Bunge linavyotakiwa kuifanyia kazi kauli ya ‘Tanzania ni tajiri’

Muktasari:
Bunge la 11 ambalo Spika Job Ndugai aliwahi kujinasibu kuwa ni Bunge lenye wasomi wengi tangu uhuru wa Taifa hili liliweka historia kwa kumsaidia Rais Magufuli lilipounda kamati na kufukua uozo kwenye madini ya almasi.
“Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.” Ni kauli ya Rais John Magufuli kwa wabunge wa Bunge la 12.
“Nchi yetu ni tajiri ila tulitaka kuaminishwa na watu waliotaka kututumia sisi kama masikini ..nimeitaja hii baadhi ya miradi saa nyingine najiuliza hivi tumeweza maana yake kila palipo na nia na Mungu yupo ..ndugu zangu Watanzania Mungu yupo pamoja na sisi .. Mimi siwezi kusimama mbele ya watu kusema haya ni kwa sababu yangu.
“Mimi ni dereva tu, lakini pia najiuliza ikiwa siku moja Mungu atanichukua hawa wanaokuja watakuja kuyamaliza kweli kwa sababu panahitaji moyo ujitoe sadaka unafanya hivi huku unatukanwa , lakini inabidi ufanye kwa sababu unafanya kwa ajili ya Watanzania namshukuru Mungu na Watanzania kwa kuniombea na kunipa moyo,” ni kauli ya Rais Magufuli kuhusiana na utajiri wa Taifa la Tanzania.
Kauli hii ya Rais Magufuli haiwezi kufanikiwa kama wabunge wa Bunge la Tanzania hawatakuwa na uzalendo, kutoa ushirikiano kwa Serikali na kuacha ukasuku, ububu na mzaha (komedi) katika kuzungumzia masilahi ya Taifa.
Bunge la 11 ambalo Spika Job Ndugai aliwahi kujinasibu kuwa ni Bunge lenye wasomi wengi tangu uhuru wa Taifa hili liliweka historia kwa kumsaidia Rais Magufuli lilipounda kamati na kufukua uozo kwenye madini ya almasi.
Usomi wa wabunge ulioelezwa na Spika Ndugai Septemba 14, 2018 ni wabunge maprofesa walikuwa saba na wote kutoka CCM, wabunge wenye Shahada ya uzamivu (PhD) walikuwa 29 huku 27 wakitoka CCM na waliosalia mmoja alitoka CUF na mwingine Chadema. Bunge hilo la 11 mbunge mwenye umri mdogo (kwa mwaka 2018) alikuwa na miaka 27 na mwenye umri mkubwa alikuwa na miaka 75, huku wabunge wenye umri wa miaka 40 na kuendelea wakiwa asilimia 80.
Japo takwimu sahihi hazijajulikana kuhusu wasomi wa Bunge 12 lenye wabunge wapya 206 kati ya wabunge 356 walioapishwa, nalo linaonekana lina wasomi wengi zaidi hivyo ni matarajio ya Serikali litafanya kazi mara tatu zaidi ya Bunge la 11 ambalo liliunda kamati ya kuchunguza makinikia ya almasi na kubaini madudu mengi. Mbali na kuunda kamati ya kuchunguza makinikia ya almasi, pia Bunge la 11 kwa mujibu wa Rais Magufuli limemsaidia kudhibiti sekta ya madini kwa kupitisha miswada ya sheria iliyopelekwa na Serikali kwa lengo la kulinda utajiri wa Watanzania.
Akiwahutubiwa wabunge wa Bunge la 12, Rais Magufuli alilipongeza Bunge la 11 kwa kuchangia mafanikio ya sekta madini kwa kupitisha miswada ya sheria iliyopelekwa na Serikali kwa ajili ya kuifanya sekta hiyo inufaishe Watanzania. “Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge la 11 kwa kutoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa mafanikio haya.
“Nina imani kuwa Bunge hili la 12 litafuata nyayo za Bunge la 11. Na katika hili, napenda niliarifu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa madini yetu, (kama tulivyofanya kwa kujenga ukuta Mirerani) kwa kuimarisha Sheria zetu ili madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato,” alisema Rais Magufuli.
Watanzania kuwa mabilionea
Matumaini ya Serikali ya Rais Magufuli ya kuwafanya Watanzania kuwa mabilionea au kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi wafadhili, itategemea na utendaji wa wabunge katika kufanikisha matarajio ya Serikali.
Spika Ndugai aliwaeleza wabunge wasiwe mabubu wala kujipendekeza na kwamba kazi iliyo mbele yao siyo nyepesi kwa kuwa bajeti ya Serikali, mipango ya maendeleo, utungaji wa sheria, marekebisho ya sheria na ufutaji wa sheria vyote vitapita bungeni na wabunge ndiyo watakuwa na kazi kupitisha kwa weledi na siyo bora liende.
Bunge la 12 linatakiwa liende mbele zaidi kwakuwa mipango ya Serikali ni mingi na hasa katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo ina kurasa 303 zenye ahadi nyingi ikilinganishwa na ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 ambayo ilikuwa na kurasa zaidi ya 200.
Katika kuonyesha mafanikio ya Bunge la 11, Rais Magufuli aliwaeleza wabunge wa Bunge la 12 kwamba kwenye miaka mitano iliyopita Serikali imepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini.
“Mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 527 mwaka 2019/2020. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019.
“Zaidi ya hapo, kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7,” alisema Rais Magufuli.
Hata hiyo, Rais Magufuli aliwaeleza wabunge kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel na copper.
“Tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana,” alisema Rais Magufuli.
Kuonyesha kwamba Tanzania imekwenda kwa kasi katika maendeleo, Julai, 2020 Benki ya Dunia iliiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati.
Hatua hii imejiri miaka mitano kabla ya ruwaza ya maendeleo ya taifa hilo ambapo ilikuwa imelenga kuafikia kiwango hicho kufikia 2025.
Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, Deus Kibamba aliwahi kunukuliwa kuhusu sababu za Tanzania kuingia uchumi wa kati kwamba ni kutokana na uongozi uliopo kudhibiti matumizi ya fedha na kukabiliana na ufujaji wa fedha ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na Serikali kufikia malengo hayo yaliyotarajiwa mwaka 2025.
Wabunge wa Bunge la 12, kama walivyoelezwa na Spika Ndugai kwamba kazi iliyo mbele yao siyo nyepesi na matarajio ya Serikali ni makubwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo. Spika Ndugai wakati akipokea ripoti ya makinikia ya almasi aliahidi Bunge kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba juhudi, uthubutu na uzalendo aliouonesha Rais Magufuli katika kulinda rasilimali za madini haupotei bure.
Alieleza kuwa baadhi ya matatizo kwenye sekta ya yamekuwa yakijirudia ikiwemo mikataba mibovu ya uchimbaji madini, utendaji mbovu wa Bodi na mifumo mibovu ya kitaasisi zinazosimamia uchimbaji wa Madini Pia, alisema Bunge la 11 katika kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake lilipitisha miswada 60.
“Miswada iliyopitishwa na Bunge la 11 ni 60, yote imepata kibali halali cha Rais kwa hiyo sheria heria halali,” alisema .