Waziri auawa na mlinzi wake

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano ya Viwanda nchini Uganda, Kanali mstaafu Charles Okello Engola enzi za uhai wake.
Kampala. Waziri wa Nchi anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano ya Viwanda nchini Uganda, Kanali mstaafu Charles Okello Engola ameuawa kwa kupigwa risasi asubuhi ya leo na mlinzi wake akiwa nyumbani kwake.
Tukio hilo limetokea leo Mei 2, 2023 jijini Kampala katika Kitongoji cha Kyanja anakoishi waziri huyo ambapo bado chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.
Naibu msemaji wa polisi wa Kampala, Luke Owoyesigire amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku maofisa usalama wakiimarisha ulinzi katika eneo yalipotokea mauaji hayo.
“Ndiyo kuna mauaji eneo la Kyanja. mlinzi amempiga risasi bosi wake,” Owoyesigire ameiambia Daily Monitor katika mahojiano mafupi kwa njia ya simu.
Spika wa Bunge la Uganda Anita Among, naye pia amethibitisha kifo cha waziri huyo alipokuwa akiongoza kikao cha mashauriano leo asubuhi.
“Leo asubuhi, nilipata taarifa za kusikitisha kuwa Mhe Engola amepigwa risasi na mlinzi wake na baada ya tukio hilo na yeye kujipiga risasi. Roho yake ipumzike kwa amani. Huo ulikuwa mpango wa Mungu. Hatuwezi kubadilisha chochote,” Bi Among alisema.
Waziri wa Jinsia, Betty Amongi ni miongoni mwa maofisa wa serikali ambao tayari wamefika nyumbani kwa Engola huko Kyanja.