali kutengeneza hata barabara ya molamu ikiwa fedha kwa ajili ya kutengeneza kwa kiwango cha lami hazipo.
Amesema ubovu wa barabara hiyo unaweza kuwa chanzo cha ajali, kutokana na vibonde vinavyowalazimu madereva kuvikwepa.
Mmoja wa madereva wanaoitumia barabara hiyo mara kwa mara, Julius Edward amesema mpango wa kujenga barabara ya mwendokasi (express) kwa utaratibu wa kulipia ungesaidia kuondoa changamoto hiyo kwa wale wenye uwezo wa kulipia kuitumia.
“Ni miaka sasa Serikali imesema itajenga barabara hiyo, lakini hatujui uamuzi huu umefikia wapi? Lakini ikijengwa itasaidia kuondoa changamoto ya foleni katika kipande hiki cha Kibaha hadi Chalinze,” amesema Edward.
Jana Jumatano, Aprili 9, 2025, katika kipindi cha maswali na majibu, liliibuka swali kuhusu barabara hiyo, na mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka, alihoji ni lini Serikali itaendeleza upanuzi wa barabara ya kipande cha Kibaha–Chalinze kuwa njia nane ili kuondoa msongamano wa magari Kibaha.
Akijibu, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alisema Serikali haitaendeleza upanuzi wa barabara sehemu ya Kibaha hadi Chalinze kuwa njia nane, na badala yake itajenga barabara ya mwendokasi (Express Way) kutoka Kibaha–Chalinze–Morogoro (km 159) kwa utaratibu wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Kasekenya alisema zabuni ya kumpata mwekezaji kwa sehemu ya Kibaha hadi Chalinze iko katika hatua za mwisho za majadiliano.
“Ujenzi unatarajiwa kuanza baada ya majadiliano kukamilika na mkataba (Concession Agreement) kusainiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa barabara hiyo inafanana na ujenzi wa daraja la Kigamboni, ambapo watu waliona kuna fursa.
Kauli za viongozi
Novemba 16, 2022, Mkurugenzi wa Manunuzi na Mikataba wa Makao Makuu ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Kingdom Mbangula alisema mkandarasi amepatikana, atakayejenga kwa fedha zake, huku malipo atakayopata yatatokana na matumizi ya barabara hiyo.
“Tunatarajia kuanza mwakani (2023) Aprili au Mei mkandarasi atajenga barabara hii kwa fedha zake, halafu magari yanayopitia atachukua hela ili arudishe fedha alizotumia kujenga mradi huo,” alisema Mbangula.
Lakini Desemba 9, 2022, Kasekenya, alisema barabara ya kutoka Kibaha, Chalinze hadi Morogoro wanatafuta wawekezaji wengine watakaojenga kwa haraka, ambapo watumiaji watalipia tozo.
“Hadi sasa wakandarasi wenye nia wameshakwenda kuona na wako wengi. Tulikuwa na barabara nane ambazo tulitangaza, lakini kwenye huu mfumo ni hii moja. Wakandarasi zaidi ya 20 waliomba wajenge hiyo barabara kwa sababu ni fursa,” alisema.
Alisema watu hawatalazimishwa kutumia barabara hiyo ya haraka, bali watachagua wanataka kupita wapi.
Desemba 29, 2023, Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, David Kafulila, alisema mchakato wa ujenzi wa barabara ya kulipia kutoka Kibaha hadi Morogoro uko katika hatua za mwisho na kufikia Februari 2024, mkandarasi atapatikana.
Katika mahojiano hayo, Kafulila alisema tayari kampuni kadhaa zimeonyesha nia ya kujenga barabara hiyo ya kulipia kutoka Kibaha hadi Morogoro yenye urefu wa kilomita 130, kwa lengo la kupunguza msongamano.
Alisema China ni moja ya nchi zilizotoa kampuni nyingi zilizoonyesha nia ya kujenga kipande cha Kibaha kwenda Chalinze, Chalinze kwenda Morogoro, na baadaye kutoka Morogoro kwenda Dodoma.
“Mpango wa Serikali ni kuunganisha haya majiji mawili -- Dar es Salaam na Dodoma kwa barabara za Express Way (barabara za haraka), barabara ambazo ni mbili za kwenda na mbili za kurudi.
“Kuna kampuni tisa ziliomba kwa ajili ya kipande cha Kibaha–Chalinze chenye urefu wa kilomita 78.9. Kampuni hizo zilifanyiwa mchujo zikabakia tano; kati ya hizo, nne ni za China. Unaweza ukaona namna China inavyoshiriki kwenye ushindani huu wa ubia,” alisema Kafulila.
Aidha, akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2024/25, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa, alisema moja ya vipaumbele vya sekta ya ujenzi ni pamoja na kuanza ujenzi wa barabara ya Express Way kutoka Kibaha–Chalinze–Morogoro kwa mfumo wa PPP.