Prime
Lissu ahoji mashahidi wake kuwekwa kando
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameibuka na mapya akiilalamikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pamoja na mambo mengine kwa kutokuorodhesha mashahidi anaokusudia kuwaita mahakamani katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Miongoni mwa mashahidi aliodai aliwataja lakini hawakuorodheshwa ni Samia Suluhu Hassan, Dk Philip Mpango na Kassim Majaliwa.
Lissu ameibua madai hayo leo Jumanne, Septemba 9, 2025, Mahakama Kuu Dar es Salaam, wakati wa usikilizwaji wa pingamizi lake kuhusu Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo.
Vilevile, Lissu ameibua hoja ya kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Kisutu akidai uliendeshwa kinyume cha matakwa ya sheria.
Amedai kuwapo kumbukumbu mbili za mwenendo wa kesi kutoka Mahakama ya Kisutu, kwamba aliopelekewa gerezani wenye kurasa 16, wakati aliopewa na Mahakama Kuu ukiwa na kurasa 101.
Lissu amedai kasoro za kisheria zimeathiri mwenendo wa uhamishaji wa kesi kutoka mahakama hiyo ya chini na kuifanya kuwa batili, jambo ambalo linaifanya Mahakama Kuu isiwe na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Ameiomba Mahakama ifute mwenendo huo na iamuru leo Septemba 9, asirudishwe mahabusu katika Gereza la Ukonga anakoshikiliwa kutokana na kukabiliwa na shtaka lisilodhaminika, bali akalale nyumbani kwake.
Jamhuri kupitia jopo la mawakili likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga limedai madai ya Lissu likidai hayana mashiko.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno anayodaiwa kuyatamka kuhusu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya taratibu za awali, kabla ya kesi kuhamishiwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza.
Anadaiwa akiwa raia wa Tanzania, alishawishi umma kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Agosti 18, 2025 Mahakama ya Kisutu baada ya kukamilisha jukumu lake iliihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.
Kesi ilipangwa kusikilizwa na majaji watatu, jopo likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, Majaji wengine ni James Karayemaha, kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde, kutoka Mahakama Kuu Bukoba.
Lissu aliweka pingamizi akipinga mahakama kuendelea na usikilizaji akidai ni batili kutokana na kasoro za kisheria katika hati ya mashtaka, pia akidai haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kutokana na pingamizi hilo mahamama ilisimamisha usikilizwaji wa shauri hilo ili kushughulikia kwanza pingamizi la Lissu aliyetoa hoja na kuzihitimisha leo Septemba 9.
Lissu akitoa hoja kuhusu mamlaka ya mahakama, amedai mashauri yanayofunguliwa mahakama za chini kwa hatua za awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, yana utaratibu wake wa kisheria.
Amedai katika kesi dhidi yake utaratibu huo haukufuatwa; moja ikiwa ni pamoja na kuwapo nakala mbili tofauti za kumbukumbu za mwenendo wa kesi katika mahakama ya chini, mmoja aliopelekewa gerezani kutoka Mahakama ya Kisutu, alioupa jina la kumbukumbu za Ukonga na alizopewa jana Septemba 8 na Mahakama Kuu.
Akizungumzia tofauti hizo amedai kumbukumbu za Ukonga zina kurasa 16 lakini ya Mahakama Kuu ziko 101.
Pili, amedai kumbukumbu za Ukonga hazina alama ya utambuzi wa uhalisia wa nyaraka (scanning batch) chini kulia lakini ya Mahakama Kuu inayo kila ukurasa.
Tatu, kumbukumbu za Ukonga zinaanzia Agosti 18, 2025 na kuishia Agosti 18, 2025, yaani ni ya siku hiyohiyo, lakini ya Mahakama Kuu ilianza Aprili 10, 2025, siku aliyosomewa shtaka mpaka Agosti 18, wakati wa kuhamisha shauri hilo.
Nne, amedai ukurasa wa 15 wa kumbukumbu za Ukonga na ukurasa wa 100 wa kumbukumbu za Mahakama Kuu kuna orodha ya mashahidi wa Jamhuri lakini hakuna wa kwake licha ya kwamba aliwataja.
"Si kwamba hawakuwapo bali walikataliwa mbele ya mahakama kwamba ‘sitaandika hayo majina utayataja Mahakama Kuu’, nilishaanza kuwataja. Wa kwanza, Samia Suluhu Hassan wa pili, Phillip Mpango na wa tatu Kassim Majaliwa. Hakimu akakataa kuwa siwaandiki," amesema Lissu na kuongeza:
"Hizo zote ni tofauti katika nyaraka hizi ambazo zote zimetoka kwenye mahakama moja, sasa ipi ya kuchukua ipi ni halisi na ipi ni ya ku-fabricate (kughushi) na kwa nini kuna tofauti hizi.”
Amedai kesi hiyo iliahirishwa mara 10 bila sababu za msingi kama sheria inavyoelekeza ambazo zilitakiwa kuonyeshwa kwenye mwenendo na mahakama ilitoa sababu mara tatu.
Lissu amedai Mahakama ya Kisutu ilibadilisha uamuzi na amri za Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi kwa kuzuia mwenendo wa kesi hiyo kurushwa mubashara mtandaoni siku ya mwenendo wa kuhamisha kesi, amri aliyodai haikuwapo kwenye uamuzi wa Mahakama Kuu.
Amedai Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi zilitungwa katikati ya keshi kwa ajili yake na kwamba, hata maombi ya Jamhuri kuwalinda mashahidi hayakuwa na nia hiyo, kwani hawakutekeleza amri ya Mahakama.
Amedai mashahidi raia 11 wote walioombewa ulinzi licha ya kutokuwa na majina lakini kuna taarifa zao zinazowatambulisha kama namba za simu, mahali wanakofanya kazi, makazi yao na hata za familia zao.
Pia amesema sheria inasema aalipaswa kushtakiwa mahali alipokamatiwa ambapo ni Mbinga Mkoa wa Ruvuma, lakini akasafirishwa na kushtakiwa Kisutu.
Lissu amedai Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marejeo ya Mwaka 2023, vifungu vinavyohusu utaratibu wa mwenendo wa kuhamisha kesi, vinaelekeza mshtakiwa kupewa kumbukumbu na nyaraka zinazoambatana nazo, kama hayo ya mashahidi, mwenendo wa kesi na uamuzi.
Amedai kuna nyaraka zilizotajwa hakupewa akisisitiza kasoro hizo zinafanya mwenendo huo kuwa batili.
"Kwa hiyo ombi langu ni kwamba, hakukuwa na ‘committal’ na futilieni hii na mtoe amri leo baada ya siku 130 leo nilale nyumbani kwangu. Naombeni mtoe amri hiyo leo nisirudi gerezani,” ameomba Lissu.
Majibu ya Jamhuri
Akijibu hoja Wakili Katuga amedai pingamizi la Lissu halina mashiko na akaomba mahakama ilitupilie mbali.
Kuhusu Samia, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake kuwa miongoni mwa mashahidi wa Lissu, Katuga amedai ana kinga ya kutokuwa shahidi kwa mujibu wa Sheria ya Masuala ya urais kifungu cha 9.
Amedai baada ya kutajwa mashahidi wa asili hiyo, ndiyo maana Mahakama ya Kisutu haikuwaorodhesha.
Dk Mpango ni Makamu wa Rais na Majaliwa ni Waziri Mkuu.
Katuga amedai mahakama ilimwelekeza kuwa atawataja mashahidi wake Mahakama Kuu na hakuwataja wengine wisio na kinga kama hiyo.
Kuhusu Lissu kutokushtakiwa alikokamatwa Mbinga, mkoani Ruvuma, Katuga amedai ameshtakiwa mahali alikofanyia kosa japokuwa alikamatwa Mbinga lakini kosa alitenda Dar es Salaam.
Kuhusu kumbukumbu za mwenendo wa mahakama amedai wao ndio waliieleza mahamama baada ya kubaini alichokuwa akikirejea hakikuwa kamili, ndiyo maana mahamama ikampatia mwenendo huo.
Amedai mwenendo aliopewa kutoka Mahakama ya Kisutu ulihusu mwenendo wa siku ya kuhamisha kesi.
Kuhusu hoja ya kuahirishwa kesi, amedai iliahirishwa kwa mujibu wa sheria kwa sababu zilizotokana na mshtakiwa mwenyewe, akitoa mfano wa kugoma kufika mahakamani, upelelezi kutokamilika na sababu za kimahakama.
Amedai mwenendo ulifanyika kwa mujibu wa sheria, akijoji kama analalamikia kuahirisha basi ina maana anataka mwenendo wote ufutwe ili arudishwe Kisutu, iahirishwe kama anavyotaka.
Kesi hiyo inaendelea kesho Septemba 10, kwa Jamhuri kuendelea kujibu hoja za Lissu.