Askofu Kasala atoa kauli aliyenajisi kanisa
Geita. Maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki na wa madhehebu mengine kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Geita, wameshiriki Ibada maalumu ya kutakatifuza Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita.
Pia, maaskofu 19, mapadri zaidi ya 50, watawa kutoka ndani na nje ya Jimbo hilo walishiriki ibada hiyo iliyoongozwa na aliyewahi kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Ibada hiyo ilifanyika baada ya kijana mmoja kuvamia kanisani hapo usiku wa kuamkia Februari 26 mwaka huu na kufanya uharibifu wa mali katika eneo la Altare, ikiwemo kumwaga ekaristi.
Kijana huyo anadaiwa kuingia kanisani kwa kuvunja kioo cha lango kuu na kuharibu mimbari, kuvunja kiti cha kiaskofu, misalaba, sanamu za kiimani ikiwemo misalaba na vyombo vya kuhifadhia maji ya baraka ambayo pia aliyamwaga.
Tukio hilo lilitafasiriwa na Kanisa hilo kuwa ni unajisi kwa utakatifu wa jengo hilo la kanisa na vifaa mbalimbali vya ibada takatifu na ni kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala alichukua uamuzi wa kulifunga kwa siku 20 kuanzia Februari 27 mwaka huu na kuingia kwenye adhimisho la toba ya malipizi, kusali, kutubu, kupokea sakramenti ya upatanisho na kuomba huruma ya Mungu katika matendo yaliyotendeka kanisani hapo.
Jana, ilikuwa siku ya Ibada ya kutakatifuza iliyoanza kwa maandamano yaliyoongozwa na maaskofu, mapadri, mafrateri, mashemasi, watawa na watumishi pamoja na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki waliotembea umbali wa kilomita tatu kutoka Parokia ya Bikira Maria wa Fatma hadi Kanisa Kuu la Kiaskofu lililoko mtaa wa Mbugani Mjini Geita.
Maandamano hayo yalipokelewa na Kardinali Pengo katika lango wa kanisa hilo lililokuwa limefungwa kisha kulifungua na waandamanaji, wakiwemo viongozi wa Serikali pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela kuingia kanisani.
Ibada ilivyoanza
Mara baada ya kuingia kanisani, ilianza kwa Kardinali Pengo, kubariki maji ya baraka yaliyotumika kutakasa kanisa na kisha maaskofu kunyunyuzia maji hayo kwa waumini walioshiriki ibada waliokuwa ndani na nje ya kanisa, kisha kunyunyuzia kwenye kuta za kanisa.
Katika mahubiri yake, Kardinali Pengo alisema kinachotofautisha jengo la ibada na majengo mengine ni imani iliyojengeka miongoni mwa waumini.
Kardinali Pengo alisema kitendo kilichofanyika katika kanisa hilo kiliondoa thamani ya kanisa kwenye ibada ya kumuabudu Mungu.
Alisema pamoja na afya yake kutokuwa vizuri lakini amependa kuungana na waumini wengine kumuomba Mwenyezi Mungu asikie kilio chao na atakase eneo hilo upya.
“Wapendwa wanajimbo la Geita, matukio kama lililotokea ni ishara ambayo Mwenyezi Mungu anaitoa kwetu tuitafakari polepole, kujua mwenyezi Mungu anataka kutuambia kitu gani kwa tukio kama hili.”
Baada ya Ibada kumalizika, waumini walishiriki sakramenti takatifu kisha Kardinali Pengo na maaskofu wengine wakaibariki Tabenacro mpya na ikafuatiwa na ibada ya kuweka sakrameti ndani ya Tebanacro.
Ibada hiyo ya kuweka sakramenti iliongozwa kwa maandamano madogo ndani ya kanisa hadi nje ambapo Askofu wa Jimbo hilo, Flavian Kassala aliyebeba ‘Monstans’ (kifaa cha kubebea sakrament) aliongoza akifuatiwa na mapadri na kuzunguka ndani ya kanisa kisha nje na kurudi ndani.
Hatua hiyo ilihitimisha shughuli za kutakatifuza kanisa hilo.
Tunaweza kumsamehe lakini…
Katika salamu zake, Askofu Kassala aliwashukuru watu na madhehebu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walioungana nao mara tukio hilo lilipotokea, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.
Askofu Kassala aliliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuchunguza tukio hilo na kuonyesha mashaka ya kuwa mtuhumiwa alikuwa mlevi kwa kuwa kwa yaliyotendeka yalitendeka kimkakati na kwa mpangilio ili kuhakikisha kanisa linapata maumivu.
“Tunaamini alikuwa na akili timamu na alikusudia na kufikia wakati wa kutekeleza, tunaomba suala hili lifuatiliwe, yakiwemo maelezo tuliyotoa kama kanisa ushahidi wetu utumike, umekuwa shahidi wa kwanza wa tukio na baadhi ya uharibifu tumeshughudia ukitendeka kupitia dirishani, tuna ushahidi wa huyu mtu baadhi ya matendo sio ulevi, hata kama angekuwa mlevi asingeweza kufanya alichofanya,” alisema.
Askofu Kassala alisema kitendo cha kuruka mita mbili kwenda juu na kuvunja mtambo wa kumbukumbu za kamera unaonyesha ni mtu mwenye mafunzo au mapepo na kuomba uchunguzi wa kina ufanyike.
Alisema ili kurudisha kanisa katika utakatifu wake wametumia zaidi ya Sh60 milioni kuagiza vifaa vingine, ikiwemo Tebenacro kutoka nchini Italia.
Awali, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga alisema kama kanisa walisikitishwa na kitendo hicho kinachotia doa imani, lakini akasema masikitiko hayo hayapunguzi imani yao na kutangaza kumsamehe aliyehusika na matendo hayo na kumuombea wongofu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella alisema Serikali ilipokea kwa masikitiko kitendo kilichofanywa na mhalifu na kutoa salamu za pole kutoka kwa Rais Samia ambaye ameelekeza kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo yote ya ibada bila kujali imani.