Kifo cha kamanda Iran chazua hofu Mashariki ya Kati
Kiongozi wa wanamaji wa Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) wa Iran, Alireza Tangsiri. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kifo cha Alireza Tangsiri pamoja na vigogo wengine wa Iran, kimeongeza hofu ya kuendelea mzozo wa Mashariki ya Kati, huku miundombinu muhimu ikiendelea kuharibiwa kwa mashambulio ya anga.
Dar es Salaam. Hofu ya kuendelea kwa vita Mashariki ya Kati imeongezeka baada ya kushambuliwa kwa Kiongozi wa Jeshi la Wanamaji la Iran Machi 26, 2026.
Alireza Tangsiri, kiongozi wa wanamaji wa Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) wa Iran, aliripotiwa kushambuliwa na Jeshi la Israel.
Reuters na Al Jazeera zimeripoti kuwa Jeshi la Israel (IDF) katika shambulizi hilo, lilidai kumlenga kamanda huyo kama sehemu ya mashambulio makuu dhidi ya ngome za juu za jeshi la Iran.
Iran ilithibitisha kifo cha kiongozi huyo Machi 30, 2026, ikisema alifariki kutokana na majeraha makali aliyoyapata katika shambulio hilo.
Tangsiri alikuwa kiongozi mwenye jukumu la kudhibiti usalama wa majini, akiwa sehemu muhimu katika mkakati wake wa ulinzi katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya mafuta duniani.
Kifo chake kinahofiwa kupunguza uwezo wa operesheni za baharini za Iran na mikakati ya ulinzi wa njia za maji ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, vifo vya vigogo wengine wa Iran, ikiwemo Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa Iran aliyeuawa Februari 28, 2026, na Ali Larijani, mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa aliyeuawa Machi 17, 2026, vimeathiri muundo wa kisiasa na mikakati ya diplomasia ya nchi hiyo.
Aidha, mawaziri na makamanda wengine pia wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi tofauti ya anga yanayofanywa na Marekani na Israel, hali inayoonesha mwelekeo wa vita vya kulenga viongozi wa juu na miundombinu muhimu badala ya mapigano ya kawaida.
Matamko yachochea hofu
Matamko ya viongozi wa Marekani, Iran na Israel bado yanaonyesha kila upande unasalia katika msimamo wake mkali.
Mashirika ya habari ya kimataifa, yakiwemo The Guardian na Reuters, yameripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump ameendelea kusisitiza hatua za kijeshi dhidi ya Iran na kutahadharisha kulenga miundombinu muhimu ikiwa mashauriano ya kisiasa hayatafanikiwa.
Iran, kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi imedai itaendelea kushambulia maeneo ya kijeshi ya adui zake kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora.
Kwa upande wake, Israel imeendelea kutumia ulinzi wa anga dhidi ya makombora yanayotoka Iran, huku ikisisitiza kuwa lengo lake ni kudumisha usalama wa Mashariki ya Kati na kuzuia Iran kuendeleza mradi wa silaha za nyuklia.
Athari zinavyoendelea duniani
Wakati mvutano ukiendelea kushika kasi, tayari mashambulizi hayo yameathiri usafirishaji wa mafuta na miundombinu muhimu duniani, hali iliyosababisha mfumuko wa bei ya nishati.
Shirika la habari la Ujerumani la DW limeripoti uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu nchini Iran, ikiwemo kuporomoshwa kwa daraja la B1, daraja refu zaidi Mashariki ya Kati, baada ya mabomu yaliyodaiwa kufanywa na Marekani na Israel huko Karaj, magharibi mwa Tehran.
Daraja hilo lilikuwa sehemu ya mradi wa barabara kuu unaounganisha Tehran na kaskazini mwa Iran, hivyo kuvunjwa kwake kumeathiri biashara kwa baadhi ya masoko kutofikika na kuathiri maisha ya watu.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mashambulizi yanayofanywa kushinikiza taifa hilo kuacha misimamo yake hayatabadilisha hatua hiyo.
"Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia hayatawalazimisha Wairan kujisalimisha," aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X.
Aidha, vita hivyo pia vimeathiri masoko ya nishati duniani, kusababisha bei za mafuta kuongezeka na hatari ya kupanda kwa gharama za maisha ya raia, hali inayoongeza mashinikizo ya kimataifa.
Tayari mataifa kadhaa ya Afrika, yakiwemo Afrika Kusini, Zambia na Namibia, yametangaza kufuta au kupunguza kodi na ushuru kwenye mafuta, huku Tanzania ikitangaza kuanza uchunguzi ili kuchukua hatua kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta na tishio la kupanda kwa gharama za usafiri na usafirishaji.
Kwa mujibu wa The Washington Post, matukio haya yamepunguza uwezekano wa mazungumzo ya haraka ya amani, huku vifo vya viongozi wakuu wa Iran vikihofiwa kuchochea uwezekano wa mzozo kuendelea kwa muda mrefu zaidi.
Kwa sasa, dunia yote inashuhudia tishio la ongezeko la gharama za maisha kutokana na vita hivyo, hasa hatari za kijeshi na kimkakati katika maeneo ya Hormuz na kando ya mipaka ya Mashariki ya Kati.