'Hausigeli' nusura atoroshe mtoto kulipa kisasi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na mwandishi wa Mwananchi leo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Taarifa ya mtoto huyo ilisambaa kuanzia jana Jumatano Februari Mosi mwaka huu katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha binti huyo akihojiwa na mwanamke ambapo alinukuliwa akijibu kuwa kichanga hicho ambacho ni cha mwajiri wake .

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limeanza uchunguzi wa tukio la mtoto ambaye jina lake limehifadhiwa (10) anayedaiwa kukamatwa na wasamaria wema katika stendi ya mabasi ya Nyegezi jijini Mwanza katika harakati za kutoroka na mtoto wa mwajiri wake kwenda mkoani Mbeya.

Taarifa ya mtoto huyo ilisambaa kuanzia jana Jumatano Februari Mosi mwaka huu katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha binti huyo akihojiwa na mwanamke ambapo alinukuriwa akijibu kuwa kichanga hicho ambacho ni cha mwajiri wake.

Akizungumza leo na Mwananchi Digital Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema katika mahojiano binti huyo alidai kusafirishwa kutoka kwa wazazi wake mkoani Mbeya na mwalimu wa Shule ya Msingi Ilendeja iliyoko Kisesa wilayani Magu mkoani hapa kwa lengo kuja kumsaidia kazi huku kukiwa na ahadi ya kumsomesha jambo ambalo halikufanyika.

"Februari Mosi mwaka huu aliamua kutoroka na mtoto huyo kwa lengo la kwenda Mbeya kwa sababu alikuwa amechoka kukaa na yule mwalimu ambaye anamtuhumu kwamba alikuwa akimfanyia vitendo vya ukatili kwa kumchapa mara kwa mara," amesema Mutafungwa

Mutafungwa amesema jeshi hilo pia lilikutana na mwalimu huyo, Diana Mwaihoji ambaye alikiri kuwa kichanga hicho ni chake huku akikiri kuwa binti huyo alikuwa hausigeli wake ambaye alimtoa mkoani Mbeya kwa ajili ya kumsaidia kazi za ndani.

"Tunashirikiana na wenzetu (Polisi) wa mkoa wa Mbeya ili kufika katika familia ya binti huyu kufahamu ilikuwaje wakamruhusu binti huyo kuja kufanya kazi mkoani Mwanza ilihali ni mwanafunzi,"

"Baada ya kumaliza mahojiano na mwalimu huyo ambaye alikiri kuishi na binti huyo kama mfanyakazi wake, tulimkabidhi mtoto wake lakini tunaendelea na upelelezi kwa hatua zaidi za kisheria," amesema Mutafungwa.