Mitambo miwili Bwawa la Nyerere kuwashwa kwa pamoja

Muktasari:

 Mitambo hiyo imekamilika na kinachofanyika sasa ni kumalizia vitu vidogo vidogo

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema mtambo namba nane na namba saba kwenye Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere itawashwa kwa pamoja hivi karibuni.

Amesema mkakati wa awali ilikuwa ni kuwashwa kwa mtambo namba nane mwezi Machi 2024, baada ya ule namba tisa kuwashwa Februari 25, 2024 lakini tayari na mtambo namba saba nao umekamilika hivyo yote itawashwa kwa pamoja.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 14, 2024 Mramba amesema mitambo hiyo imekamilika na kinachofanyika sasa ni kumalizia vitu vidogo vidogo na mkakati uliopo ni yote kuwashwa kwa pamoja mwishoni mwa mwezi huu.

Amesema mtambo namba 8 na 7 itaingiza kwenye gridi ya Taifa megawati 470, hivyo nchi kuwa na ziada kubwa ya umeme.

"Tutakuwa na ziada kubwa ya umeme na hata mitambo mingine (namba 6-1) itakapokamilika, umeme wake utakuwa ni ziada na hapo ndipo tutafikiria kuuza nje ya nchi," amesema Mramba.

Kuhusu mgao wa umeme nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo-Hanga amesema umekwisha na inapotokea umeme umekatika ni changamato nyingine na si sababu ya mgao.

Mgao wa umeme ulianza Septemba 2023, Februari mwaka huu mtambo namba tisa kwenye bwawa la Nyerere ulipowashwa na kuingiza megawati 235 kwenye gridi ya Taifa ilielezwa kupunguza makali ya mgao kwa kiwango kikubwa.

Leo Jumapili, Nyamo-Hanga amesisitiza mgao nchini kumalizika na nchi inazalisha umeme wa kutosha.

"Hivi sasa hatuna mgao, tunazalisha umeme wa kutosha kwa mahitaji tuliyonayo," amesema Nyamo-Hanga na kubainisha kwamba, ikitokea eneo umeme umekatika ni changamoto nyinginezo za kiufundi na si mgao.

"Hata binadamu anayetembea siku nyingine atajisikia vibaya na kwenda hospitali, hata kwenye umeme ikitokea sehemu umekatia kwa kipindi hiki si kwa sababu ya mgao ni changamoto nyingine," amesema Nyamo-Hanga.

Amesema, mahitaji ya umeme Tanzania yameongezeka hadi kufikia megawati 1600 na nchi inazalisha zaidi ya mahitaji.

"Hata kabla ya Bwawa la Nyerere na mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo na vinu tulivyonavyo vilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 1914, hivyo vilikuwa vinazidi mahitaji.

Amesema tatizo lililosababisha mgao ni pale inatokea kinu fulani kutozalisha kwa uwezo wake au wakati wa kiangazi maji kuwa ni kidogo au kinu ni kibovu kinasubiri matengenezo.

"Lakini kwa rasilimali tulizonazo wala hatukutakiwa kuwa na mgao," amesema Nyamo-Hanga.

Amesema watakapowasha mtambo namba nane na namba saba kwenye, ziada itakayopatikana mbali na kuuza nje, lakini matumizi ya ndani pia yanaongezeka hivyo na matumizi ya nchini yataongezeka.

"Hiyo ziada tunategemea pia itabebwa na shughuli mpya za kiuchumia ambazo hazijaanza kutumia umeme, kuna viwanda vingi vinajengawa, wachimbaji madini wanaongezeka.

"Hivyo ziada tutakayokuwa nayo, mbali na kuuza nje pia itamezwa na ukuaji wa matumizi ya umeme ndani ya nchi," amehitimisha.