Zuma ajitenga na ANC, aanzisha chama kipya

Muktasari:

  • Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ameanzisha chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK) ikimaanisha silaha ya Taifa na amesema hatakipigia kura chama cha ANC.

Johannesburg. Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amesema hatakipigia kura chama cha ANC katika uchaguzi ujao badala yake ameanzisha chama chake kipya, Umkhonto we Sizwe.

Zuma ni mmoja ya wapigania ukombozi wa Afrika Kusini, hususan kwa kujitoa kwake katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri nchini humo.

Kama mmoja wa vijana waliokulia ndani ya ANC, Zuma amefanya kazi mbalimbali hadi kuwa Rais wa ANC na Rais wa nchi na ni mmoja kati ya wapigania ukombozi wachache wa Afrika Kusini waliobaki hai.

Zuma ambaye amekuwa Rais kati ya mwaka 2009 - 2018, amesema itakuwa ni usaliti kuifanyia kampeni ANC inayoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa.

"Siwezi na sitaifanyia kampeni ANC ya Ramaphosa," amesema Zuma katika taarifa aliyoitoa kwa umma na kuripotiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Chama kipya cha Zuma kinaitwa Umkhonto we Sizwe (MK) ikimaanisha Silaha ya Taifa. Umkhonto we Sizwe ni sawa na kikundi cha kijeshi kilichoanzishwa ndani ya ANC wakati wa harakati za ukombozi.

Kikundi hicho ambacho Zuma naye alikuwa miongoni, kilipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi. Kilipigwa marufuku mwaka 1993 baada ya kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi na ANC chini ya Nelson Mandela ikashinda uchaguzi.

Zuma amesema ANC imebadilika na kuwa kitu ambacho hawakitambui. Amemtuhumu Rais Ramaphosa kwamba anakusudia kukiua chama hicho kwani amewaacha watu weusi wa Afrika Kusini na kuwakumbatia watu weupe nchini humo.

Zuma amejiweka pembeni wakati nchi hiyo ikitarajia kufanya uchaguzi mkuu mwakani ambao wachambuzi wa duru za siasa za Afrika Kusini wanaeleza utakuwa na ushindani mkali.

Zuma ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa, hasa kwa wananchi wa hali ya chini. Kujitenga kwake na ANC kutakididimiza chama hicho kwenye uchaguzi ujao ambao Rais Ramaposa anatarajia kugombea muhula wake wa pili.

Zuma alijiuzulu urais mwaka 2018 kutokana na shinikizo kutoka ndani ya ANC. Aliyekuwa Makamu wa Rais, Ramaphosa akachukua nafasi yake ya urais, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe alifungwa mwaka 2021 kwa kutoheshimu amri ya Mahakama baada ya kutokwenda kutoa ushahidi mahakamani kama alivyotakiwa.

Kufungwa kwake kulisababisha maandamano makubwa ya kitaifa nchini humo ambapo watu 350 walipoteza maisha. Maandamano hayo yalidhihirisha nguvu na ushawishi wa Zuma huko Afrika Kusini.

Alitumikia kifungo chake kwa miezi miwili kabla ya kuachiwa huru kwa kile kilichoelezwa ni sababu za kiafya.