Michoro ya kale Kondoa kuvuta watalii

Muktasari:

  • Vivutio vingine vya Tanzania vilivyopo Unesco ni maeneo ya urithi ya Hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Wanyamapori la Selous, Mji Mkongwe Zanzibar, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara

Dodoma. Maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia kwa Afrika kesho Mei 5, 2024 kuwaleta watalii wa ndani na  nje kwenye michoro ya mapangoni iliyopo Kijiji cha Kolo, Kondoa Irangi mkoani hapa.

Michoro hiyo ambayo ni Urithi wa Utamaduni na Malikale imetangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kuwa moja ya Urithi wa Dunia.

Meneja wa uhifadhi wa Kituo cha Michoro ya Miambanai ya Kondoa, Zuberi Mabie amesema jana Ijumaa, Mei 3, 2024 wilayani Kondoa kuwa michoro ya Kondoa ni miongoni mwa maeneo saba ya urithi ya Tanzania yaliyorodheshwa Unesco.

Michoro ya Kondoa iliwekwa kuwa vivutio vya Urithi wa Utamaduni Duniani chini ya Unesco tangu mwaka 2006.

Vivutio vingine vya Tanzania vilivyopo Unesco ni maeneo ya urithi ya Hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Wanyamapori la Selous, Mji Mkongwe Zanzibar, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Mabie amesema michoro hiyo baada ya kuwekwa Unesco imekuwa chanzo cha mapato, sehemu ya mafunzo kwa vitendo na pia kuonesha historia ya nchi.

Mabie amesema kwa mwaka huu Kondoa ni mwenyeji wa maadhimisho hayo yanayofanyika Mei 5, ya kila mwaka na mara ya kwanza yalianza mwaka 2021 kwenye mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe kisiwani Zanzibar.

Amesema mwaka juzi yalifanyika kwenye magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na mwaka jana yalifanyika katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro wilayani Moshi na kwa mwaka huu ni zamu ya Kondoa.

Pia, Mabie amesema mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa maazimisho hayo ni mwitiko wa umma.

“Maana changamoto kubwa tuliyokuwa tunakabiliana nayo sisi kama wahifadhi ni kwa namna umma utakavyoshiriki katika shughuli hizi za uhifadhi na wao kuwa sehemu ya uhifadhi.

“Kupitia maadhimisho haya tumejenga uelewa kwa umma kwamba sasa hivi Watanzania wanajua walau shughuli za uhifadhi na umuhimu wa uhifadhi katika maeneo haya kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

“Lakini, uungwaji mkono wa viongozi wa kisiasa ambao wako kwenye ngazi za maamuzi, sababu tuligundua moja ya matatizo ambayo nchi zetu nyingi za Afrika zinakumbana nayo ni pamoja na shughuli hizi kutoeleweka kwa viongozi wetu juu ya masuala ya uhifadhi, lakini kupitia madhimisho haya nao wamekuwa wakishiriki na kusaidia pale ambapo inahitajika kwa ajili ya kufanya maamuzi yanayosaidia uhifadhi kuwa endelevu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi na uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar, Ali Said Bakar mesema vituo vyote vya uhifadhi Tanzania vinakutana sehemu moja Kondoa.

Amesema moja ya vitu muhimu kwa utalii ni tabia za watu na hali ya mji; na kwa Kondoa amesema ni sehemu ambayo iko tayari kupokea watalii kwa kuwa watu wake ni wakarimu na kuna hoteli nzuri.

“Tumefika hapa kwa sababu ya Jamhuri ya Muungano, kama si Muungano tusigefika hapa, kwa hiyo tunaendelea kushirikiana kwa njia zote,” amesema Bakar.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dk Khamis Mkanachi amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi wa Kondoa na kwamba tayari wamefanya maandalizi ya kuonesha vitu vya asiali ikiwamo vyakula.

Amewahakikishia wageni kwamba wilaya hiyo imejiandaa kuufanya mji huo wa kitalii kwa kuwa wakazi wake wa mjini ni wafanyabiashara.

Naye mamalishe, Zainabu Dosa amesema michoro ya Kondoa kwa kuwekwa Unesco kumeongeza mapato kwenye biashara yake.

Amesema kwa kawaida kwa siku alikuwa akiuza kuku watano, lakini uwepo wa wageni wanaokwenda kwenye kichoro hiyo, kwa siku amekuwa akiuza kuku waliopikwa hadi 15.

Meneja wa Kituo cha Michoro ya  Miambani Kondoa, Ziberi Mabie (katikati) akizungumza na waandishi wa habari. Kulia ni Mhifadhi wa kituo hicho, Amon Mgimwa na kishoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar, Ali Said Bakar.


Michoro ya Kondoa

Michoro ya Kondoa ni kundi la michoro ya miambani iliyopo kwenye vilima vinavyotazama mtelemko wa Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki.

Michoro hiyo inaonyesha picha za watu, wanyama na uwindaji. Hii inatazamwa kutoa ushuhuda wa namna ya maisha ya wachoraji waliokuwa wawindaji.

Aina nyingine za michoro zinaonyesha milima, duara au alama za kimsingi.

Wataalamu wengine huamini ya kwamba picha hizi zilichorwa tangu miaka 1,500 iliyopita na jamii za wawindaji waliokalia eneo hili, lakini wengine husema inaewezekana ni za zamani zaidi, labda hata miaka 10,000.

Michoro hii imegawanyika kwenye makundi mawili michoro mekundu na njano na yenye rangi nyeupe na nyeusi.

Michoro yenye rangi nyekundu ndio yenye umri mrefu zaidi ikikadiriwa kuchorwa miaka takribani 5,000 iliyopita.

Ilichorwa kwa kutumia mchanganyiko wa mwamba mlaini unaojulikana kama oka ambao husagwa na unga wake kuchanganywa na kimiminika cha Mti wa Mkuyu na mafuta ya mnyama jamii ya swala  kisha kutumika kuchora kwa kutumia mwiba wa nungunungu kama brashi.

Michoro yenye rangi nyeupe husadikiwa kuwa na umri wa miaka takribani 3,000 na imechorwa kwa kutumia mchanganyiko wa majivu kwa rangi nyeupe, mkaa kwa nyeusi, kinyesi cha ndege na mafuta ya mnyama jamii ya swala na kuchorwa kwa vidole.

Jamii inayohusishwa na michoro hii ya awali ni ile ya Wasandawe ikiwa ni njia ya mawasiliano, simulizi pamoja na kutunza historia kwa kipindi hicho.

Michoro inafanana na michoro kwenye mwamba inayopatikana katika Afrika ya Kusini na katika milima ya Sahara. 

Kuna dalili ya kwamba sehemu ilichorwa na mababu wa Wasandawe na Wahadzabe wa leo, ambao walihifadhi desturi ya kuchora mwambani hadi miaka ya karibuni na walikuwa wawindaji.